Afya

Ugonjwa wa ini janga lingine Tanzania, Maambukizi yatajwa kuongezeka kwa kasi kuliko Ukimwi

Imeelezwa kuwa maambukizi ya ugonjwa wa homa ya ini (Hepatitis B) yameongezeka nchini, huku wananchi waliowengi wakiwa hawana uelewa juu ya ugonjwa huo.

Taarifa hiyo ilitolewa jana Julai 18, 2019 katika kongamano la madaktari na wauguzi lililofanyika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Ambapo Daktari bingwa wa homa ya ini, Dkt. John Rwegasha, amesema utafiti unaonesha kiwango cha homa hiyo kimeongeza na vyanzo vikuu vya kasi hiyo ni kujamiiana na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Takwimu zilizotolewa na Shirika la Utafiti la Taifa zinaonesha maambukizi ya homa ya ugonjwa wa ini yamefikia asilimia 4.5, huku jamii ikiwa haina uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa huo,” amesema Dkt. Rwegasha.

Kuhusu muathirika wa ugonjwa huo, Dkt. Rwegasha amesema virusi vya ugonjwa huo vinaweza kukaa ndani ya mwili kwa muda mrefu, hivyo endapo mgonjwa atachelewa kutibiwa, unaweza kuwa sugu na kusababisha kifo.

Hepatitis B na C zote zina madhara, ni ugonjwa sugu ambao unaweza kukaa ndani ya mwili zaidi ya miaka 20, ukichelewa kuutibu kuna madhara makubwa, hata kusababisha kifo,” alisema Dk. Rwegasha na kusisitiza kuhusu chanjo ya ugonjwa hu.

Huduma ya chanjo ipo kwa hospitali zote, lakini bado watu hawajitokezi kwa wingi, nafikiri hii ni kutokana na uelewa mdogo kuhusu ugonjwa huo. Hata hivyo kwa sasa Shirika la Afya Duniani  (WHO) linapendekeza chanjo itolewe kwa watoto mapema ili kudhibiti maambukizi au mama mjamzito kama ana maambukizi anaweza kutumia dawa ili asiweze kumwambukiza mtoto,” ameeleza Dkt. Rwegasha.

Dkt. Rwegasha amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya, ina mpango wa kuwekeza kwenye vipimo na utoaji wa dawa kwa ugonjwa huo kwani vipimo kwa sasa ni changamoto kwa hospitali nyingi na gharama za upimaji kwa hospitali binafsi hufikia hadi Tsh laki 5.

Kwa mujibu wa tafiti za mwaka 2016, Takwimu za Shirika la Afya la Kimataifa (WHO) zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi ya homa ya ini B kwa Tanzania ni wastani wa watu 8 katika kila watu 100.  Huku maambukizi ya VVU, Yalikuwa ni wastani wa watu watano katika kila watu 100.

Soma taarifa hiyo – https://www.mwananchi.co.tz/Homa-ya-ini-hatari-kuliko-Ukimwi/1596774-1964904-view-printVersion-145jgnj/index.html

Fahamu zaidi kuhusu ugonjwa huo:

Homa ya Ini ni ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya virusi ambavyo vikiingia mwilini hushambulia ini na virusi hivyo huitwa HBV (Hepatitis B Virus), ni moja ya ugonjwa hatari zaidi na unaopoteza maisha ya watu wengi kwa kasi kubwa zaidi.

Tafiti zinaonyesha kasi ya ugonjwa huu ni ya hatari zaidi  kuliko hata ya Ukimwi kwa sababu virusi vya Hepatitis B  vinaweza kuishi nje ya mwili wa binadamu (yaani nje ya mfumo wa damu) kwa siku saba ambapo Virusi vya Ukimwi (VVU) havina uwezo wa kuishi nje ya mfumo wa damu hata kwa dakika moja.

Watu takriban 1,000,000 wanapoteza maisha duniani kote kutokana na ugonjwa wa Homa ya Ini (Hepatitis B) na mara nyingi endapo ugonjwa huu haujatibiwa hutengeneza uvimbe katika ini na kusababisha kansa ya ini na baadae kifo.

Kama ilivyo kwa Ukimwi, Virusi vya Homa ya Ini pia huambukizwa kwa njia ya kujamiiana, mate, jasho na mwingiliano wowote ule wa damu, Mama mwenye ugonjwa kumwambukiza mtoto wakati wa  kujifungua, Kuchangia damu isiyo salama, Kuchangia vitu vya ncha kali kama sindano, wembe, Kuchangia miswaki, kuchangia taulo na mwenye ugonjwa huo, kubadilishana nguo au kukumbatiana wakati mkiwa mnavuja jasho.

Kwa wastani kirusi cha HBV kikishaingia mwilini, hupevuka ndani ya siku 75, hata hivyo upo uwezekano wa kupevuka kati ya siku 30 hadi 180. Ndani ya siku 30 mpaka 60, mtu mwenye HBV anaweza kugundulika ikiwa atapimwa.

Mtu mwenye Homa ya Ini ana wastani mdogo wa kuishi kuliko mwenye Ukimwi. Kwa maana hiyo, mwenye maambukizi ya Virusi vya Homa ya Ini hufariki dunia haraka kuliko mwenye VVU.

Watu wengi hawaonyeshi dalili yoyote. Kwa maana hiyo mtu anaweza kuishi na HBV na kusababisha maambukizi kwa wengine bila kugundulika.

Japokuwa watu wengine husumbuliwa na homa kali na dalili ambazo hudumu kwa wiki kadhaa dalili hizo ni Uchovu
Kichefuchefu, Mwili kuwa dhaifu, Homa kali, Kupoteza hamu ya kula, Kupungua uzito, Maumivu makali ya tumbo, upande wa ini, Macho na ngozi kuwa vya njano, Mkojo mweusi.

Kwa wagonjwa wengine, Virusi vya Hepatitis B hukua hadi kusababisha ini kuharibika kabisa (cirrhosis of the liver) au saratani ya ini (liver cancer).

Mpaka sasa Homa  ya  Ini  haina  tiba, vilevile hakuna dawa maalum za kurefusha maisha. Ugonjwa huo ukishafikia kiwango cha ini kuharibika au kupata saratani ya ini, maana yake kinachofuata  ni kifo.

Namna ya kujikinga na ugonjwa huu ni pamoja na Chanjo, Kutumia kinga wakati wa kujamiana, Kuacha kuchangia, vitu vya ncha kali kama sindano, wembe, Kutochangia miswaki, Kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu, Kutochangia damu isiyo salama.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Kusini ya Jangwa la Sahara ndiyo eneo hatari zaidi.

Tanzania ni moja ya nchi zilizopo katika eneo hilo, Kiwango cha hatari Kusini mwa Jangwa la Sahara kinalingana na kile cha Mashariki ya Bara la Asia.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa watu wengi walipata maambukizi nyakati za utotoni na kwamba kati ya asilimia tano mpaka 10 ni waathirika sugu.

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents