Habari

Trump awafukuza kazi maofisa hawa wawili waliotoa ushahidi kwenye kesi yake

Trump awafukuza kazi maofisa hawa wawili waliotoa ushahidi kwenye kesi yake

Rais Donald Trump amewafuta kazi maafisa wawili waandamizi waliotoa ushahidi dhidi yake katika kesi ya kutokuwa na imani naye iliyokuwa inamkabili.

Balozi wa Marekani kwa Muungano wa Ulaya, Gordon Sondland, amesema “Nimeambiwa kwamba rais anataka nirudi nyumbani mara moja”.

Awali, Luteni kanali Alexander Vindman, mtaalamu mkuu katika masuala ya Ukraine, alisindikizwa kutoka nje ya Ikulu ya Marekani.

Inasemekana kwamba Bwana Trump amesema anataka kufanya mabadiliko baada ya bunge la Seneti kumuondolea mashtaka yaliyokuwa yanamkabili Jumatano.

Katika kura ya kihistoria iliyopigwa, Bunge la Seneti limeamua kutomuondoa rais huyo wa 45 wa Marekani madarakani kwa madai yaliyokuwa yameibuliwa dhidi yake kutokana na mahusiano yake na Ukraine.

Kaka yake Luteni kanali Vindman ambaye pia ni pacha mwenzake, Yevgeny Vindman, wakili mwandamizi katika baraza la Usalama la taifa pia alirejeshwa katika idara ya jeshi Ijumaa.

Vipi kuhusu kurejeshwa kwa balozi Sondland?

Katika taarifa iliyotolewa na wakili wake, bwana Sondland amesema: “Nimearifiwa hii leo kwamba rais anataka nirudi nyumbani mara moja baada ya kunivua wadhifa wa balozi wa Marekani kwa Muungano wa Ulaya.

“Nashukuru kwa fursa ambayo Rais Trump alinipa ya kuhudumia taifa, pia namshukuru Waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo kwa kuniunga mkono, na tena shukrani zangu ziwaendee wafanyakazi wote wa ubalozini wa Muungano wa Ulaya kwa utalaamu wao na kujitolea kwao.

Gordon Sondland testifying before the House Intelligence CommitteeHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionGordon Sondland amepigwa kalamu kama balozi wa Marekani kwa Muungano wa Ulaya

“Najivunia kile ambacho tumefikia. Kazi yetu hapa imekuwa kielelezo chema kwa taaluma yangu,” Bwana Sondland amesema.

Lakini je Vindman ameondolewa vipi?

Mshauri wa Luteni kanali Vindman, David Pressman, ameiambia BBC kwamba mteja wake ametolewa nje ya Ikulu ambako amekuwa akifanya kazi yake kwa uadilifu kwa nchi yake na kwa rais wake”.

“Hakuna raia yeyote wa Marekani anayejiuliza kwanini raia huyu amefutwa kazi, kwanini nchi hii sasa ina mtu mmoja tu mwenye nguvu anayeongoza Ikulu ya Marekani,” taarifa hiyo imesema.

“Luteni Vindman alifutwa kazi baada ya kusema ukweli Heshima yake, kujitolea kwake kufanya kilicho sawa, kulitia hofu wenye nguvu.”

Taarifa hiyo imeongeza: ” Ukweli umemgharimu Alexander Vindman kazi yake, taaluma yake, na faragha yake.”

National Security Council Director for European Affairs Alexander Vindman arrives for a closed-door deposition at the US Capitol in Washington, DC on October 29, 2019Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionAlexander Vindman alikuwa mtaalamu wa masuala ya Ukraine ndani ya Baraza la Usalama wa Taifa Marekani

Luteni kanali Vindman alifika kazini Ijumaa katika Ikulu kama kawaida.

Trump na Utawala wake umesema nini?

Wakati anaondoka Ikulu Ijumaa kuelekea North Carolina, Bwana Trump aliwaambia wanahabari: “Sina furaha na yeye [Luteni kanali Vindman].

“Munadhani kwamba nitakuwa namfurahia? hapana.”

Na hadi kufia sasa Rais Trump bado hajasema lolote kuhusiana na hilo.

Kulingana na vyanzo vya Ikulu ya Marekani, Luteni kanali Vindman amekuwa akitarajia kuhamishwa. Kwa wiki kadhaa sasa amekuwa akiwaarifu wafanyakazi wenzake kwamba yuko tayari kurejea katika idara ya ulinzi, ambako bado anatekeleza majukumu yake ya kijeshi.

Mapema Ijumaa, Waziri wa Ulinzi Mark Esper aliwaambia wanahabari kwamba idara yake inawakaribisha wafanyakazi wake wote waliokuwa wamepewa majukumu mengine.

“Na kama nilivyosema, tunalinda maafisa wetu kutokana na matukio ya ulipizaji kisasi ama kitu chochote kile cha aina hiyo,” Bwana Esper ameongeza.

Sondland na Vindman walimkasirisha vipi Trump?

Walipokuwa wanatoa ushahidi wao bungeni Novemba mwaka jana, Bwana Sondland alikuwa muwazi kabisa katika ushahidi wake kwamba ujio wa rais Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya Marekani ulifikiwa kwa masharti tu kwamba Kyiv itaanzisha uchunguzi ambao utamsaidia Rais Trump kisiasa.

“Je kulikuwa na makubaliano ya kunufaika kwa namna yoyote ile?” Sondland aliulizwa. “Kama nilivyosema awali, kwa simu iliyopigwa kutoka Ikulu na mkutano katika Ikulu, jibu ni ndio.”

Wakati huo, Bwana Sondland alikuwa akifanyakazi na wakili binafsi wa Trump, Rudy Giuliani, kuhusiana na sera ya Ukraine kwa mwongozo wa rais.

Luteni kanali Vindman pia naye alitoa ushahidi Novemba mwaka jana. Alisema alikuwa na wasiwasi baada ya kusikia mazungumzo ya simu ya Trump ambayo hayakuwa yakawaida Julai 25, na Rais wa Ukraine.

Simu hiyo ndio chanzo cha kura ya kutokuwa na Imani na Trump mnamo mwezi Desemba na Bunge wa Wawakilishi kwasababu ya kutumia vibaya mamlaka na kuingilia bunge.

Wabunge wa Democratic walisema kwamba rais alizuia msaada wa Marekani kwa Ukraine kwa manufaa yake ya kisiasa.

Baada ya kuulizwa ni vipi alikabiliana na hofu ya kutoa ushahidi wake, Luteni kanali Vindman alisema: “Ni kwasababu hii ni Marekani… na hapa ukweli ni muhimu sana.”

Siku moja kabla ya kuwatimua, Trump alisema kwamba mapacha hao Vindman wameshirikiana na maadui zake wa kisiasa katika Ikulu.

Hisia zilizoibuka kwa uamuzi wa Trump ni zipi?

Eliot Engel, mwenyekiti wa Democratic wa kamati ya bunge ya mambo ya nje, alisema katika taarifa: Bila shaka hili ni jambo la aibu.

“Lakini pia hili ni jambo ambalo tunastahili kulitarajia kutoka kwa rais aliyekuwa amepigiwa kura ya kutokuwa na Imani naye, ambaye chama chake kimeamua yeye ni mwenye nguvu kuliko sheria na hawajibiki kwa yeyote.”

Lakini mbunge wa Republican Thomas Massie akasema angekuwa amemfuta kazi Luteni kanali Vindman.

“Yeye amevujisha taarifa wala hajafichua,” Massie amesema. Kwasasa mkuu wa jeshi hapokei maagizo yoyote kutoka kwa Luteni kanali!”

Je Mick Mulvaney ndiye atakayefuata?

Katika taarifa yake kupitia vyombo vya habari Ijumaa, Trump alisema taarifa za kwamba kaimu mkuu wa wafanyakazi Mick Mulvaney atapigwa kalamu ni za uwongo.

“Nina uhusiano mzuri na Mick, “Trump amesema.

Kuna tetesi kuwa mbunge wa North Carolina Mark Meadows ndiye atakaechukua nafasi ya bwana Mulvaney.

Meadows, ambaye anastaafu kama mbunge wa wawakilishi ambako anaongoza chama chenye msimamo mkali cha Freedom Caucus, alisafiri na Trump katika ndege ya rais Ijumaa.

Acting White House Chief of Staff Mick MulvaneyHaki miliki ya pichaREUTERS

Katika Mkutano na wanahabari usiokuwa wa kawaida Oktoba mwaka jana, Mulvaney alionekana kumhusisha Trump na madai ya ufisadi na Ukraine.

Kaimu huyo wa wafanyakazi aliwaambia wanahabari: “Huwa tunafanya hivyo kila wakati.” Inasemekana kwamba Trump alikasirishwa sana na hatua hiyo.

Baadate, bwana Mulvaney akarejelela matamshi yake na kuandika taarifa iliyosema: “Naomba kueleweka, hakukuwa na mpango wowote uliodhamiria manufaa ya kisiasa kati ya usaidizi wa kijeshi kwa Ukraine na uchunguzi wowote wa uchaguzi wa 2016.”

Former US congressman Joe Walsh in Des Moines, Iowa, on 31 January 2020Haki miliki ya pichaEPA
Image captionJoe Walsh aliyejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea wa urais ndani ya chama na kusema kwamba chama cha Republican kimekuwa “dhehebu”

Nani mwengine huenda analengwa?

Aliyekuwa mbunge wa Illinois Joe Walsh, mmoja kati ya waliokuwa wanampinga Trump katika uteuzi wa kugombea urais wa chama cha Republican, Ijumaa alitangaza kwamba amejiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Bwana Wash, ambaye alipata asilimia 1 pekee ya kura Jumatatu katika jimbo la Iowa caucus, ameliambia shirika la habari la CNN kwamba chama cha Republican cha sasa, “kimekuwa ‘dhehebu”.

“Ninataka kumuondoa Trump. Kwasababu ninaamini kwamba yeye ni tishio kwa nchi hii. Lakini hakuna anayeweza kumuondoa kwenye urais ndani ya chama cha Republican. Hakuna anayeweza kumshinda katika uchaguzi.”

Bill Weld, aliyekuwa gavana wa jimbo la Massachusetts, ndiye pekee aliyesalia katika chama cha Republican anayetaka kumuondoa Rais Trump katika uteuzi wa mgombea atakaye peperusha bendera ya Republican, ambaye atatafuta kuchaguliwa tena Novemba.

Chanzo BBC.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents