Habari

‘Uchumi wa Viwanda uende sambamba na Usalama na Afya mahali pa kazi’ Katibu Mkuu Andrew Massawe 

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umetakiwa kuongeza jitihada katika kuwaelimisha wananchi kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa njia ya mtandao.


Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Andrew Massawe, alipotembelea ofisi za OSHA zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo alifanya kikao na menejimenti ili kupata mrejesho wa utekelezaji wa maelekezo na miongozo mbalimbali ambayo ofisi yake imekuwa ikiyatoa katika kuboresha huduma kwa wananchi.


“Katika kipindi hiki ambacho serikali inaweka msukumo mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, tunataka mageuzi haya ya viwanda yaende sambamba na uzingatiaji wa viwango vya Usalama na Afya mahali pa kazi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokeaa endapo suala hili muhimu halitazingatiwa,” alisema Massawe na kuongeza

“Mmezungumzia pia kuhusu kupanua wigo wa kazi zenu hizi katika maeneo mengi ya nchi, hilo nalo ni jambo la msingi japokuwa tunataka kuweka msisitizo katika utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao (automation) lakini tunahitaji kuwa na ofisi walau katika maeneo yote muhimu. Hivyo tunatakiwa kujenga mahusiano mazuri na taasisi nyingine katika Wizara ili tuweze kutumia majengo yaliyopo kwa pamoja kwasababu hatuhitaji kujenga au kukodisha majengo kila mahali.”

Maagizo hayo ya Katibu Mkuu yalitolewa baada ya kupokea taarifa fupi ya utekelezaji ya maagizo ya Wizara kutoka kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda ambapo pamoja na kuelezea utekelezaji mzuri wa maagizo na miongozo mbali mbali ya serikali, alielezea mpango wa kufungua ofisi za Kanda ya Magharibi mkoani Tabora itakayohudumia mikoa ya Tabora, Kigoma, Rukwa na Katavi.

Aidha, katika taarifa hiyo, Mwenda ilielezea jinsi ambavyo taasisi yake imefanikiwa katika matumizi ya mifumo mbali mbali ya serikali ikiwemo mifumo ya malipo serikalini ya GePG, MUSE pamoja na mfumo Ununuzi na Ugavi serikalini wa TANePS.

Katibu Mkuu alisema: “Nimeridhishwa na utekelezaji wa mambo mbali mbali tuliyowaagiza hususan matumizi ya mifumo mbali mbali ya serikali.”

OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu ambayo husimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Kupitia sheria hii, OSHA husajili maeneo ya kazi na kuyafanyia ukaguzi kuhakikisha kwamba yanazingatia viwango vya kiusalama na afya na hivyo kuwakinga wafanyakazi dhidi ya magonjwa na ajali zitokanazo na mazingira ya kazi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents