Habari

TUCTA kujadili ongezeko la ada Chuo Kikuu

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) linatarajia kuijadili Serikali katika vikao vyake na kuunda mtandao utakaoshirikisha asasi za jamii, kushinikiza ada za vyuo vikuu zisiongezwe.

Na Joseph Lugendo

 

 

 

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) linatarajia kuijadili Serikali katika vikao vyake na kuunda mtandao utakaoshirikisha asasi za jamii, kushinikiza ada za vyuo vikuu zisiongezwe.

 

 

 

Akizungumza na Majira makao makuu ya TUCTA Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Msaidizi wa Shirikisho hilo, Bw. Nicholas Mgaya, alisema ongezeko hilo la takribani asilimia 80 ya ada katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, linaonesha jinsi Serikali inavyojichanganya.

 

 

 

“Serikali inataka kuanza kuajiri wafanyakazi wenye diploma na kuendelea, huoni kwamba hapa wataalamu watapungua?,” alihoji na kubainisha kwamba kuna wageni wenye shahada za kwanza katika fani za Biashara (BCom) ambao wanaajiriwa nchini kama wataalamu na kuchukua nafasi za Watanzania.

 

 

 

“Tujiulize wenyewe, hivi ile miaka ambayo watu walitoka vijijini na kuja kusoma chuo kikuu itarudi?,” alihoji Bw. Mgaya na kuongeza kwamba ataishangaa Serikali ambayo Baraza lake la mawaziri linatoka vijijini, iwapo itaidhinisha ongezeko hilo la ada.

 

 

 

Bw. Mgaya alisema nguvu ya Tanzania kutaka kuwa na ushiriki wenye uwiano mzuri katika soko la Afrika Mashariki itapungua zaidi, kwa kuwa itakuwa na wasomi wachache kuliko Kenya na Uganda, ambazo hata hivyo, ndizo zinazoongoza kwa kupeleka wanafunzi wengi vyuo vikuu.

 

 

 

Aidha, alitaadharisha kwamba ongezeko hilo likikubaliwa kuanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), litasababisha vyuo vingine vya umma vikiwamo vya Mzumbe na Sokoine (SUA), kuongeza ada ambayo itaathiri wafanyakazi wengi wa ngazi za chini ya ukurugenzi na wakulima.

 

 

 

“Elimu ya juu inaelekea kutolewa kwa ‘privilage’ (upendeleo) ambapo watu wachache tu ndio watakaoipata,” alisema Bw. Mgaya na kuongeza kwamba kama Serikali itakurupuka na kukubali ada hiyo, Watanzania watajuta.

 

 

 

Ongezeko hilo la ada UDSM linatarajiwa kuanza rasmi Septemba mwaka huu, kwa wanafunzi watakaofaulu mtihani wa kidato cha sita unaoendelea kote nchini, baada ya kuthibitishwa na Serikali.

 

 

 

Kiwango cha chini cha ada kinatarajiwa kupanda kutoka sh. 722,000 mpaka sh. milioni 1.3 na kiwango cha juu kitapanda kutoka sh. milioni 1.22 mpaka sh. milioni 2.52.

 

 

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents