Siasa

Trump rais wa kwanza Marekani kupigiwa kura na wabunge kukosa imani naye

Bunge la uwakilishi nchini Marekani limepiga kura ya kutokuwa na imani dhidi ya rais Donald Trump kwa kuchochea ghasia zilizosababisha uvamizi wa jumba la bunge la Capitol.

Wabunge 10 wa chama cha Republican walishirikiana na wenzao wa chama cha Democrat kupitisha kura hiyo ya kumshtaki rais kwa 232 dhidi ya wabunge 197 waliopinga hatua hiyo.

Ni rais wa kwanza katika historia ya Marekani kupigiwa kura ya kutokuwa na imani mara mbili ama kushtakiwa kwa makosa ya uhalifu na bunge hilo la Congress.

Rais Trump ambaye ni mwanachama wa Republican sasa atakabiliwa na kesi katika bunge la seneti ambapo iwapo atapatikana na hatia huenda akapigwa marufuku kushikilia wadhfa wowote wa ofisi ya umma.

Bwana Trump anaachia madaraka tarehe 20 mwezi Januari kufuatia kushindwa kwake katika uchaguzi mkuu mwezi Novemba uliomtangaza Joe Biden mshindi.

Bunge hilo linalodhibitiwa na wabunge wengi wa Democrat lilipiga kura siku ya Jumatano saa kadhaa baada ya mjadala mkali huku walinzi wa kitaifa wakiimarisha usalama ndani na nje ya jumba la bunge hilo.

Shirika la kijasusi nchini Marekani FBI limeonya kwamba kuna uwezekano wa kuzuka kwa maandamano katika majimbo yote 50 kabla ya kuapishwa kwa rais mteule Joe Biden wiki ijayo.

Nancy Pelosi

Katika kanda ya video iliotolewa baada ya kura hiyo kupigwa , bwana Trump aliwataka wafuasi wake kusalia watulivu lakini hakuzungumzia kwamba alikuwa amepigiwa kura ya kutokuwa na imani naye bungeni.

‘Ghasia na uharibifu hauna nafasi katika taifa letu…hakuna mfuasi wangu ambaye angependelea kufanyika kwa ghasia za kisiasa’ , alisema akionesha huzuni na mwenye kutaka maridhiano.

Mashtaka hayo ni ya kisiasa na sio ya uhalifiu.

Rais huyo alituhumiwa na bunge la Congress kwa kuchochea ghasia ziizosababisha uvamizi wa Jumba la bunge la Capitol kufuatia hotuba yake aliyotoa tarehe sita mwezi Januari katika mkutano wa hadhara nje ya Ikulu ya Whitehouse.

Aliwataka wafuasi wake kuandamana kwa amani na uzalendo ili sauti zao zisikike, lakini pia kukabiliana na uchaguzi ambao alidai kwamba ulikumbwa na udanganyifu mkubwa.

Kufuatia matamshi hayo ya rais Trump , wafuasi wake walivunja na kuingia katika Jumba la Capitol , na kuwalazimu wabunge kuahirisha kikao cha kuidhinisha ushindi wa rais mteule Joe Biden na baadaye kujificha.

Jumba hilo lilifungwa kwa muda na watu watano wakafariki wakati wa ghasia hizo.

Kifungu cha sheria kumshtaki rais huyo kilisema kwamba bwana Trump alirejelea mara kadhaa matamshi ya uwongo akidai kwamba matokeo ya uchaguzi huo wa urais yalikuwa yamekumbwa na udanganyifu na kwamba hayafai kukubaliwa.

Yalisema kwamba alirejelea madai hayo na kutoa wito kwa wafuasi wake ,hatua iliowachochea na kusababisha utovu wa nidhamu katika jumba la Capitol uliosababisha vurugu na vifo.

Wiki iliopita Wanachama 139 wa Republican walipiga kura ya kupinga kuidhinishwa kwa matokeo hayo ya uchaguzi wa 2020 na kushindwa kwa rais Trump.

Wabunge wa Congress walitoa taarifa zao wakiunga mkono na kupinga kura hiyo katika bunge hilo ambapo walijificha chini ya viti na kuvalia barakoa wakati ambapo waaandamanaji walijaribu kuingia ndani wiki iliopita.

Spika wa Bunge Nancy Pelosi , mwanachama wa Democrat alisema kwamba ”rais wa Marekani alichochochea ghasia , uasi dhidi ya taifa letu.Lazima aondolewe. Yeye ni mtu hatari kwa taifa hili ambalo tunalipenda sote”

Mbunge wa chama cha Democrat Julian Castro alimuita rais Trump ‘kama mtu hatari zaidi kuwahi kushikilia ofisi ya rais”.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents