Habari

Tume yaundwa kusaka kaburi la Faru John

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda Tume kuchunguza taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha Faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti Serengeti pamoja na kutafuta kaburi la faru huyo.

Amesema timu hiyo ya wataalamu tayari imeshafika Sasakwa VIP Grumeti kwa ajili ya kutafuta kaburi na kuchukua vinasaba vya masalia ya Faru John na kisha watakwenda kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kuchukua vinasaba vya watoto wake na kisha kuvilinganisha na pembe hiyo kubaini kama kweli pembe aliyopelekewa ni ya faru huyo ama la.

Majaliwa aliyasema hayo Jumapili hii wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha. Ziara hiyo ililenga kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuona utoaji wa huduma kwa wananchi.

Desemba 9 mwaka huu nyumbani kwake Oysterbay, Dar es Salaam, Majaliwa alipokea taarifa iliyoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha Faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti ambapo aliahidi kuifanyia kazi zaidi.

Alisema baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Julai 10, 2016 afya ya faru huyo ilidorora na alikufa Agosti 18, mwaka huu. Hata hivyo, aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kumletea nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru huyo kutoka kwenye hifadhi hiyo.

Waziri Majaliwa alisema, “Tume niliyounda kwa ajili ya uchunguzi wa faru John imetua VIP Grumeti Serengeti kujiridhisha kama kuna kaburi la faru John na kama lipo wachukue vinasaba na baada ya hapo watakwenda Kreta na kuchukua vinasaba vya watoto wa faru John na kuvipima kwa pamoja. Lengo ni kutaka kubaini kama pembe iliyowasilishwa kwangu Desemba 9 mwaka huu ni ya faru John,” alisema.

BY: EMMY MWAIPOPO

CHANZO: HABARILEO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents