Shinda na SIM Account

Tuzo ya mchezaji bora wa ligi kuu Tanzania Bara kutua Msimbazi

Kamati ya Tuzo za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), imekamilisha uteuzi wa wachezaji watatu watakao wania tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/2018.

Wachezaji watatu waliobaki katika kinyang’anyiro hicho ni Emmanuel Okwi, John Bocco na Erasto Nyoni wote kwa wekundu wa Msimbazi Simba SC, ambapo kamati ya Tuzo hiyo ya Mchezaji Bora imeandaa utaratibu wa kupiga kura kuwashirikisha Wahariri wa Habari za Michezo, manahodha wa timu za Ligi Kuu ya Vodacom na makocha wa timu za Ligi Kuu.

Pia kamati imekamilisha uteuzi wa wachezaji watakaowania tuzo katika kategori mbalimbali kwenye sherehe hizo za Tuzo ya Mchezaji Bora wa VPL itakayofanyika ukumbi wa Mlimani, City Dares Salaam Juni 23 mwaka huu.

Tuzo 16 zinatarajiwa kutolewa siku hiyo, ambapo baadhi ni za kikanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara, ambazo tayari washindi wake wamefahamika, ambazo ni bingwa, mshindi wa pili, mshindi wa tatu, mshindi wa nne na mfungaji bora.

Ukiacha hizo tano za kikanuni, zipo tuzo 10 ambazo zimefanyiwa kazi na Kamati ya Tuzo kulingana na takwimu mbalimbali za ligi hiyo, ambapo tuzo moja nyingine ya Mchezaji Bora chini ya umri wa miaka 20 (Tuzo ya Ismail Khalfan), inayohusisha vikosi vya vijana vya timu za Ligi Kuu yenyewe inaendelea kufanyiwa kazi kwa vile mashindano yanaendelea mkoani Dodoma na itakapokamilika watatangazwa wateule watatu.

Tuzo nyingine zitakazotolewa siku hiyo ni Timu yenye Nidhamu inayowaniwa na Kagera Sugar, Simba na Mtibwa Sugar, wakati Mchezaji Bora Chipukizi inawaniwa na Shaaban Idd Chilunda, Yahya Zayd (Azam) na Habibu Kiyombo (Mbao).

Mwamuzi Msaidizi Bora inawaniwa na Helen Mduma, Mohammed Mkono na Ferdinand Chacha, wakati Mwamuzi Bora wateule ni Elly Sasii, Jonesia Rukyaa na Hans Mabena.

Tuzo ya Kipa Bora wanaowania ni Aron Kalambo (Prisons), Aishi Manula (Simba) na Razack Abalora (Azam), huku Kocha Bora wateule ni Abdallah Mohamed (Prisons), Zuberi Katwila (Mtibwa) na Pierre Lechantre (Simba).

Goli Bora ni Seif Karihe (Lipuli) na Shaaban Idd Chilunda (Azam) ambaye ameingiza mabao mawili.

Tuzo nyingine ambazo zitatolewa Juni 23 ni Mchezaji wa Heshima ambayo licha ya kuwa kamati ina majina ya wachezaji mbalimbali inaoona wanastahili tuzo kwa mwaka husika, lakini haitangazi majina hayo, isipokuwa hutaja jina la aliyepewa tuzo siku ya sherehe.
Pia kutakuwa na kikosi bora (VPL Best Eleven), ambacho kitatangazwa siku ya sherehe.

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW