Habari

TRA yanasa sukari ya Tanzania iliyobadilishwa kuwa ya Kenya

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoani Mara imekamata sukari kutoka viwanda vya Kagera na Kilombero ikiwa inabadilishiwa kwenye mifuko ya Kiwanda cha Sukari cha Son Sugar cha Kenya ili kusafirishwa kwenda nchini humo.

Sukari hiyo ilikamatwa kwenye ghala la mfanyabiashara Maselo Ghati kwenye mpaka wa Sirari. Mifuko 353 ya sukari kutoka kiwanda cha Kagera Sugar ilikamatwa ikihamishiwa kwenye mifuko ya kiwanda cha Son Sugar ili kupelekwa Kenya.

Meneja wa TRA Mkoa wa Mara, Ernest Nkangaza, alisema operesheni inayoendeshwa na mamlaka hiyo kwa ushirikiano wa wananchi ndiko kulikofanikisha kukamatwa sukari hiyo.

Aidha alisema katika tukio hilo, watu 20 walikamatwa pamoja na mmiliki ambao wanaendelea kuhojiwa na polisi sababu za kuibadilisha sukari ya Tanzania ionekane inazalishwa Kenya wakati kukiwa na changamoto ya uhaba wa sukari na kupanda bei nchini.

“Katika ghala la mfanyabiashara huyu, tumekuta pia mifuko tupu ya Kiwanda cha Son Sugar cha Kenya pamoja na mifuko ya sukari ya Kagera Sugar na Kilombero, jambo ambalo linaonyesha kuna mchezo mchafu unaofanywa. “Hili siyo jambo jema hasa ikizingatia kwa sasa kuna shida ya upatikanaji wa sukari na kupanda bei yake,” aliongeza Nkangaza.

Sambamba na kukamata sukari hiyo serikali iliwataka wafanyabishara waache kufanya mambo kinyume na taratibu kwa kuwa mamlaka hiyo imejipanga kudhibiti wote wasio waaminifu.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents