Bongo5 MakalaBurudani

Uchambuzi: One, Stereo, Songa – Kivyovyote, Usione Hatari na Usiku, ni hatari tupu

Wafalme watatu wa underground hip hop ya Tanzania wametupa bombshell zao. Nakuambia mitaa haina amani tena sababu these boys are sick, damn! Nawazungumzia One the Incredible, Songa na Stereo. Ni kama wameambiana kuachia silaha zao mwezi huu na kwa sikio moja tu, ni rahisi kujipa jibu mwenyewe kichwani kuwa hawa vijana ni hatari mno.

Hatari

Hawakamatiki na kama wewe ni rapper nusu huwezi hata kuiruhusu ngoma yako ichezwe pamoja na zao.Naongelea ‘raw talents’, real hip hop, ujuzi usioelezeka wa kucheza na maneno na mitindo mikali kama moto.

One the Incredible – Kivyovyote

Nianze kwa kukiri kuwa One the Incredible ni rapper niliyempa taa ya kijani kuingia kwenye orodha ya wasanii wa hip hop hatari kuwahi kutokea Tanzania. Hajawahi kuniangusha tangu nianze kumsikia kwa mara ya kwanza.

Nikutahadharishe kuwa ili uweze kuiona almasi ya ubunifu kwenye Kivyovyote inakuhitaji kujipa muda wa dakika kama nane hivi kuusikiliza wimbo huu mara mbili na kuiruhusu akili yako iyatafsiri mawimbi ya sauti na uchezeswaji wa maneno ya Kiswahili unaotumiwa na rapper huyu.

Nachelea kusema, Kivyovyote inaingia kwenye list ya ngoma tatu za One ninazozipa salute zaidi, ya kwanza ikiwa ni ‘The Incredible. Kivyovyote ni ngoma yenye mchanganyiko wote muhimu wa rap ya majigambo. One anajaribu kuwatahadharisha wachanaji goi goi kukaa kando kumpisha mfalme apite.

“Naposhika biki watoto wanashika speech, midondoko Moko wa moto unamshika vipi? Chagua kujenga imani au kujenga ghorofa, kumtenga mpinzani au kumpa ushindani wa kutosha,” anachana One.

Anajaribu kueleza jinsi ambavyo maneno ya kukatisha tamaa yasivyo na madhara kwake kwa kuandika: Unapovunjwa moyo, unaujenga tena na usijenge chuki wacha iondoke na iende vyema,” anachana na kusisitizia kwa mstari usemao ‘Milele nitasimama nikidondosha fasihi, wanabana kwakuwa nimekataa kuipotosha jamii.’

Kivyovyote ni ngoma kali na mdundo matata wa AK 47 unaisindikiza vyema mistari mikali ya One ambayo inageuka kama onyo kwa rapper wengine wa aina yake.

Songa: Usiku

Songa na Duke wameungana pamoja kuja na kitu kipya kabisa kwenye kurasa za hip hop ya Tanzania. Kila wiki kwa mwezi mzima watakuwa wakiachia wimbo mmoja wenye simulizi za Songa. Wimbo wa kwanza kutoka kwenye mradi huo unaitwa Usiku. Ukisikiliza simulizi katika Usiku, unaweza kufananisha na ile hadithi ya kitabu kilichoandikwa na mwandishi wa riwaya, Bairu Katama kiitwacho ‘Sokoni Kariakoo’. Kwenye kitabu hicho, mhusika mkuu anaamua kutoka kwao Iringa kuja kumtafuta kaka yake anayefanya biashara kwenye soko la Kariakoo. Lakini kwakuwa Kariakoo ni sehemu kubwa, mtu huyo anapata adhabu ya siku moja kumtafuta kaka yake bila mafanikio na kuamua tu kurudi kwao.
Kwenye Usiku, Songa anakuja Dar es Salaam kutoka kijijini kumtafuta mjomba wake. ‘Natoka bush naingia Dar mataa yamejaa kuona mwangaza nasikia raha,” anaanza Songa kueleza hali inavyokuwa kwa mgeni wa jiji la Dar pale anapofika kwa mara ya kwanza.

Songa anafika Dar na kuanza kumtafuta mjomba wake na mbaya zaidi hajui anapoishi. Anamsaka kila anapoweza kwenda lakini anaambulia patupu. Anaamua kwenda kwenye kibanda cha simu kumpigia simu mjomba wake ili amwelekeza atampataje. ‘Napiga simu hewani “samahani mteja unayempigia hapatikani, jaribu baadaye na kama ukishindwa hata mwakani”. Majibu hayo yanammaliza nguvu Songa na mbaya zaidi hakuna anayemjua mjini.

Ikiwa tayari ni saa 6 usiku, Songa anaamua kupita vichochoroni kwenda kusikojulikana ilimradi tu aondoke mahali alipokuwa. Wakati anapita, akasikia sauti ikipiga kelele kuomba msaada. “Nikashtuka kuona njemba zimejipanga wawili wamemshika binti mwingine amebeba panga, akili ikacheza usoni kijacho chembamba huku nikiwaza kwa hizi njemba ntaweza tamba?” anaendelea Songa.

Kuona hivyo Songa akainama chini na kuokota jiwe na kumpiga nalo mmoja. Jiwe hilo likawatisha wawili walioamua kukimbia lakini mmoja akabaki kupambana na Songa. Songa anarap kujisifia kuwa kijijini anakotoka ana tuzo ya mieleka na hivyo hakuwa na woga wa kukabiliana na kibaka huyo. Ndicho alichokifanya. Baada ya kumchapa ngumi na mitama kadhaa, kibaka huyo akakimbia na kumwacha binti waliyetaka kumbaka akilia.

Songa akamshangaa msichana huyo mrembo kuwa maeneo yale usiku huo na akamuambia kuwa huenda mavazi aliyokuwa amevaa yaliwatega wahuni hao. Hata hivyo hakujua kuwa msichana huyo alikuwa maeneo yale kujiuza mwili ili kuilisha familia yake. “Mara akaanza kulia ‘eti kaka una roho ngapi’ nikamwambia usilie mimi ndo Songa nna roho safi”. Baada ya story mbili tatu, Songa anaagana na msichana huyo na kuendelea na safari ya kumsaka mjomba wake.’

Stereo ft Ben Pol – Usione Hatari

Tofauti na One na Songa, Stereo anatumia ngoma hii iliyotayarishwa na producer wa Arusha, DX wa Noiz Maker kumwimbisha mrembo wake. ‘Naomba nafasi nikupatie kile unachohitaji, nakupenda kweli wanajua hadi washkaji,’ analalamika Stereo. ‘Sina mavumba, sina nyumba wala benz, Usiwe na wasi nipe nipe nafasi nikuenzi’

Usione Hatari ni wimbo tofauti kidogo na zile mashabiki wake wamemzoea. Ameamua kutoka kidogo kwa underground hip hip kuutafuta mkondo mkuu wa muziki ambao siku zote ndio wenye chemchem za hela. Pamoja na kuwa wimbo wa mapenzi, beat yake ni tofauti kidogo na zile za Duke ama maproducer wa Tamaduni Muzik ambao beat nyingi huzifanya kwa kuchop sample mbalimbali. Huu ni wimbo mzuri kuudedicate kwa msichana unayemtaka awe pamoja nawe.

Nikupe nafasi ya kuamua mwenyewe, ipi ni kali?

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents