Moto Hauzimwi
TECNO Spark 2

Uchambuzi: Ngoma ya ZaiiD ‘Umeme Umerudi’

Naam wapwa, mambo vipi? natoka kupiga duru ka ya 18 ya miamsho ya Umeme umerudi, hizi ni mila na desturi za enzi na enzi za kwanza Unit.

Lazima tusikilize kwa duru nyingi mfululizo kabla kujiridhisha kutoa kauli yoyote, Muulize Samia X kama unabisha. Imenichukua muda kidogo kuitafakari ngoma hii kuona ZaiiD amekua anajaribu kutuletea nini safari hii.

Hii ni hadhari yangu

Kama tulivyo wengi huwa tunakuwa kama tupo kwenye kifungo cha mazoea ambacho funguo za pingu na makomeo yake yako ndani ya fikra zetu bali ni mtihani wa ujasiri wetu wa kuyafungua.

Bado katika kujaribu kuzoea haya maudhui mapya kutoka kwa ZaiiD japo siyo mapya sana kwangu kwa kuwa tayari ameshawahi kunionjesha kazi zake kibao ambazo hazijatoka ni za tofauti mno. Jamaa katoa ngoma yake mpya wiki iliyopita ya Juni 30 siku ambayo Jay Z pia ameachia albamu yake ya 13 iitwayo 4:44. Nitauliza kwake hili na timu yake nione kama ni kusudi au imetokea tu.

Tena ninapomuongelea Jigga nakumbuka nimeona mahojiano yake hivi karibuni akisema kuwa anashangaa kuona watu wanavyokua na haraka ya kutoa maoni tofauti tofauti juu ya albamu yake hiyo ambayo imefanikiwa kufikia mauzo ya Platinum ndani ya siku tano tangu ilipotoka. Hata kabla hawajaipa fursa kidogo ituame maskioni na nyoyoni mwao, hawajaipa wasaa wa kupambanua mashairi, kujikonga na mitambao huku wakinesa na midundo!!!

Turejee pale Mwenge, chochoro za Silent Inn (sijui siku hizi kunaitwaje) maskani ya Marquiz Du Zaire, alikozaliwa na kukulia Zaiid, mazingira yanatuakisi kwenye kila nyanja za maisha yetu.
Si ajabu ZaiiD anapoamua kupita mipito yenye vionjo mbadala, unaweza kuskia kabisa kweli kujikita moja kwa moja kwenye kuimba… tonge kadhaa za ugali za wengine zitatoeka.

Natania tu wapwa

Kama nilivyosema ugali mkubwa sana huu, watu bado wanaletea fani usela bure, ndio maana Mchaff ZaiiD anawasibabi washika dau “washika dau wanashika dau lote”.
Nimeona hii kazi imebeba kiujumla harakati za msanii kujikwamua toka uduni wa maisha, kichupa kina haya mandhari ya hisia za kujiondoa kule mashokorani. Napata mtazamo wa jaribio la nafsi kujiepusha na kuwa mbali na mazingira tatanishi yanotuzunguka kila siku. Mzuka huu ni tafsida ya kusibabi siasa za kifisadi kwa ustadi na hadhari ili isimletee fanani muhali.

Inaonyesha ZaiiD hajasahau mila na desturi za mwambao. Ushairi na tenzi kuonyesha umahiri wa kiswahili. Umeme umerudi iko wazi sana maana kunapokua na giza kubwa basi msisimko huwa kama dhoruba kitaani pale umeme unaporudi.

Wiki moja tu imepita tangia suala la mabinti na ujauzito lilivyotawalaa vyombo vya habari baada ya kiongozi wa nchi kutoa msimamo juu ya wanafunzi wapatao ujauzito wakiwa masomoni.
Sipo hapa kushawishi wale walopokea ujio huu wakiwa bado wamefunikwa gubigubi na mapazia ya giza la mazoea, bali naamini wakijipanafasi jicho la roho litaona miali ya nuru angavu ya ukombozi.

Wataskia wenyewe wito wa vita ya kujikwamua toka makucha hatari ya zimwi Mazoea, Ujasiri na uthubutu alouchukua ZaiiD kujiachia atakavyo, unastahili kuungwa mkono kwenye hali hii ambayo tasnia yetu ilipo. Umeme umerudi ni kauli mbiu ya kitaa, umeme ni nishati asema ZaiiD nilipo jenga nae. Basi kama nishati muhimu kwetu basi kaitumia kuonyesha pamoja na ugwadu wa maisha uliopo.

Bado watu tunaweza kuwa imara na kuwa na mzuka wa kusherehekea maisha, ile kuruka juu kwa mori wa kimasai ndani ya mdundo ulopigwa mande na watayarishaji wawili dogo wa kwanza anaitwa Young keys na mwingine anaitwa S2kizy.

Kichupa mkono wake mwenyewe Inno Mafuru na ndo alokichepa kwa viwango hivyo. Gonga kichupa, kipe dole gumba na ka’ alivyotuasa Jay Moe msaidie ZaiiD kusambaza mzuka huu kama umeme umerudi. Twenzetu wapwa, tuko pamoja.

Imeandikwa na Zavara Mponjika
[email protected]
Twitter @Dzavpharaoh 
Insta.    @dzavpharaoh
Fb :     Zavara Mponjika

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW