Technology

TCRA yazindua usajili wa simu wa kielektroniki, utahusisha watumiaji wa simu kupigwa picha

Mamlaka ya mawasiliano nchini, TCRA, makampuni ya simu na mamlaka ya vitambulisho, NIDA, imezindua zoezi la usajili wa simu kwa njia ya kielektroniki.

IMG_0312
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma akiongea na waandishi wa habari Jumanne hii

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma, amesema zoezi hilo litasaidia kupata taarifa sahihi za watumiaji wa simu nchini.

“Sasa hivi zoezi litakuwa kiteknolojia zaidi. Utakuwa ukipigwa picha na simu. Kwahiyo uso huwezi ukafeki,” amesema Profesa Nkoma.

Ameongeza kuwa zoezi hilo litasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa udanganyifu uliopo kwenye matumizi ya simu nchini na hakutakuwa na urahisi wa mtu kutumia jina la bandia pamoja na picha isiyokuwa yake.

Profesa Nkoma amesisitiza kuwa zoezi hilo halimaanishi kuwa ni usajili mpya wa sim card bali ni uhakiki wa taarifa za watumiaji wa simu nchini na linamhusu kila mmoja.

Kwa upande wake Rene Meza ambaye pamoja na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, ni mwenyekiti wa chama cha watoa huduma za mawasiliano nchini, MOAT alisema zoezi la usajili wa simu nchini limeingia kwenye hatua nyingine ya juu zaidi.

IMG_0316
Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha watoa huduma za mawasiliano nchini, MOAT akiongea na waandishi wa habari

“Ni kwa kutumia teknolojia, na tena ni kwa smartphone ambayo wakala wa usajili ataipata kwa si zaidi ya shilingi laki moja ambayo itamsaidia kuchukua picha ya mteja anayetaka kusajili sim card yake. Mchakato huo hautumia zaidi ya dakika tano,” alisema Meza.

Meza amesema usajili huo utafanyika nchi nzima na wameifanyia uhakiki teknolojia hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu na tayari kuna vituo zaidi ya 5000 vinavyofanya usajili huo mpya.

Wateja watatakiwa kuonesha vitambulisho vinavyokubalika kufanikisha zoezi hilo na utagharimu shilingi 1000 tu.

Kwa upande wake mamlaka ya vitambulisho nchini, NIDA, imedai kuwa vitambulisho vya uraia vitalazimika kutumika zaidi ili kupata taarifa sahihi za watumiaji wa simu.
NIDA imesema imeboresha pia utoaji wa vitambulisho hivyo wa Dar es Salaam ambapo wananchi wakiwasilisha viambatanisho vinavyotakiwa watakuwa wakivipata ndani ya siku 7.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents