Siasa

Uhuru Kenyatta akutana na JK

MWENYEKITI wa Chama cha KANU cha Kenya, Uhuru Kenyatta, jana alikuwa na mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.

na Irene Mark


MWENYEKITI wa Chama cha KANU cha Kenya, Uhuru Kenyatta, jana alikuwa na mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.


Habari za uhakika zilieleza kuwa Kenyatta, ambaye pia ni mtoto wa Rais wa kwanza wa nchi hiyo, hayati Jomo Kenyatta, alikuwepo Ikulu tangu asubuhi akisubiri kuonana na Rais Kikwete ambaye alikuwa Arusha.


“Ni kweli huyo mgeni (Uhuru Kenyatta) yupo hapa na ratiba inaonyesha kuwa atazungumza na mheshimiwa (rais) saa saba mchana.


“Hivyo ni bora urudi baadaye kwa sababu hata rais mwenyewe hajatua, ndiyo ametua Arusha sasa hivi na hapa anafuata ratiba,” alisema mmoja wa watumishi wa mapokezi Ikulu akimtaka mwandishi kusubiri.


Hata hivyo, ilipotimu saa 7:10 mchana, mwandishi na mpigapicha wa gazeti hili, walifika Ikulu kwa lengo la kupata habari za mazungumzo hayo, lakini hali ilikuwa tofauti.


“Aisee, watu wa habari wamesema watawatumia habari kwenye ‘media’ zenu (ofisi zenu)… mazungumzo hayo ni ya siri hamtakiwi.


“Alitakiwa kuwepo mpigapicha kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo, lakini kwa sasa mmechelewa mazungumzo yameshaanza. Watu wa habari hapa (Ikulu) wataandika story (habari) na kuwatumia,” alisisitiza mtumishi huyo.


Hata hivyo, hadi jana jioni, maofisa wa Ikulu hawakutoa taarifa yoyote kuhusu mazungumzo ya viongozi hao.


Alipopigiwa simu, Mwandishi Msaidizi wa Rais, Maura Mwingira, alisema kuwa atafutwe Mkurugunzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu ambaye simu yake ilikuwa imezimwa.


Inaaminika kuwa, Kenyatta alionana na Rais Kikwete kuhusu ghasia na vurugu zilizotokana na uchaguzi mkuu nchini humo.


Vurugu hizo tayari zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 350 baada ya wafuasi wa ODM kukataa kumtambua Rais Mwai Kibaki baada ya mgombea wao, Raila Odinga kudai kuwa uchaguzi ulikuwa umevurugwa.


Kuja kwa Kenyatta, inaaminika ni mwendelezo wa jitihada za Rais Kikwete kutatua mgogoro huo ambao unazidi kusababisha hali mbaya nchini humo na kwa nchi jirani.


Wakati jitihada hizo zinaendelea, taasisi kadhaa za kimataifa zimeanza kutoa tahadhari zikibainisha kuwa takriban Wakenya nusu milioni hawana makazi, chakula na maji na kuwa wanahitaji msaada wa haraka ili kuokoa maisha yao.


Hali hiyo imetokana na vurugu zilizodumu kwa muda wa wiki moja sasa, kutokana na kutokubalika kwa matokeo ya kura za urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Desemba 27, mwaka jana.


Chama cha upinzani cha ODM kinayalalamikia matokeo hayo kwa madai kuwa Kibaki ameshinda kwa udanganyifu na tayari hata Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) iliyoyatangaza matokeo hayo, imeonyesha kuwepo kwa wasiwasi wa uhalisi wa matokeo hayo.


Pamoja na mambo mengine, vurugu hizo zimesababisha zaidi ya Wakenya 5,400 kukimbilia Uganda, huku maelfu wengine wakijihifadhi katika vituo vya polisi, shule na makanisa baada ya nyumba zao kuchomwa moto au kuamua kuyakimbia mapigano katika maeneo yao.


Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa, zimeshaonya kuwa watu hao wanahitaji msaada wa haraka kwani hawana chakula wala maji.


Naye msemaji wa Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), Sara Cameron, alisema kuwa wanawake na watoto ndio walioathirika kwa kiasi kikubwa na vurugu zilizotokea.


“Pamoja na kuwa wengi wa waathirika walioko hospitali ni wanaume, lakini watoto ndio wanaoumia zaidi. Wengi wao wanasumbuliwa na unyafuzi hasa katika majimbo ya Magharini na Nyanza,” alisema.


Alisema shirika lake lina chakula na dawa za kuwatosheleza watu 100,000.


Wakati juhudi zinafanyika kufikisha misaada katika maeneo yaliyoathirika zaidi na vurugu hizo, Mkurugenzi Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Elizabeth Lwanga, ameonya kuwa msaada wa polisi unatakiwa kuhakikisha kuwa misafara hiyo ya misaada inafika maeneo inakokusudiwa.


Alikuwa akizungumza baada ya kikao cha taasisi 20 zisizo za kiserikali pamoja na taasisi za kidini ambazo zilikutana kujadili namna ya kupata misaada kwa ajili ya wahitaji.


Shirika la WFP nalo limesema kuwa linajitahidi kuwafikishia chakula watu zaidi ya 100,000 ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao katika eneo la Rift Valley.


Chama cha Msalaba Mwekundu kimeomba kiasi cha paundi za Uingereza milioni saba kwa ajili ya kupata misaada ya kuwasaidia watu hao.


Mwandishi wa BBC aliyeko Eldoret ambako watu 30 walikufa katika kanisa lililochomwa moto, alisema kuwa zaidi ya watu 30,000 hawana makazi.


Alisema kuwa takribani 10,000 kati yao wameweka makazi katika Uwanja wa Kanisa Katoliki, ambalo linaongoza jitihada za kuwasaidia watu wasio na makazi katika eneo hilo.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents