Habari

Uchunguzi kufanyika baada ya uchaguzi wa Nigeria kuahirishwa, Rais asema tume lazima walieleze taifa kwanini waliahirisha

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amesema baada ya uchaguzi kumalizika, Tume ya Uchaguzi (INEC) inafaa kueleza sababu za kuahirishwa kwa uchaguzi huo kwa muda wa juma moja huku akiwaonya wale walio na nia ya kuiba kura.

Katika kikao cha dharura na wakuu wa chama tawala cha All Progressives Congress (APC) katika mji mkuu wa Abuja, Buhari alisema kuna haja ya tume hiyo kueleza kwa nini ilishindwa kufanya uchaguzi siku iliyopangwa na kuuahirisha saa tano kabla ya vituo kufunguliwa.

Kwa mujibu wa DW, Buhari aliwataka maafisa wa polisi na jeshi wasiwe na huruma kwa watakaotaka kuvuruga uchaguzi huo huku akionya kwamba yeyote atakayeiba masandaku ya kupigia kura ama kutumia wahuni kutatiza upigaji kura basi huenda hiyo ikawa ni mara yake ya mwisho kuvunja sheria.

”Hawakuwa na haja ya kusubiri hadi saa sista kupiga kura ndio waahirishe. Sijui vipi hilo linawezekana. Bila shaka sababu ya kushindwa kwao huko ni lazima ielezwe kwa taifa. Baada ya uchaguzi tunataka kujua hasa kilichotokea na nani anahusika. Tuwaambie wapigaji kura wetu wawe na subira na wawajibike kwa kwenda kupiga kra kwa amani. Sitarajii mtu yoyote kusumbua. Nimewapanga maafisa wa usalama na jeshi, wametambua sehemu zilizo na hatari.na wako tayari,” alisema rais Buhari.

Mpinzani mkuu wa Buhari, Atiku Abubakar wa chama cha Peoples Democratic Party (PDP) amedai kwamba serikali ya Buhari ndio waliokuwa nyuma ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo japo hakutoa ushahidi.

Wagombeaji wote hao wawili wa chama kinachotawala APC na chama kikuu cha upinzani PDP wamekuwa wakishutumiwa kwamba wanataka kuchakatua matokeo ya uchaguzi huo kwa kununua kadi za kielektroniki za kupiga kura.

Tume ya uchaguzi ya Nigeria iliusogeza uchaguzi huo wa Urais na Wabunge kwa sababu ya matatizo ya usafirishaji wa vifaa vya kupigia kura huku wakikana kwamba imetokana na shinikizo la kisiasaS

Kutokana na kuahirishwa kwa kura hizo sarafu ya Nigeria, Naira, imeanza kushuka na soko la hisa kuteremka kwa sababu ya wawekezaji kuingia hofu kwamba kuna uwezekano wa mzozano juu ya matokeo ya kura.

Mtaalamu wa Uchumi katika shirika la Afrika Kusini la NKC African Economics, Cobus de Hart amesema baadhi ya wawekezaji wanasubiri kukamilika kwa uchaguzi huo kuangalia hali itakavyokuwa kama kutakuwa na mzozo wa matokeo jambo ambalo linawezekana kutokana na kuahirishwa kwa uchaguzi.

Hii sio mara ya kwanza kwa taifa la Nigeria kuahirisha upigaji wa kura, mwaka 2015 uchaguzi uliahirishwa kwa wiki sita kutokana na tishio la kiusalama kutoka kwa Boko Haram Kazkazini mwa Nigeria na mwaka 2011 pia uchaguzi ulisimamishwa saa kadhaa baada ya watu kuanza kupiga kura sababu ikiwa ni kukosekana kwa karatasi za kupigia kura, karatasi za kuandika majibu ya kura miongoni mwa vifaa vyengine muhimu kwa uchaguzi.

Takriban wapigaji kura milioni 84 wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi huu wa 6 katika muda wa miaka ishirini tangu Nigeria kurudi katika utawala wa kiraia baada ya miongo ya utawala wa kijeshi.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents