Habari

TCU yaongeza muda wa udahili wa wanafunzi vyuo vikuu

Tume ya vyuo vikuu nchini TCU, imesema kumekuwa na ushindani mkubwa kwa baadhi ya nafasi ambazo zimeombwa na wanafunzi ambao wanataka kujiunga na vyuo vikuu nchini hali inayofanya zoezi la udahili huo kuongezewa muda.

tcu-620x375

Akizungumza na mwandishi wa TBC ofisini kwake, kaimu katibu mtendaji, Profesa Eliuther Mwageni, amesema zoezi la udahili wa wanafunzi kwa mwaka 2016/2017 limeongezewa muda kwa awamu ya tatu hadi Jumapili, Oktoba mwezi huu.

“Katika kuomba watu wengine walikuwa hawaangalii kwa mfano kuna course ambazo zinataka huyu mwanafunzi awe amefaulu hesabu kwa mfano, kweli mnaweza mkalingana lakini kama haukufaulu hesabu hiyo utakuwa umechagua course ambayo haikuhusu. Kuna course nyingine zinataka hata mwanafunzi afaulu hesabu alipo kuwa form four kwahiyo wewe unaweza ukaangalia matokeo ya sasa alipokuwa form six lakini mahitaji ya ile course yanahitaji matokeo yaliyo yalivyokuwa form four,”alisema Mwageni.

Aidha Prof Mwageni alizungumzia kuongezwa kwa zoezi hilo amesema imetokana na wanafunzi wengi kuomba course ambazo tayari zimekwisha jaa.

“Programu ambazo zilipata watu wengi waombaji wengi, ni pamoja na udaktari na sheria watu wengi waliziomba hizo,lakini nafasi katika maeneo haya sio nyingi kama idadi ya waombaji na wengine kwa namna moja ama nyingine walikosea namna ya kujaza. Kwa mfano kuna watu ambao walikuwa hawana sifa za hizo course lakini waliomba, kwahiyo hao tukawapa fursa ya pili,ambayo tuliimaliza mwisho wa mwezi Septemba. Lakini bado kukatokea na kundi lingine la watu, kuna watu ambao wapo 6000, ambao wamemaliza kidato cha sita, ambao bado vile vile walikuwa wamefanya makosa yale yale, walikuwa bado wanatafuta zile course ambazo tayari zina ushindani mkubwa. Sasa tukasema tusiwanyime nafasi kwasababu wana sifa ya kusoma chuo kikuu,” aliongeza.

Hadi sasa waombaji wa kujiunga na nafasi ya vyuo vikuu ambao wamesajiliwa na TCU ni zaidi ya wanafunzi elfu 58.

Kwa upande wake mkurugenzi msaidizi wa habari,elimu na mawasiliano,Cosmas Mwaisoba kutoka bodi ya mikopo nchini amekiri kuchelewa kwa mikopo kwa wanafunzi.

“Ni kweli tofauti na miaka mingine, taarifa za wale ambao wananufaika na mikopo zimechelewa kidogo. Zimechelewa kidogo kwasababu wiki hii na wiki ijayo ndiyo vyuo vingi vitakuwa vinafungua programu ya orientation. Hii imechangiwa kutokamilika kwa taratibu fulani fulani. Unajua zoezi la utaoji wa mkopo linahusisha upatikanaji wa taarifa kutoka kwa wadau mbalimbali kwa mfano taarifa za udahili,” alifafanua Mwaisoba.

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents