Habari

Trump agusia Wamarekani wanaotaka kusafiri katika majimbo yalio athirika zaidi na Virusi vya Corona

Rais Donald Trump wa Marekani  amejizuwia kutangaza  karantini kwa  ajili  ya  maeneo  hatarishi ya  virusi  vya  Corona mjini  New York, New Jersey na  Connecticut, badala  yake  ameelekeza  usiku wa Jumamosi  kuwa ,taarifa kali ya  ushauri kwa wanaotaka  kusafiri , itolewe kupunguza kusambaa  kwa  virusi  hivyo.

USA Corona-Pandemie | Trump Statement (Reuters/J. Ernst)

Mike Pompeo aliandika  katika  ukurasa wa  Twita kuwa kituo cha udhibiti wa  magonjwa  ya kuambukiza CDC anawataka  wakaazi  wa  majimbo  hayo  matatu , “kujizuwia na safari zisizo  za  lazima katika  muda wa  siku  134 zijazo.”

Suala  la karantini lilipendekezwa na magavana, ikiwa  ni Pamoja  na gavana wa  chama  cha  Republican Ron DeSantis wa  jimbo  la Florida, ambaye  alitaka  kuzuwia  wasafiri  kutoka  maeneo yaliyoathirika  zaidi  kwenda  katika  majimbo  yao.

Lakini  hatua  hiyo  ilikumbana  na  ukosoaji  mkubwa  kutoka  kwa viongozi  wa  majimbo  hayo yanayotajwa  kuwa  na  maambukizi makubwa, ambao  wameonya  kuwa  hali  hiyo  italeta  taharuki kubwa  katika  jamii  ambayo  tayari  imeathirika  kwa  virusi.

Kwa mujibu wa chombo cha habari cha DW, Trump  alitangaza  kuwa  amefikia  uamuzi  huo  baada  ya mashauriano  na  kikosi  kazi  cha  Ikulu  ya  White house kinachoongoza hatua  zinazochukuliwa  na  serikali  kuu na magavana  wa  majimbo  hayo  matatu. Amesema  amekiagiza  kituo cha udhibiti  na  kuzuwia  magonjwa , CDC , kutoa ushauri  mkali wa kusafiri, utakaotekelezwa na  magavana, kwa  kushauriani na serikali  kuu. Ameongeza  kuwa  karantini  haitakuwa  lazima.

Athari katika  sekta za  maisha ya jamii

Zaidi ya  theluthi  moja  ya  watu wote  duniani  wamefungiwa hawatoki  nje wakati  virusi vinasababisha  athari  kubwa  katika karibu  kila  sekta  ya  maisha  ya  jamii, vikifuta  mamlioni  ya  ajira, mbinyo katika  huduma za  afya na  kuleta shinikizo  kubwa  katika hazina za  taifa kwa  miaka  mingi  ijayo.

Duniani , idadi  ya  vifo  imepita 30,000 na  maafisa  katika  baadhi ya  nchi wanasema  hali  mbaya  zaidi  bado  inakuja.

Lakini  katika  mji  wa  Wuhan  nchini  China, ambako  virusi  hivyo vilijitokeza  kwa  mara  ya  kwanza , maafisa  wamechukua  hatua  za awali  kuelekea  katika  hali  ya  kawaida, kwa  kufungua  sehemu  ya mji  huo  baada  ya  zaidi ya  miezi  miwili  kuutenga  kabisa  mji  huo wenye  wakazi  wapatao  milioni 11. Ukilinganisha  na  Marekani, Mataifa  ya  Ulaya  yameathirika  zaidi  kwa  msingi wa uwiano wa watu, ambapo  vifo 20,059 vimetokea.

Vifo kutokana na virusi vya corona  vimepindukia 20,000 barani Ulaya kufikia Jumamosi, ambapo Italia na Uhispania kila moja imeripoti  zaidi ya vifo 800 kwa siku moja, na Trump amejizuwia kuiwekea New York karantini.

Italia yazidi kuathirika  na  virusi vya corona

Italia  siku  ya  Jumamosi  ilitangaza  vifo  vipya  889, na  kufikisha zaidi  ya  vifo 10,000. Uhispania , ambayo  ina  idadi  ya  pili  ya  juu ya  vifo  kutokana  na  virusi  vya  corona, iliongeza  vifo 832  katika jumla  ya  vifo 5,812. Madrid  imeimarisha hatua  ya  kuzuwia  watu kutoka  nje , na  kuzuwia  shughuli zote  ambazo  si  za  lazima, licha ya  kuwa  maafisa  wamesema  janga  hilo nchini  humo  linaonekana kufikia  kilele  chake.

Urusi  ambayo imeripoti viwango vya  chini  vya  maambukizi, imesema itafunga  mipaka  yake Jumatatu katika  juhudi  za kupunguza  kusambaa  kwa  virusi. Zaidi ya mambukizi 640,770 ya virusi  vya  Corona  yamerekodiwa  rasmi  duniani  kote tangu kuzuka  kwa  virusi  hivyo mwishoni  mwa  mwaka  jana, kwa  mujibu wa  idadi  iliyotolewa  na  shirika  la  habari  la  Ufaransa  AFP.

Nchini  Ufaransa, ambayo  imeshuhudia  vifo karibu 2,000, waziri mkuu Edouard Philippe amenya  kuwa  mapambano  ndio  kwanza yanaanza. Wiki  mbili  za  kwanza  za  mwezi  Aprili zitakuwa  ngumu zaidi  kuliko  wiki  mbili  zilizopita, amesema.

Uingereza  imefikisha  watu 1,000  waliofariki  kutokana  na  ugonjwa huo COVID-19.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents