Michezo

Tuzo za Ballon d’Or kufanyika leo usiku, Messi Ronaldo na van Dijk, matokeo yaliyovuja yanamuonyesha huyu ndio mshinda

Tuzo za Ballon d'Or kufanyika leo usiku, Messi Ronaldo na van Dijk, matokeo yaliyovuja yanamuonyesha huyu ndio mshinda

Mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or kwa mwaka 2019 anatarajiwa kutangazwa leo usiku, na kwa mara nyengine tena kwa mwaka huu Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Virgil van Dijk watakuwa wanachuana vikali.

Kwa kipindi cha miaka 10, tokea 2008 mpaka 2017 tuzo hiyo maarufu zaidi ya wasakata kandanda duniani ilitawaliwa na washambuliaji hatari katika kizazi cha sasa Messi na Ronaldo, kila mmoja wao akishinda mara tano.

Kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa la Croatia Luka Modric alivunja ufalme wa Messi na Ronaldo baada ya kunyakua tuzo hiyo mwaka jana.

Mlinzi wa klabu ya Liverpool, Van Dijk ambaye ameshinda Kombe la Klabu Bingwa Ulaya msimu uliopita anaonekana kutishia kuendeleza machungu kwa Ronaldo na Messi kwa mara ya pili mfululizo.

Hii itakuwa mara ya tatu kwa Messi Ronaldo na Van Dijk kukutana uso kwa uso katika kuwania tuzo kubwa mwaka huu.

Messi, Ronaldo na Van Dijk
Image captionHii ni mara ya tatu kwa Messi, Ronaldo na Van Dijk kuwania tuzo kwa pamoja mwaka huu.

Mara ya kwanza walikutana katika tuzo za Mchezaji Bora wa Ulaya (Uefa) mwezi Agosti ambapo Van Dijk aliibuka na ushindi.

Mara ya pili wakaminyana katika tuzo za Mchezaji Bora wa Fifa ambapo Messi aliibuka mshindi.

Je Messi anasubiri kutangazwa tu?

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za vyombo vya habari vikubwa barani Ulaya, kuna tetesi kuwa matokeo ya tuzo hizo yamevuja na kuonesha kuwa Messi ameshinda.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Messi anayecheza katika klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Argentina amepata alama 446, akifuatiwa na Van Dijk mwenye alama 382.

Mshambuliaji wa Liverpool Mohammed Salah anatajwa kuwa katika nafasi ya tatu, Ronaldo nafasi ya nne huku mshambuliaji mwengine wa Liverpool Sadio Mane akaikamilisha tano bora kwa mwaka huu.

Matokeo rasmi hata hivyo yanatarajiwa kutolewa baadae hii leo.

Luka ModricMwaka jana, kiungo wa Real Madrid Luka Modric alikuwa mchezaji wa kwanza tofauti na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kushinda tuzo hiyo baada ya miaka 10.

Akiongea na BBC baada ya kushinda mwaka jana, Modric alisesema tuzo yake ni zawadi kwa wachezaji wote ambao waliikosa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

“Labda huko nyuma kuna wachezaji ambao walistahili kushinda Ballon d’Or kama Xavi, Andres Iniesta au [Wesley] Sneijder lakini sasa watu wameamka a wanaanza kuangalia wachezaji wengine,” amesema.

Modric aliwasifia Ronaldo na Messi kama “wachezaji bora kabisa”, na kuongeza “hivyo ushindi wangu huu unamaanisha kuwa nimefanya vitu vikubwa sana uwanjani mwaka huu, na ndio maana 2017-18 umekuwa ni mwaka wangu.”

Tano Bora ya Ballon d’Or mwaka jana

1. Luka Modric (Real Madrid and Croatia)

2. Cristiano Ronaldo (Juventus and Portugal)

3. Antoine Griezmann (Atletico Madrid and France)

4. Kylian Mbappe (Paris St-Germain and France)

5. Lionel Messi (Barcelona and Argentina)

Ballon d’Or ni nini?

Tuzo ya Ballon d’Or imekuwa ikitolewa nchini Ufaransa kila mwaka toka 1956, na mshindi wake wa kwanza alikuwa mchezaji kutoka Uingereza Stanley Matthews.

Awali tuzo hiyo ilikuwa ni kwa wachezaji wa Ulaya tu kabla ya kufanyika mabadiliko mwaka 1995 na kujumuisha wachezaji wa mataifa yote duniani, mradi wanasakata kandanda katika vilabu vya Ulaya.

Orodha ya majina ya wachezaji 30 bora huandaliwa na baadae kupigiwa kura na wanahabari wa michezo kutoka sehemu tofauti duniani, ambapo kila nchi hupiga kura moja.

Kutoka mwaka 2010 mpaka 2015 tuzo hiyo iliunganishwa na ile ya Fifa lakini zilitengana mwaka 2016 ambapo Fifa ilianza kundaa tuzo zao wenyewe.

Washindi wa Ballon d’Or : Ronaldo & Messi walitawala kuanzia 2008
2007 Kaka Cristiano Ronaldo Lionel Messi
2008 Cristiano Ronaldo Lionel Messi Fernando Torres
2009 Lionel Messi Cristiano Ronaldo Xavi
2010 Lionel Messi Andres Iniesta Xavi
2011 Lionel Messi Cristiano Ronaldo Xavi
2012 Lionel Messi Cristiano Ronaldo Andres Iniesta
2013 Cristiano Ronaldo Lionel Messi Franck Ribery
2014 Cristiano Ronaldo Lionel Messi Manuel Neuer
2015 Lionel Messi Cristiano Ronaldo Neymar
2016 Cristiano Ronaldo Lionel Messi Antoine Griezmann
2017 Cristiano Ronaldo Lionel Messi Neymar
2018 Luka Modric Cristiano Ronaldo Antoine Griezmann

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents