Habari

Tetemeko lazikumba Dodoma ,Arusha

MIJI ya Arusha na Dodoma imekumbwa na tetemeko la ardhi juzi na jana, huku wananchi wa Arusha wakikesha nje ya nyumba zao kwa kuhofia usalama wao.

Paul Sarwatt, Arusha


MIJI ya Arusha na Dodoma imekumbwa na tetemeko la ardhi juzi na jana, huku wananchi wa Arusha wakikesha nje ya nyumba zao kwa kuhofia usalama wao.


Tetemeko hilo lilitikisa maeneo kadhaa ya mji wa Arusha kwa zaidi ya mara mbili na kusababisha watu wengi kukesha nje ya nyumba zao kwa kuhofia usalama wa maisha yao.


Mapema juzi mchana, tetemeko hilo lilitikisa maeneo kadhaa ya Mkoa wa Arusha ingawa halikuleta madhara kwa maisha ya binadamu na mali zao.


Tetemeko hilo lilitikisa tena usiku majira ya saa 5:38 kwa sekunde kama tano katika maeneo ya Kimandoru, Baraa, Moshono, Ilboru na maeneo ya tambarare yaliyoko magharibi mwa mlima Meru ambao ni wa pili kwa urefu katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Saa 6:10 za usiku tetemeko hilo lilitikisa tena kwa sekunde na kutia hofu zaidi kwa wakazi wengi ukanda huo wa kaskazini. Kwa mtikisiko huo wa pili, watu wengi walilazimika kutoka nje ya nyumba zao na kuamua kukabiliana na baridi kali ya Arusha kwa kuhofia kuwa tetemeko kubwa lingetokea hivyo kuhatarisha usalama wao.


“Tumelazimika kukaa nje kwa sababu tangu mchana kumekuwa na tetemeko na usiku huu limerudia tena ingawa hakuna madhara makubwa lakini linaweza kurudi na nguvu kubwa,” alisema Fulgance Massawe mkazi wa Baraa katika Manispaa ya Arusha.


Kwa muda huo, wakazi wengi walionekana kupigiana simu na kutumiana ujumbe mfupi kujuliana hali na kuulizana iwapo kulikuwa na madhara yaliyosababishwa na tetemeko hilo.


Kwa mujibu wa taarifa Kituo cha Utafiti cha Geological Survey Earthquakes Hazards cha Denver Colorado, Marekani iliyopatikana kwenye mtandao tetemeko la kwanza juzi mchana lilitokea saa 8:24 za mchana.


Chanzo cha mtikisiko huo inahisiwa kuanzia kilomita 85 kusini magharibi mwa Arusha hasa karibu na Mlima Oldonyo Lengai ambao bado una volkano iliyo hai.


Mjini Dodoma, tetemeko hilo lilitokea jana alfajiri lakini halikusababisha madhara yoyote kwa binadamu na mali zake.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents