Habari

TUCTA yashauri kufanyika uhakiki wa vyeti katika sekta binafsi

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) limeunga mkono utaratibu wa serikali wa kuhakiki vyeti vya watumishi wa umma na kutaka utaratibu huo ufanyike pia kwenye sekta binafsi.

nicholas-mgaya
Katibu Mkuu wa shirikisho (TUCTA), Nicholaus Mgaya.

Akizungumza na gazeti la Habari Leo Jumatatu hii , Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Nicholaus Mgaya alisema uhakiki huo utasaidia kuondoa watumishi wengi wasiowajibika kwa kukosa sifa na kuhakikisha wale wenye sifa ndio wanapata ajira.

“Tunaomba huu uwe utaratibu wa nchi nzima, maeneo yote yaguswe na uhakiki huu kwa sababu ukweli uko wazi kwa sasa kuna watanzania wengi tena wasomi wa hali ya juu hawana ajira lakini nafasi zao zimezibwa na watu wasio na sifa,” alisisitiza Mgaya.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao na Mawasiliano Tanzania (Tewuta), Yunus Ndaro alisema vyama vya wafanyakazi vinaunga mkono hatua hiyo ya serikali kwani itasaidia kurejesha heshima ya ajira nchini.

Alisema sekta binafsi pia ni sehemu ya Tanzania na inajiendesha pia kwa kufuata Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Mwaka 2004, hivyo nayo inapaswa kuhakikiwa ili kuhakikisha inafuata misingi, kanuni na sheria za nchi.

“Mfano zipo kampuni nyingi za simu baadhi yake zikiwa binafsi zinaingiza wafanyakazi wageni kutoka nje ya nchi, wengi wakiwa hawana sifa, kupitia uhakiki huu haya yote yatavumbuliwa,” alisisitiza Ndaro.

Hivi karibuni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Iringa (UOI), Askofu Dk Owdenburg Mdegella pamoja na kuipongeza serikali kwa kuanzisha utaratibu huo, naye aliomba kufanyike hadi sekta binafsi ili kupunguza ongezeko la vyeti bandia.

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents