Burudani

Tumejifunza nini kwa mwamko huu tulioonesha kwa Idris na Happiness?

Diamond Platnumz, Idris Sultan na Happiness Watimanywa wamesaidia kuonesha wazi nguvu tuliyonayo Tanzania.

Happiness Watimanywa

Kutoka kwenye ushindi wa tuzo tatu za Channel O uliompa Diamond sifa nyingine kwenye CV yake hadi kwenye ushindi wa pili wa Tanzania kwenye shindano la Big Brother Africa uliompa utajiri wa zaidi ya shilingi milioni 514 mpiga picha Idris Sultan na sasa tukishuhudia Happiness Watimanywa akiyapita mataifa makubwa duniani kwenye kura za People’s Champion Award ya shindano la Miss World.

Mafanikio hayo yote hayajaja kirahisi, bali yamekuja na umoja, mshikamano, ubishi na upendo wa wananchi wa Tanzania wakipewa support na mataifa mengine yenye mapenzi mema nasi. Ushindi huo umetupa fundisho kuwa tukiamua tunaweza.

Nguvu iliyooneshwa na Watanzania wa kila aina, mastaa, wafanyabiashara, wanafunzi, wanaume kwa wanawake na watu wa kila rika katika kusisitizana kumpigia kura Happy ni ya kipekee na inatia moyo. Huo ni upendo ambao hatujaona katika nchi zingine. Kile kilichofanyika kwa Happy kimewavutia hata majirani zetu na wanatamani wao pia wangekuwa na umoja huu tulionao Tanzania.

Hebu angalia Instagram jinsi jina na picha za Happiness zilivyoenea! Wasanii wa muziki na wa filamu karibu wote hawajaishia kumpigia debe tu, bali wao pia wamepiga kura. Dada zake, Happiness Magese, Faraja Kotta, Nancy Sumari, Wema Sepetu na wao pia tumeona walivyokuwa mstari wa mbele kumpigia debe.Huu ni upepo wa aina yake.

Sisi sote na serikali kwa msisitizo, tunajifunza nini kwenye mapinduzi haya ya kwenye mitandao ya kijamii? Labda kuisaidia serikali, mapinduzi hayo yanaifundisha kuwa tasnia ya burudani ndio imetokea kuwa kitu pekee kinacholitangaza jina la Tanzania. Si michezo hususan soka ambayo licha ya serikali kumwaga pesa nyingi kwa kuajiri makocha na mambo mengine, inayoitangaza Tanzania.

Burudani kimegeuka kitu pekee kinachoiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia. Hivyo serikali inapaswa kuanza kuiangalia tasnia hiyo kwa jicho la kujali zaidi. Serikali inapaswa kuanza kuwasadia vijana hawa wanaojituma wenyewe kwa hali na mali. Inatakiwa kuanza kutenga fungu kusaidia harakati kama hizi.

Kama inavyofanywa kwa timu ya taifa ya soka ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikivuna matokeo mabovu au timu ya Tanzania kwenye mashindano ya riadha yakiwemo yale ya Jumuiya ya Madola ambayo hurudi mikono mitupu, serikali inapaswa kuanza kutoa msaada wa kifedha pia kusupport harakati hizi za vijana wa Tanzania kwenye mashindano kama haya ya burudani na urembo.

Tukumbuke kuwa kabla Happiness hajaenda London, mama yake aliwahi kulalamika kuwa kamati ya Miss Tanzania haikuwa imekamilisha kumwandalia baadhi ya mahitaji yake. Kama familia yake isingekuwa na uwezo kiasi, kuna mambo mengi ambayo asingeweza kuyafanya mrembo huyu. Leo hii tunaona anavyoliweka juu jina la Tanzania na serikali inayosaidiwa kutagwaziwa vivutio vyake vya kitalii haijaweka mchango wake wowote.

Hata kama serikali ikiwageuzia mgongo mashujaa hawa, inatosha kuona tu kuwa umoja wetu unaweza kutufanya kuonekana taifa kubwa lenye nguvu. Tuendelee hivi hivi, kuna mengi makubwa tutayafikia.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents