Siasa

Tutamshangaa atakayempinga Kikwete…

CCMChama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitashangaa kama atatokea mwanachama wa kupambana na Rais Jakaya Kikwete, katika uteuzi wa kugombea urais mwaka 2010

Na Mashaka Mgeta



 


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitashangaa kama atatokea mwanachama wa kupambana na Rais Jakaya Kikwete, katika uteuzi wa kugombea urais mwaka 2010.

Kauli hiyo imekuja huku kukiwa na tetesi za kuwapo viongozi waandamizi, wanaojiandaa kuchukua fomu, ili wateuliwe kuwania nafasi hiyo ya juu katika uongozi wa nchi.

Baadhi ya vyombo vya habari, vilikariri vyanzo vyao mbalimbali hivi karibuni, vikidai kuwa miongoni mwa wana-CCM hao wanaouataka urais kabla Kikwete hajamaliza kipindi cha pili, walishiriki katika kinyang`iro cha kuwania kuteuliwa na chama hicho mwaka 2005.

Katibu wa Idara ya Uchumi na Fedha wa CCM, Bw. Amos Makala, alisema chama hicho kimejiwekea utaratibu wa Rais aliyepo madarakani, kutumikia vipindi viwili, hivyo Rais Kikwete, atagombea tena urais mwaka 2010.

“Nitamshangaa mwanachama atakayejitokeza kushindana na Rais Kikwete kuwania uteuzi wa kugombea urais mwaka 2010, kwa sababu tuna utamaduni wetu uliojenga mazoea, kwamba Rais atatumikia vipindi viwili,“ alisema.

Bw. Makala, alikuwa akihojiwa katika kipindi cha midani za siasa na uchumi kilichorushwa hewani na kituo cha luninga cha Star TV mwishoni mwa wiki iliyopita.

Licha ya kuwepo utaratibu huo ambaao kimsingi haupo kikatiba, kwa mujibu wa Bw. Makala, aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Dk. Ghalib Bilal, alichukua fomu za kuwania Urais wa visiwa hivyo mwaka 2005.

Wakati Dk. Bilal akichukua fomu hizo, Rais Amani Abeid Karume wa Zanzibar, alikuwa anaingia katika awamu ya pili ya uongozi wake.

Hata hivyo, jina la Dk. Bilal, liliondolewa katika vikao vya juu vya uteuzi katika CCM, vilivyofanyika mjini Dodoma, hivyo kuliwezesha jina la Rais Karume kupita peke yake.

Bw. Makala, alidai kwamba utaratibu wa kumwachia Rais kuongoza kwa vipindi vinavyotambuliwa kikatiba, unachangia kuimarisha utulivu ndani ya chama na serikali yake, hali inayopaswa kuigwa na mataifa mengine, ikiwemo Zimbabwe.

Taifa hilo mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo na Uchumi Kusini mwa Afrika (SADC), linakabiliwa na mzozo wa kisiasa, uliotokana na Uchaguzi Mkuu ambao hata hivyo, mshindi wa urais bado hajapatikana.

Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo, anashutumiwa na baadhi ya watu, taasisi za kijamii na mataifa, akidaiwa kung`ang`ania madarakani.

Hata hivyo, Bw. Makala, aliunga mkono sera ya kurejesha ardhi kwa wazawa, na kutoridhishwa na mpango wa kuinyima misaada nchi hiyo.

Alifananisha hatua ya kuinyima Zimbabwe misaada na kuhoji kasi ndogo ya maendeleo yake kuwa sawa na kumfungia mtu mawe miguuni na kumtaka akimbie.

Kwa upande mwingine, Bw. Makala, alisema CCM kupitia awamu ya tatu ya mpango wa uboreshaji chama, inaendelea kujiimarisha katika ngazi za chini kwenye jamii, hali inayoweka mazingira bora ya kushinda chaguzi za mwakani na 2010.

Uchaguzi wa serikali za vitongoji, vijiji na mitaa utafanyika mwaka ujao wakati Uchaguzi Mkuu wa Rais na wabunge utafanyika mwaka 2010.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents