Habari

TvT yaibua mambo makubwa bungeni

MJADALA mzito umezuka bungeni juu ya uhalali wa Taasisi ya Utangazaji nchini (TUT) kutumia kodi ya wananchi kushindana na vyombo vya habari binafsi chini ya muungano wao wa MOAT.

na Martin Malera, Dodoma


MJADALA mzito umezuka bungeni juu ya uhalali wa Taasisi ya Utangazaji nchini (TUT) kutumia kodi ya wananchi kushindana na vyombo vya habari binafsi chini ya muungano wao wa MOAT.


Aliyeanzisha mjadala huo alikuwa ni Mbunge wa Mbeya Vijijini, Richard Nyaulawa (CCM), ambaye pia ni mmiliki wa vyombo vya habari vya Business Times.


Akichangia hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, iliyosomwa na Waziri Muhammed Seif Khatib, mbunge huyo alisema ushindani wa vyombo vya habari vya serikali na binafsi hauko sawa kwa madai kuwa vyombo vya serikali vinatumia pesa ya walipa kodi kushindana na vyombo binafsi, hali ambayo ni kinyume cha sheria.


Alisema sehemu kubwa ya biashara ya vyombo vya habari ni matangazo, lakini matangazo mengi yanakwenda kwenye vyombo vya serikali na kuvinyima vyombo vya habari binafsi.


Nyaulawa alisema hata matangazo machache yanayoletwa kwenye vyombo vya habari binafsi, bado yanakatwa kodi kubwa, lakini kodi hiyo hiyo ndiyo inayotumiwa na TUT kushindana na vyombo binafsi.


“Kwanza vyombo vya habari binafsi vinatoa kodi na kodi hiyo inatumika kukuza vyombo vya habari vya serikali. Hapa vyombo vya habari binafsi vinajikaanga kwa mafuta yake vyenyewe, kwa hali hii hakuwezi kuwa na ushindani ulio sawa,” alisema Nyaulawa.


Alisema vyombo hivi vikifa, ajira nyingi zitapotea kwani sekta hiyo ina zaidi ya watu 10,000 waliopata ajira na kuendesha maisha yao kwa kutegemea vyombo vya habari binafsi.


Akitolea mfano wa moja ya mchezo mchafu wa TUT, Nyaulawa alisema kuwa, vyombo vya habari binafsi chini ya muungano wao wa MOAT, viliomba zabuni ya kutangaza mashindano ya mpira nchini Uingereza kwa sh milioni 70, lakini TUT ilitangaza zabuni hiyo hiyo kwa sh milioni 200 ambazo ni fedha za walipa kodi na kushinda zabuni hiyo.


“Sisi tunasema huku ni kuua ushindani wa vyombo vya habari, kama serikali imeamua kujitoa kwenye biashara kama tunavyoelezwa, iache kutoa ruzuku kwa TUT kushindana na sisi, vinginevyo kama TUT inapata ruzuku, basi ifanye shughuli nyingine kama ya kutoa elimu vijijini, kueleza sera za nchi, elimu ya kilimo na hata kutafsiri baadhi ya sheria na vyombo vya habari binafsi viachwe vifanye biashara,” alisema Nyaulawa.


Kwa upande wake, Mbunge wa Newala, George Mkuchika (CCM), alipingana na Nyaulawa kwa kusema MOAT ina wivu na mafanikio ya TUT hasa katika kipindi kifupi baada ya kuingia Tido Mhando.


Alisema hakuna ubaya kwa TUT kutumia kodi ya wananchi kufanya biashara ya ushindani na vyombo binafsi, kwani hata katika nchi jirani ya Kenya, Afrika Kusini na hata Idhaa ya Kiswahili ya BBC nayo inajiendesha kwa mtindo wa TUT.


“Mimi naipongeza sana serikali kuiruhusu TUT ifanye biashara na nampongeza Tido Mhando kwa kuiwezesha TUT kupata zabuni hiyo. Kwa nini TUT kupata zabuni hiyo inakuwa nongwa?” alihoji Mkuchika.


Mbunge wa Ilala, Mussa Hassan Zungu, yeye alitoa mpya wakati akichangia hoja hii alipoanza kwa kusema ‘ Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza aliyemrejesha Tido nchini, Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.”


Aliendelea: “Tido ameibadilisha kabisa TvT, vipindi vyake vina mvuto, kelele zote zinazopigwa dhidi ya TvT ni wivu tu,” alisema Zungu.


Mbunge mwingine aliyechangia hoja hiyo ni Mudhihir Mohamed Mudhihir ambaye aliwalaumu MOAT kwa kutanguliza faida mbele na akataka hilo lisiwe sababu ya kuzuia ushindani na TUT.


Alisema kuwa vyombo binafsi vinapaswa kutambua kuwa, wafanyakazi wa TUT wanalipwa mishahara midogo ikilinganishwa na wale wa vyombo binafsi.


Mudhihir alisema kwa hali hiyo, TUT bila kujiendesha kibiashara, itashindwa kuhimili ushindani na ndiyo maana kwa muda mrefu imeshindwa kufanya vizuri kutokana na ufinyu wa fedha.


“Mishahara ya TUT ni midogo, kwa hiyo kwa kufanya hivi, TUT itaweza kuleta wafanyakazi wake bungeni na baadaye wataweza hata kujiunga na wenzao wa vyombo binafsi kuingia pale Chako ni chako na kuchoma nyama, hivyo tuiache TUT ifanye kazi katika ushindani wa kibiashara,” alisema Mudhihir.


Akizungumza jana jioni, Waziri Khatib aliungana na wabunge wengine katika kuitetea TUT na akasema serikali itaendelea kuipa ruzuku hadi hapo itakapoweza kujiendesha kama ilivyo kwa magazeti yake ya Daily News na Sunday News.


Aidha, Khatib alitumia fursa hiyo kuisoma makala ya mwandishi Deodatus Balile, iliyochapishwa katika gazeti hili toleo la Jumapili iliyopita, ambayo pamoja na mambo mengine ilieleza kuhusu matatizo ya MOAT.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents