Michezo

Tunakuja sasa kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi– Azam FC

Klabu ya Azam FC, huenda ikaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara endapo itashinda katika mchezo wake ujao dhidi ya Lipuli ya Iringa siku ya Jumapili utakao chezwa uwanja wa Azam Complex.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika mtandao wa klabu hiyo zinaeleza kuwa inanafasi kubwa ya kukaa kileleni mwa Ligi hiyo yenye jumla ya timu 16 baada ya kupata alama tatu muhimu katika mchezo wao ujao.

Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, ina nafasi nyingine ya kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) endapo itaichapa Lipuli ya Iringa Jumapili hii, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.

Lakini huenda pia ikajihakikishia nafasi hiyo, kama Mtibwa Sugar iliyokuwa kileleni kwa pointi zake tisa itapoteza mchezo wake siku hiyo watakapokuwa ugenini kwa mara ya kwanza msimu huu kuivaa Ruvu Shooting.

Azam FC iliyojikusanyia pointi saba katika nafasi ya tatu, ikishinda itafikisha pointi 10 na kuiacha Simba iliyonafasi ya pili kwa pointi zake nane, ambayo ilipata sare ya mabao 2-2 jana dhidi ya Mbao.

Mabingwa hao waliofanikiwa kushinda mechi mbili na sare moja, wanaendelea na mazoezi makali kwenye viunga vyake vya Azam Complex na juzi ilijipima ubavu dhidi ya Friends Rangers na kuilaza mabao 6-0.

Kocha Mkuu, Aristica Cioaba, amekuwa akiwapa mbinu mbalimbali wachezaji kuhakikisha wanakuwa imara kupambana vilivyo na wapinzani wao na kuvuna pointi zote tatu kwa kushinda kila mchezo.

Azam FC inayodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora ya NMB na Tradegents, itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi iliyopita ya ligi kwa kuichapa Kagera Sugar bao 1-0, lililofungwa na Mbaraka Yusuph.

Lipuli ambayo imejikusanyia jumla ya pointi tano ikiwa nafasi ya nane kwenye msimamo, imefanikiwa kutoka suluhu na Ruvu Shooting katika mchezo uliopita, ikiwa ni sare ya pili msimu huu huku wakiwa wameshinda mchezo mmoja na kutopoteza.

Kihistoria hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Azam FC kupambana na Lipuli kwenye ligi, lakini itakumbukwa ya kuwa timu hizo ziliwahi kucheza mchezo wa kirafiki katika maandalizi ya msimu huu mkoani Iringa na Azam FC kuibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 4-0.

Mabao hayo yaliwekwa kimiani na beki Yakubu Mohammed, washambuliaji Wazir Junior, Yahya Zayd na kiungo mng’arisha timu Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye amekuwa na kiwango kizuri cha kufunga mabao kwa misimu hii miwili.

Azam FC inatisha

Mpaka sasa kitakwimu, Azam FC ndio timu pekee ambayo haijaruhusu wavu wake kuguswa tokea msimu huu uanze Agosti 26 mwaka huu ikiwa imecheza dakika 270 (sawa na mechi tatu), ambapo safu ya ulinzi imekuwa ikiongozwa vema na kipa kutoka nchini Ghana, Razak Abalora aliyepachikwa jina na mashabiki la ‘mikono 100’ kutokana na ubora wake langoni.

Abalora amekuwa akilindwa vilivyo na mabeki wa kati wenye ubora wa hali ya juu, nahodha msaidizi, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, beki wa kulia Daniel Amoah, wa kushoto Bruce Kangwa, viungo wakabaji nahodha Himid Mao ‘Ninja’, Stephan Kingue na Frank Domayo.

Hadi inaingia kwenye mchezo huo, Azam FC ina majeruhi wawili tu ambao ni wa muda mrefu, winga Joseph Kimwaga na mshambuliaji Shaaban Idd.

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents