Trafiki akamatwa na `rushwa` ya 3,000/-

Askari polisi wa kikosi cha Usalama barabarani, maarufu kama trafiki, Sauda Kaijage (39), ameachishwa kazi kutokana na kutuhumiwa kumuomba dereva wa daladala jijini Dar es Salaam, rushwa ya sh. 3,000

Na Hellen Mwango



 


Askari polisi wa kikosi cha Usalama barabarani, maarufu kama trafiki, Sauda Kaijage (39), ameachishwa kazi kutokana na kutuhumiwa kumuomba dereva wa daladala jijini Dar es Salaam, rushwa ya sh. 3,000.

Kutokana na hilo, askari huyo jana aliburuzwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka hilo.

Aidha, mahakama ilimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. 3,000 kila mmoja.

Kaijage alisomewa shtaka lake mbele ya Hakimu Mkazi Benadetha Beda wa mahakama hiyo.

Mwendesha Mashtaka, Inspekta Msaidizi wa Polisi, Francis Mboya, alidai kuwa Machi 31, mwaka huu eneo la Kamata, kati ya Barabara ya Nyerere na Kilwa jijini, mshtakiwa aliomba hongo ya Sh. 3,000 kutoka kwa Samadu Mzallah.

Ilidaiwa kuwa Mzallah ni dereva wa daladala yenye namba za usajili T 781 ALS, na kwamba mshtakiwa aliomba fedha hizo baada ya gari hiyo kuwa na makosa ya kiusalama barabarani.

Mboya alidai kuwa katika shtaka la pili, siku ya tukio la kwanza katika kituo kidogo cha polisi gerezani, mshtakiwa alipokea Sh. 3,000 kutoka kwa Mzallah kwa nia ya kumuachia bila kumlipisha faini kama sheria inavyotaka.
Mshtakiwa alikana shtaka hilo.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umeshakamilika ambapo mshtakiwa atasomewa maelezo ya awali Mei 22, mwaka huu.

Mshtakiwa alitimiza masharti ya dhamana na yuko nje hadi Mei 22, mwaka huu.

Wakati huohuo, Gloria Michael (31), mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, amefikishwa mahakamani hapo kujibu shtaka la wizi wa dola 500 za Marekani.

Ilidaiwa kuwa Aprili 22, mwaka huu eneo la Kinondoni jijini, mshtakiwa akiwa kama mtumishi wa ndani, aliiba fedha hizo kutoka kwa muajiri wake, Viviane Abbolt.

Gloria alikana shtaka hilo na kesi itatajwa tena Mei 19, mwaka huu.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents