Habari

Ujambazi watikisa Bunge

KAMBI ya upinzani bungeni imeonyesha wasiwasi wake na uwezo wa majeshi nchini kudhibiti mipaka ya nchi na kuishauri serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha hali hiyo inarekebishwa.

Mwandishi Wa Tanzania Daima


KAMBI ya upinzani bungeni imeonyesha wasiwasi wake na uwezo wa majeshi nchini kudhibiti mipaka ya nchi na kuishauri serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha hali hiyo inarekebishwa.


Aidha, kambi hiyo imeonyesha wasiwasi wake kutokana na kuibuka kwa mtindo wa wafanyabiashara kutoa misaada kwa Jeshi la Polisi na kubainisha kuwa hali ikiachwa iendelee, kuna uwezekano wa kulipunguzia nguvu jeshi hilo katika kupambana na uhalifu.


Akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani baada ya kusomwa kwa bajeti ya Wizara ya Usalama wa Raia, Waziri Kivuli, Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe-CUF), alisema kuwa, wakati umefika sasa kwa Jeshi la Polisi kufanya kazi za ziada ili kuutokomeza kabisa ujambazi nchini.


“Ule wakati wa kupongezana umekwisha, ni lazima usimamizi wa uchumi wetu uende sambamba na ulinzi wa uhakika kwa raia na mali zao. Hasa ukizingatia tunao wawekezaji wa ndani na wa nje,” alisema.


Hata hivyo, Sanya alidokeza kuwa katika matokeo ya hivi karibuni, inaonekana kuwa hali ya mipaka ya nchi si shwari kama inavyoaminika.


“Hapa simaanishi baina ya nchi yetu na nchi jirani kisiasa, lakini hoja ni kwamba vipi raia kutoka nchi jirani kuingia na silaha nzito nzito yakiwamo mabomu ya kuzika na ya kutupa, SMG, bastola na risasi kadhaa na hata kupatikana na nguo maalumu za kujikinga na risasi?” alihoji waziri huyo kivuli.


Sanya alikuwa akizungumzia tukio la hivi karibuni mjini Arusha ambako raia wawili wa Kenya walikamatwa baada ya mapigano ya risasi na polisi yaliyodumu kwa takriban saa saba.


Pamoja na kiasi kikubwa cha fedha, watu hao walikutwa na fulana za kuzuia risasi, mabomu ya kutupwa kwa mkono, bunduki aina ya SMG, bastola pamoja na risasi.


Katika maoni yake Sanya alihoji vifaa hivyo ambavyo ni maalumu kwa shughuli za majeshi viliingiaje nchini?


“Hivi wameingizaje bidhaa hizi hatari kupitia mipakani au tuseme wamezipata hapa hapa nchini? Leo vijana wetu wanaofanya biashara ya kuingiza sukari kwa njia za panya huwa wanakamatwa mara zote kule mpakani Mbeya, lakini inashindikana kuwakamata raia kama hawa wa kigeni ambao hujiandaa kuja kufanya ujambazi na huwa wanapata fursa ya kuingia na silaha hizo nzito mpaka mijini bila ya kukamatwa?” alihoji.


Aidha, Sanya alisema kuwa, kuna uwezekano mkubwa kuwa fedha walizokamatwa nazo watu hao, ni sehemu ya fedha ambazo zilitumika kuwahonga raia au hata baadhi ya askari wasio waaminifu ili wapate kutekeleza azima yao ya ujambazi.


“Ni vyema sasa tukajipanga vyema maeneo ya mipakani hasa upande wa Arusha, kwani inaonekana kuna matetemeko si ya ardhi tu, bali hata ya ujambazi,” alisema.


Ingawa alisifia hatua za kuyasajili makampuni binafsi ya ulinzi, Sanya alionyesha wasiwasi wake makampuni hayo yanapopewa dhamana ya kulinda mipaka ya nchi kama ilivyotokea hivi karibuni katika mpaka wa Sirari mkoani Mara.


Alisema kuwa hatua ya kuikabidhi kampuni ya ulinzi binafsi kulinda mpaka wa Tanzania na Kenya, Sirari mkoani Mara haukuwa uamuzi wa busara.


“Bahati nzuri waandishi wa habari waliliona hilo na kulitolea taarifa na tunaipongeza Serikali kwa kuchukua hatua za haraka kuweka mambo sawa,” alisema.


Alilalamikia pia mazingira mabaya ya kufanyia kazi na pia idadi ndogo ya askari polisi nchini na kusema hali hiyo inadhoofisha uwezo wa utendaji wa askari hao.


Alibainisha kuwa wakati takwimu za kimataifa zinataka uwiano kati ya askari ya watu anaowalinda ni 1:400 hadi 600, hivi sasa nchini takwimu zinaonyesha kuwa uwiano huo ni 1:1,300.


“Hii ni kusema askari wa Tanzania ana kazi mara mbili kwa kulinganisha na kiwango hicho cha kimataifa. Lakini inawezekana pia ikawa uzito wa kazi yake ni mara 12 kwa kukosa vitendea kazi, mafao na huduma zisizoridhisha na uhaba wa elimu inayoendana na wakati kwa mujibu wa kazi zake,” alibainisha.


Sanya alitaka askari ambao wamepangiwa maeneo ya miji na mikoa kupatiwa vifaa vitakavyowawezesha kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.


Alipendekeza kwamba, kwa kuwa Jeshi la Polisi halikusanyi fedha nyingi kwa kuwa kazi zake ni za kutoa huduma, fedha kidogo zinazokusanywa kwa njia ya faini zibakishwe katika maeneo zinakokusanywa ili kuwawezesha kununua vitendea kazi.


Akionya kuhusu misaada ambayo Jeshi la Polisi linapatiwa na wafanyabiashara, Sanya alisema kuwa, chombo hicho kitafanya kazi vizuri iwapo kutaachwa kijitegemee au kisaidiwe na serikali tu.


“Tunapotoa tahadhari hii tunafikiri hakuna hata mmoja kati yetu asiyeelewa ubaya wa kukaribisha wafanyabiashara au watu binafsi kuingiza mikono yao katika Jeshi la Polisi. Kwa utendaji wa haki na uliotukuka kwa wananchi, chombo hiki kiachwe ili kijitegemee kiutendaji,” alisema.


Aliitaka serikali kutenga fedha za kutosha kulingana na mazingira halisi yaliyopo na kuwa suala la kuwa serikali haina fedha si vema likajitokeza yanapokuja masuala ya usalama.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents