Habari

Ufisadi mwingine waibuliwa Muhimbili

HARUFU ya ufisadi mwingine imeibuka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya mamilioni ya pesa kudaiwa kutumia kununua vifaa vilivyo chini ya kiwango huku zingine zikitumika kujenga na kukarabati majengo chini ya kiwango na tayari, serikali imetangaza kuunda tume kuchunguza jambo hilo.

Eben-Ezery Mende na Rehema Mwakasese

 

 

 
HARUFU ya ufisadi mwingine imeibuka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya mamilioni ya pesa kudaiwa kutumia kununua vifaa vilivyo chini ya kiwango huku zingine zikitumika kujenga na kukarabati majengo chini ya kiwango na tayari, serikali imetangaza kuunda tume kuchunguza jambo hilo.

 

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Profesa David Mwakyusa alibainisha hali hiyo jana Dar es Salaam alipofanya ziara ya ghafla hospitalini hapo kwa lengo la kuangalia ujenzi na ukarabati unaoendelea baada ya kuwepo minong’ono ya ufisadi kwenye shughuli hiyo.

 

Alisema alipanga kufanya ziara hiyo baadaye lakini kutokana na malalamiko aliyokuwa akiyapata kutoka kwa wananchi na wafanyakazi wa hospitali hiyo juu ya hali ya vifaa vipya vilivyoletwa na ujenzi unaoendelea kwa kusuasua ,aliamua kufanya ziara hiyo ghafla jana.

 

“Sikuwa na ratiba ya kuja hapa leo, lakini kutokana na malalamiko niliyokuwa nikiyapokea kuhusu hali halisi ya mazingira yalivyo, nimeona nifanye ziara hii ya ghafa ili nijionee mwenyewe kuwa yanayosemwa ni ya kweli au la,”alisema

 

Alisema katika ziara hiyo alibaini ukweli wa yale aliyokuwa akiambiwa na wananchi na baadhi ya wafanyakazi hospitalini hapo kuwa kulikuwa na kasoro katika baadhi ya maeneo na vifaa vipya vilivyonunuliwa kwa ajili ya ujenzi unaoendelea.

 

Alibainisha kuwa baadhi ya vifaa vilivyonunuliwa vimeonekana kuwa chini ya kiwango na baadhi vimeonekana kuharibika kabla ya kutumiwa huku vingine vikiwa haviwezi kutumika kabisa kwa ajili matibabu.

 

Vifaa vilivyo onekana kuwa chini ya kiwango ni pamoja na vitanda vya kuwahudumia wanawake wakati wa kujifungua ambavyo vilionekana kuwa vidogo, hivyo kushindwa kutoa huduma hiyo ipasavyo.

 

Vifaa vingine ni vitanda vya kulala baada ya mama kujifungua ambavyo navyo vilibainika kuwa vidogo na haviwezi kumudu nafasi ya mama na mtoto.

 

Vifaa vyote vya mbao vilivyonunuliwa vilionekana kuwa chini ya kiwango lakini na baadhi vilionekana kuharibika hata kabla ya kutumiwa.

 

Kutokana na hali hiyo, Prof. Mwakyusa amegiza vifaa vingine ambavyo bado havijawasili hospitalini hapo visipokelewe mpaka vipimwe na kuthibitishwa ubora wake kama unakidhi mahitaji.

 

Alisema mtu atakayetoa kauli ya mwisho kuruhusu uingizwaji wa vifaa hospitalini hapo ni Daktari Bigwa wa Idara husika, wauguzi na wataalamu wa kitengo husika.

 

Kutokana na hali hiyo, Prof. Mwakyusa aliitaka Wizara ya Katiba na Sheria kuingilia kati kuona kuwa ni hatua gani itachukua dhidi ya watu waliopewa tenda ya ujenzi na uagizaji wa vifaa hivyo walioshindwa kukidhi matakwa yaliyohitajika.

 

Alisema tangu serikali iingie mkataba wa ukarabati, ujenzi na ununuzi wa vifaa vipya na kampuni ya NOMAN & DOMAN mwaka 1990, imekuwa ikifanya kazi kwa kusuasua kutokana na mkandarasi aliyepewa tenda hiyo kudai kuwa halipwi fedha kwa wakati.

 

Prof. Mwakyusa alisema ili kutatua utata uliopo ndani ya mfumo mzima wa ujenzi, ukarabati na uagizaji vifaa vya matibabu katika hospitali hiyo, Wizara ya Fedha na Mipango ambayo imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hiyo inapaswa kuwajibika kutoa maelezo baada ya kufanya uchunguzi wa kina kama fedha walizotoa na kazi iliyofanyika, zinalingana.

 

“Hapa suluhisho liko kwa Wizara ya Fedha kutuma watu wake Muhimbili ili kubaini kama kweli fedha walizotoa na kazi iliyofanyika vimekwenda kwa mujibu wa taratibu stahiki,”alisema

 

Alisema hivi sasa yuko katika mchakato wa kuunda tume ya wiki mbili kuchunguza mwenendo mzima wa shughuli za ujenzi huo na ukarabati wa hospitali hiyo.

 

Waziri Mwakyusa, alisema endapo itabainika kuwa fedha zilizotolewa katika kutekeleza shughuli za uboreshwaji miundombinu hospitalini hapo zimekwenda kinyume na makubalino, itabidi sheria ichukue mkondo wake

 

Kwa mujibu wa Prof. Mwakyusa mkataba uliofanyika kati ya serikali na kampuni ya NOMAN & DOMAN ya Uingereza mpaka kukamilika kwa shughuli zote za ujenzi, ukarabati na uagizaji vifaa vipya vya matibabu, itakuwa imeigharimu sh. bilioni 10.

 

Hata hivyo Prof. Mwakyusa alidai kuwa mpaka sasa hana takwimu sahihi kuwa serikali imeshatoa kiasi gani katika utekelezaji wa mradi huo.

 

Katika ziara hiyo Prof. Mwakyusa alitembelea katika wodi za Sewa Haji, Mwaisela na wodi ya uzazi.

 

Maeneo mengine aliyotembelea ni chumba cha upasuaji, bohari na karakana ya kutengeneza na kukarabati vifaa vya hospitali hiyo.

 

 

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents