Michezo

Ujio wa Everton Tanzania waisaidia SportPesa kuchaguliwa kwenye tuzo za FBA

Kampuni inayoongoza kwa michezo ya kubashiri duniani ya SportPesa imeteuliwa kwenye vipengele viwili kuwania tuzo za biashara ya mpira wa miguu za nchini Uingereza zijulikanazo kama Football Business Award (FBA) ambazo zimepangwa kufanyika Novemba 2 kwenye Ukumbi wa Iconic Tobacco Dock jijini London.

Everton mapema mwezi Julai mwaka huu walivyokuja nchini Tanzania

Tuzo hizo ambazo zitafanyika mwaka huu kwa mara ya sita, zinahusisha jumla ya taasisi 97 zilizoingia kwenye hatua ya fainali ambazo zimegawanywa kwenye vipengele 16.

SportPesa imepangwa kuwania tuzo mbili kwenye kipengele cha uhamasishaji bora wa nembo ya kampuni unaohusisha mpira wa miguu kupitia vilabu vya Everton na Hull City ambao ni washirika wao wakuu.

Katika kipengele hicho cha uhamasishaji bora wa nembo ya kampuni unaohusisha mpira wa miguu, SportPesa imepambanishwa na kampuni nyingine kubwa duniani za Nivea kupitia ushirika wake na klabu ya Liverpool sambamba na kampuni maarufu ya Virgin Media ambayo ni wadhamini wakuu wa klabu ya Southampton ya nchini humo.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya SportPesa Tanzania, Bwana Pavel Slavkov amepokea uteuzi huo kwa furaha huku akiamini jitihada kubwa zinazofanywa na kampuni hiyo katika harakati za kuendeleza mpira wa miguu duniani ndio kigezo kikubwa kilichowafanya kushindanishwa na makampuni makubwa duniani.

Ni jambo la kufurahisha na kutia moyo kuona jinsi ambavyo ulimwengu unatambua jitihada za dhati za kampuni yetu ya SportPesa katika kuendeleza mpira wa miguu duniani na ndio sababu kubwa ambayo inatufanya kuweza kushindanishwa na kampuni mashuhuri duniani kama vile Nivea na Virgin Media inayomilikiwa na tajiri maarufu duniani, Sir Richard Branson,”ameisema Bwana Pavel Slavkov .

Udhamini wa SportPesa kwa klabu ya Everton uliifanya klabu hiyo ambayo ni bingwa mara tisa wa Ligi Kuu nchini Uingereza kutembelea Tanzania katika sehemu yao ya maandalizi ya msimu mpya ikiwa ni timu ya kwanza kutoka nchini Uingereza kutembelea ukanda wa Afrika Mashariki.

Wakiwa nchini Tanzania, Everton waliweza kufanya shughuli mbalimbali za kijamii kama vile kutembelea timu ya mpira wa miguu ya watu wenye ulemavu wa ngozi ya Albino United, hifadhi ya wanyama ya Ngorongoro, shule ya wanafunzi wenye ulemavu ya Uhuru Mchanganyiko pamoja na kuendesha semina mbalimbali za kuwaongezea uwezo makocha, viongozi wa mpira pamoja na wachezaji chipukizi wa vilabu vya Simba na Yanga.

Sambamba na shughuli zote hizo lakini Everton ilipata fursa ya kucheza na mshindi wa SportPesa Super Cup, klabu ya Gor Mahia Julai 13 kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam ikiwa ni mechi yao ya kwanza ya maandalizi ya msimu mpya ambapo waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Shughuli zote hizo ambazo zilifanywa na Everton kwa kipindi ambacho walikuwepo nchini Tanzania ndizo zimepelekea ushirika wao huo kuteuliwa kuwania kipengele cha uhamasishaji bora wa kampuni kupitia mpira wa miguu (Best Brand Activation involving Football).

Sambamba na ziara ya Everton nchini Tanzania kuweza kuteuliwa kuwania tuzo kwenye kipengele hicho, lakini pia Kampuni ya SportPesa imeteuliwa kwenye kipengele hicho kwa mara nyingine kupitia udhamini wake kwa klabu ya Hull City ambayo tayari imeshafanya ziara mbalimbali nchini Kenya pamoja na kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya nyota wa Ligi Kuu ya Kenya iliyopigwa Februari mwaka huu.

Huu utakuwa ni uteuzi mwingine kwa kampuni ya SportPesa kuwania tuzo za kimataifa baada ya miezi mitatu iliyopita kutwaa tuzo mbili kwenye tuzo za Discovery Sports Industry Awards zilizofanyika jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Katika tuzo hizo, SportPesa ilinyakua tuzo kwenye kipengele cha kampeni bora ya kimasoko ya “Made Of Winners” kwa nchi za Afrika sambamba na Udhamini bora kupitia mashindano ya Super 8.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents