Ufisadi wa kutisha Wizara ya Elimu

Ufisadi mkubwa umeibuliwa ndani ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambapo Sh. 3,043,609,699 (zaidi ya `vijisenti` bilioni tatu), zimetumika kulipa wafanyakazi hewa 1,413

Na John Ngunge, Dodoma



 


Ufisadi mkubwa umeibuliwa ndani ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambapo Sh. 3,043,609,699 (zaidi ya `vijisenti` bilioni tatu), zimetumika kulipa wafanyakazi hewa 1,413, huku mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa idadi kubwa ya watumishi hewa.

Mkoa huo pekee una wafanyakazi hewa wanaofikia 218.
Kadhalika imebainika kuwa wapo baadhi ya walimu wanafanyakazi katika taasisi nyingine huku wakiendelea kulipwa mishahara na Wizara pia, na hivyo kunufaika huku na kule.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Hawa Ghasia, wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.

Alisema wamegundua kuwepo kwa watumishi ambao vituo vyao vya kazi havifahamiki na wala haijulikani walipo na hivyo kuleta mashaka kuhusu uhalali wao.

Alisema wafanyakazi hao hewa waligundulika katika shule mbalimbali za sekondari nchini kufuatia uhakiki uliofanywa na serikali kuhusu rasilimali watu kwenye shule za sekondari, zoezi lililofanyika kati ya mwezi Machi na Desemba mwaka jana.

Mkoa unaofuata kwa kuwa na wafanyakazi hewa wengi baada ya Dar es Salaam ni Morogoro (149), Mwanza (132), Iringa (119), Mbeya (101), Rukwa (95), Arusha (72), Dodoma (57), Shinyanga (52) na Singida (50).

Waziri Ghasia alitaja mikoa mingine kuwa ni Lindi (48), Tanga (48), Mtwara (41), Pwani (40), Kagera (35), manyara (35), Tabora (33), Kilimanjaro (27), Ruvuma (27), Mara (19) na Kigoma (15).

Alisema kulingana na taarifa ya ukaguzi, shule za sekondari 2,861 ambazo wakati wa zoezi hilo zilikuwa na walimu 26,953 zilionekana zina walimu hewa 1,413 ambao walikuwa wakilipwa mishahara kupitia benki.

Alisema zoezi hilo limebaini kuwepo walimu wenye hundi zaidi ya moja ambazo zilikuwa zikitumika kulipia mishahara, hivyo kusababisha wahusika kuwa na mishahara miwili.

Alisema uhakika huo umebaini kuwepo kwa walimu wanaohudhuria masomo katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu bila kupata ruhusa ya mwajiri ambaye ni Wizara ya Elimu huku wakiendelea kulipwa mishahara.

Alisema zoezi hilo pia limebaini kuwepo watumishi ambao hawafundishi darasani kutokana na vifo, kuacha kazi, kustaafu pamoja na utoro, lakini wanalipwa mishahara na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.

Waziri Ghasia alieleza kuwa imebainika mishahara imekuwa ikiingizwa moja kwa moja kwenye akaunti za wahusika bila orodha ya mishahara kukaguliwa na kuidhinishwa na wakuu wa shule za sekondari ambazo ni vituo vya malipo.

Alisema tathmini ya zoezi hilo imebaini kuwa kati ya asilimia 65 na 75 ya watumishi hewa waliobainika katika zoezi hilo ni wanafunzi wanaoajiriwa baada ya kuhitimu kidato cha sita.

Alisema Wizara ya Elimu ilianzisha utaratibu wa kuajiri wahitimu wa kidato cha sita kwa lengo la kukabiliana na tatizo la upungufu mkubwa wa walimu, lakini uhakika unaonyesha kuwa mpango huo umeongeza tatizo la kuwepo watumishi hewa.

Alisema serikali imewaondoa watumishi hao hewa 1,413 kwenye orodha ya malipo ya mishahara na pia kuwaondoa kwenye orodha hiyo watumishi 1,853.

Waziri alisema serikali itachukua hatua kali kwa watumishi wanaohusika na mtandao huo mkubwa wa mishahara hewa ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi na kuwafikisha mahakamani wale wote watakaobainika kuhusika kuiibia serikali fedha kupitia njia hiyo.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents