Promotion

Udhamini ligi kuu ya soka Tanzania tafrani tupu!!


Na mwandishi wetu

Kwa wale wapenzi, wadau na mashabiki wa soka la Tanzania mpaka sasa watakuwa wanajua nini ni habari ya mjini. Kama ulikuwa hujui Kuanzia wikiendi iliyopita, siku ya Jumamosi, ligi kuu ya soka Tanzania Bara ilikuwa imeanza rasmi siku hiyo, lakini ilianza kwa mshike mshike wa hali ya juu katika Uwanja wa Taifa uliotokana na suala la udhamini na haki ya kujitangaza inayotokana na udhamini wa makampuni mawili yanayofanya aina moja ya biashara.

Sakata hilo lilitawala siku nzima ya Jumamosi jioni, Jumapili na Jumatatu hii katika vyombo mbali mbali vya habari zaidi kwenye radio na runinga na pia katika viunga ambavyo wadau na mashabiki hukutana kujadili pamoja na mambo mengine ushiriki wa timu zao, hali ya timu kimchezo pamoja na hali ya soka kwa ujumla.

tukio lenyewe lilihusisha timu ya African Lyon, Vodacom kama wadhamini wakuu waliokuwepo ambao nao walikuwa wanatarajiwa kusaini mkataba mpya na wasimamizi wa soka Tanzania TFF kwa upande mwingine.

Timu ya African Lyon ilitaka kutumia jezi na mabango ya mdhamini wao mpya Zantel ambao wao walitangaza rasmi kuidhamini timu hiyo kupitia vyombo vya habari siku ya Ijumaa ambayo ilikuwa siku moja kabla ya kuanza rasmi kwa ligi hiyo.

Kwa jinsi nilivyosikiliza maelezo kwa mara ya kwanza siku ya Jumapili mchana kupitia kipindi cha Sports Xtra ambacho kilikuwa na wageni waalikwa mmoja wapo akiwa Mkurugenzi wa African Lyon Rahim Kangezi, Katibu mkuu wa zamani wa shirikisho la soka TFF Fredrick Mwakalebela na wachambuzi wa masuala ya michezo katika Clouds FM akiwamo Shafiii Dauda na Alex lwambano.

Katika kipindi hicho kuna maswali mengi yasiyo na majibu yaliyopelekea kuonekana wazi kama kuna uzembe uliotokana na kufanya kazi kwa mazoea na ubinafsi ambao ndio ulizaa mapungufu ambayo yamepelekea kadhia katika sakata hilo.

Moja ya mapungufu hayo ni pamoja na TFF kutosimamia wajibu wake kama kiongozi ama mlezi wa ligi kwa kutotumia zaidi vitengo vyake vya sheria na masoko kwa umakini wa hali ya juu. Hii inatokana na kwamba mpaka ligi inaanza (siku ya Jumamosi iliyopita), hakuna kikao baina ya timu shiriki na shirikisho cha ku brainstorm kabla ya kuanza ligi hiyo ambacho kingejadili kwa undani vipengele vya mkataba ambao ulikuwa unasemekana umeingiwa kati ya Vodacom Tanzania na TFF.

Hapa ninamaanisha kama kweli kikao kingekuwa kimefanyika basi utata uliotokea ungeweza kuwa umeshughulikiwa kwa wakati, kabla ya tarehe za ligi kutangazwa namaanisha kabla ya ratiba kutoka, kwani Mkurugenzi wa African Lyon alisema wiki hii kuwa waliwasilisha barua rasmi ya kuwataarifu TFF kama wamepata mdhamini ambaye ni kwa kwa uhalisia wa biashara yake ni mpinzani wa kibiashara wa Vodacom.

Na katika muendelezo wa maelezo yake alisema wao timu kama moja ya wadau wa kamati ya ligi walishaongelea suala hilo la kupata wadhamini ambao ni wapinzani wa moja kwa moja wa kibiashara na mdhamini mkuu katika vikao vyao na TFF na wadhamini katika vikao vilivyopita na wakakubaliana kuwa wanaweza kuingia mikataba ya namna hiyo.

Cha kushangaza katika moja ya swali alilouliza Shafii Dauda kwenda kwa bwana Kalia mmoja wa wanakamati ya ligi ambalo alitaka kufahamu nini ilikuwa status ya udhamini mpaka hiyo Jumamosi wakati ligi inaanza rasmi, kwa maana ya kwamba je! kulikuwa tayari na mkataba wa udhamini uliosainiwa, na kama wao kamati pamoja na wadau wao ambazo ndio vilabu walikuwa na copy ama nakala za mkataba huo bwana alishindwa kujibu kwa kuwa hakuna kitu kama hicho kilichotokea. Hapo ndipo maswali magumu yanapoanza.

Mosi tukirudi nyuma katikati ya wiki iliyopita ilitolewa taarifa katika vyombo vya habari ambayo ilisema Vodacom imesaini mkataba na TFF wa kudhamini ligi hiyo ya Tanzania bara kwa miaka mitatu, sasa cha kushangaza taarifa hiyo haikuwa na maelezo ya kina yanayohusiana na mkataba huo kama ni kiasi gani kimewekwa zaidi ya kutaja muda wa udhamini, ambao ni miaka 3 pamoja na waliohusika katika hafla hiyo ya kusaini mkataba huo.

Na katika taarifa hiyo hakukuwa na jina ama mwakilishi yoyote kutoka kwa upande wa vilabu ama kamati ya ligi, licha ya kwamba udhamini huo unawahusu. Mbaya zaidi hakukuwa na picha iliyoambatana na taarifa hiyo ambayo inamhusisha Mkurugenzi mkuu wa Kampuni hiyo, jambo la kushangaza kweli kweli.

Tukirudi kwenye kiini cha mzozo swali lingine linalojitokeza kama kamati ya ligi na TFF zina uhusiano wa kikazi mzuri na wakaribu na kwamba wote kwa pamoja wana system gani ya kuratibu mawasiliano kati yao ikiwemo vitengo vya sheria na masoko vya taasisi zote mbili pamoja na mawasiliano ya ki sekretari kwa ufanisi ambao unatarajiwa.

Hapa namaanisha kwa mujibu wa maelezo ya mwanakamati na Rahim Kangezi (Zamunda) jukumu la kujadili mkataba lilikuwa chini ya TFF lakini TFF na kamati wanaonekana kutofanya kazi kwa maelewano ya kimawasiliano yaliyosahihi kwani barua ya African Lyon pamoja na kupokelewa TFF haikujibiwa na hapa ndipo tatizo kubwa lilipokuja.

Kwa nini hakukuwa na muda wa kutosha ili kutoa majadiliano ya kina kati ya wanasheria wa pande zote kabla ya hatua ya muda wa mwisho wa kusaini mkataba huo? Na hapa kuna tatizo lingine linaloonekana ambalo ni maslahi binafsi kati ya TFF na Vodacom.

Kwa jinsi ambavyo hali ilivyo hali inaweza kujitokeza kama hii siku ambayo kampuni ya Serengeti inavyoweza kudhamini timu kama ya Toto Afrika watakapopambana na timu zinazodhaminiwa na TBL yaani Yanga na Simba ama hali kama hiyo ikajitokeza siku kampuni ya Coca Cola ikidhamini timu itakayopambana na Azam, Chamazi.

Ni muhimu kwa TFF, Timu na wadhamini kuweka vipengele vyenye mrengo wa kuendeleza mchezo wa soka kuliko kudidimiza kwani kitendo cha Vodacom kukumbatia fursa kubwa zaidi na kuzinyima nafasi timu nyingine kama ilivyoonekana kwenye tafrani ya jumamosi pale uwanja mkuu wa taifa ni jambo la kukwaza wadau wote wa tasnia ya soka nchini Tanzania.

Kwa jinsi hali inavyoonekana Soka letu bado halijakuwa katika upande wa timu kujitegemea hivyo kuhitaji kampuni zaidi ya moja kuzisaidia katika mishahara, nauli, posho na mahitaji mengine yanayoendana na hali ya maandalizi na ustawi ama ukuaji wa timu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents