UDSM bado kwafukuta

UDSMWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM), wamemtaka Spika wa bunge la Serikali ya Wanafunzi, Massawe Ellimo, kuitisha kikao cha dharura chuoni hapo, ili waweze kujadili na kujua hatima ya wanafunzi wenzao waliofukuzwa

na Lucy Ngowi




WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM), wamemtaka Spika wa bunge la Serikali ya Wanafunzi, Massawe Ellimo, kuitisha kikao cha dharura chuoni hapo, ili waweze kujadili na kujua hatima ya wanafunzi wenzao waliofukuzwa.

Wakizungumza kwa jazba kwa nyakati tofauti walipokuwa wamekusanyika kwenye kiwanja cha mapinduzi (revolution square), wanafunzi hao walisema kuwa, wanatoa muda kwa bunge hilo hadi leo saa nne asubuhi, liwe limeshatoa majibu yatakayowaridhisha.

“Kufikia kesho muda kama huu wanafunzi wenzetu watano wawe wamesharudi. Tunamtaka waziri mkuu wa Daruso awajulishe wahusika juu ya hilo… hivyo kesho muda kama huu tutakusanyika tena hapa tujue nini cha kufanya,” alisema mwanafunzi mwingine.

Madai hayo yanatokana na uamuzi wa hivi karibuni wa uongozi wa chuo hicho kusimamisha uchaguzi wa rais, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kujiuzulu kwa Baraza la Rufaa.

Awali, Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi chuoni hapo (Daruso), Julius Mtatiro, alisema kuwa, Daruso itasimama kidete kuhakikisha wanafunzi wanamchagua rais wanayemtaka.

Alisema kikao cha bunge kilichokaa Jumamosi iliyopita kiliunda bodi mpya ya rufaa ambayo itasikiliza kesi zote zilizowasilishwa kuhusiana na uchaguzi wa rais, pamoja na kuunda timu ya majadiliano inayoongozwa na rais wa Daruso, Deo Daud, ambayo itakutana na bodi mbalimbali za utawala wa chuo kujua hatima ya wanafunzi hao waliofukuzwa.

“Katika kikao cha Jumamosi, iliundwa negotiation team (timu ya majadiliano) inayoongozwa na rais wa Daruso, ili iende ikutane na bodi mbalimbali za utawala, waone ni jinsi gani ya kutatua tatizo hilo.

“Lazima twende na hali hii bila kumuathiri mtu wala kuathiri masomo. Ninawaomba wanafunzi wawe watulivu sana. Muafaka wa jambo hili ni wanafunzi wenzetu waweze kurudi chuoni na kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi,” alisema Mtatiro.

Akizungumzia suala la mgombea urais ambaye ni raia wa Uganda, Odong’ Odwar, alisema kuwa suala hilo linashughulikiwa na timu hiyo inayoongozwa na rais wa Daruso, ambayo inazungumza na utawala.

“Mambo haya tutayasimamia mpaka mwisho bila kumuogopa mtu yeyote. Tutakuwa imara kusimamia mambo haya,” alisema Mtatiro.

Pamoja na maelezo hayo ya Mtatiro, wanafunzi walisema kuwa wanachotaka ni kujua wanafunzi wenzao watarudi lini na si propaganda. Hivyo wamemwagiza afikishe ujumbe kwa uongozi wa Daruso na leo saa nne asubuhi wapewe majibu yao.

Suala la ugombea urais katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam limeingia katika sura mpya baada ya mgombea huyo wa Uganda Odong’ kuambiwa kuonyesha vyeti vyake halisi vya shule ya sekondari na wanafunzi watano kusimamishwa.

Sakata hilo huenda likachukua sura mpya leo baada ya uongozi wa chuo hicho kuamua kujitokeza na kuzungumza na waandishi wa habari.

Ingawa haikuelezwa nini kitazungumzwa, lakini inaaminika kuwa masuala hayo, ambayo yameanza kupandisha ‘joto’ chuoni hapo ndiyo yatakayokuwa ajenda kuu ya mkutano huo wa waandishi wa habari.


 


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents