Diamond Platnumz

Uchambuzi: Ngoma mpya ya Diamond itahit lakini….Huu ni mtazamo wetu

Umetoka kuzinguana na demu wako, sorry mpenzi wako kiasi kwamba akili haifikirii straight tena, kiasi ambacho unaamua kwenda kwenye baa ya jirani kupiga mtungi ili upunguze mawazo. Unaenda na unaagiza bia kadhaa na mzinga mmoja ili ukuweke sawa. Wakati pombe imeshaanza kupanda kichwani na kuanza kupunguza ile picha ya ulichofanyiwa na mpenzi wako, unasikia wimbo mzuri ukipigwa kwenye spika kuukuu za baa hiyo ya jirani lakini unaweza kusikia maneno yote.

Unagundua kuwa ni wimbo mpya wa Diamond na kama kawaida yake unamsikia akilalamikia mapenzi. Unaingiwa na hamu ya kutaka kujua ni wimbo gani kijana huyu katoa tena. Wakati unasikiliza kwa makini inasikika chorus yenye maneno yanayojirudia rudia: Nataka Kulewa, Nataka Kulewa kisha anamalizia kwa kusema ‘Zikipanda nimwage radhi’.

Wimbo unakugusa kwakuwa unaelezea hali kama uliyonayo ambayo imekufanya uende kunywa pombe ili upate ujasiri wa kukabiliana na jambo zito lililopo mbele yako. Kama ukiusikia wimbo huu ukiwa kwenye mazingira hayo bila shaka utakukuna sana. ‘Nataka Kulewa’ utawagusa wengi wenye mikasa ya kusalitiwa na wapenzi wao na hivyo kuitumia pombe kama kitu cha kuwapunguzia mzigo wa mawazo kichwani.

Kwa haraka haraka wimbo huu ni muendelezo wa wimbo wa awali wa Diamond,‘Mawazo’. Kama unakumbuka katika Mawazo Diamond anasikika akisema kama angekuwa na pesa angekunywa hata pombe ili apunguze mawazo. Kwa muendelezo huu, Diamond bado anaonekana kuwa katika lindi zito la mawazo yanayotokana na jinsi anavyofanyiwa na yule ampendaye.

Sasa kwakuwa mambo hayajabadilika na ana fedha kidogo mfukoni, Diamond awamu hii anataka kulewa tu. “Kumbe mwenzangu na mimi ni bure tu najisumbua sisi tuko kama ishirini, mabuzi, ving’asti wengine anawahonga, Ohh! Mapenzi yamenifanya kama mtoto nilie vibaya na nina mengi yamenijaa moyoni,” ni baadhi ya mashairi katika wimbo huo.

Pamoja na uandishi wenye kugusa hisia za wale waliokutwa na maswahibu kama yake, vionjo vya beat iliyotengenezwa na mpishi wa AM Records, Manecky na melody za Diamond kwenye Nataka Kulewa tunashindwa kuzitofautisha na vile vilivyotumika kwenye ‘Moyo Wangu’, licha ya kwamba Moyo Wangu ilitengenezwa na Lamar.

Kwa maana nyingine ni kuwa alichokifanya Diamond ni sawa na mtu aliyepita njia moja kwa kubadilisha shati tu ili asijulikane kama amepita sehemu hiyo huku viatu na suruali akiwa amevaa vilevile na hivyo kuwa rahisi kumtambua. Kwa jinsi ambavyo watu walikuwa wakimsubiria Diamond kwa hamu kubwa, tunahisi Nataka Kulewa si wimbo uliowapa walichotarajia.

Hakuna mabadiliko makubwa ya uimbaji wa Diamond kitu ambacho amekuwa nacho tangu anaanza muziki. Melody na mituo yake kwenye nyimbo hufanana katika nyimbo zake nyingi. Pengine hii ni kwasababu wasanii wengi wa Tanzania hasa wa Bongo Flava hutunga nyimbo zao wenyewe na bahati mbaya masikio yao hushindwa kutofautisha kile walichoimba zamani na wanachoimba sasa.

Kama kungekuwa na mtindo wa ufanyaji muziki kama wa wenzetu wa nje ambao huhusisha watunzi wenye elimu nzuri ya muziki, kusingekuwa na mfanano kama huu. Na honestly, msanii anayeimba melody zinazofanana huwa hana muda mrefu kwenye soko kwakuwa watu humchoka haraka.

Pamoja na kasoro hiyo, Nataka Kulewa ambayo imezinduliwa leo, itafanya vizuri kwenye radio kutokana na kuwa wimbo wenye ujumbe unaogusa wengi na pia kuwa club banger.Ukiwa umechangamka na bia mbili tatu kichwani ngoma hii itakufanya ushuke kwenye kile kiti kirefu na ucheze kidogo sio?

Kama umeusikia, tuambie wewe unauonaje!!

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents