Habari

Ukweli uliofichika kuhusu matumizi ya Mirungi (khat)

Ina ladha ya uchachu mkali na utamu wa mbali kwa wakati mmoja.

Hufungwa katika majani ya migomba ili kuhifadhi ubichi wake. Kawaida huvunwa asubuhi sana na kuuzwa mchana wake au usiku wake, kila inavyokaa sana hupunguza ubora wake kwa walaji na thamani yake. Na kwa sababu walaji wa Tanzania hutegemea zaidi Mirungi kutoka Kenya, huwa hawapati ule ubora unaopakikana kutokana na umbali na kutofika kwa haraka; ingawa walaji wa Arusha hupata haraka zaidi kwa ukaribu wake na Nairobi kuliko wale wa Dar na Zanzibar au miji ya bara ya mbali kama Mwanza na kwengineko.

Mirungi (Khat) au (Catha edulis) Ni mmea au mti unaoota au kuoteshwa. Mirungi ni mti unaoota polepole ambao unakuwa kwa urefu wa mita 1.5 hadi mita 20, kutegemea na eneo kijiografia na pia hali ya mvua ya eneo. Likiwa na majani ya kijani yaliyokoza ambayo yana urefu wa sentimeta 5 hadi 10 na upana wa sentimeta 1 hadi 4.

Kemia ya Mirungi (khat)

Muundo wa Cathinone

Mirungi (khat) inakusanya ndani yake alkaloid mbili ambazo ni Cathine na Cathinone. Alkaloid hizi zinafanana sana na familia ya kundi la kemikali linaloitwa PPA ( phenylpropanolamine) ambalo ni kundi dogo la phenethylamines linalofanana na kundi la kemikali la catecholamine na amphetamine kama kichangamsho (stimulant) ambayo inasemekana husababisha msisimko, uchangamfu, kuwa na aina ya furaha ya kuwazika –kuhandasika- na huondosha hamu ya kula na kusababisha ukosefu wa usingizi.

Tuachane na haya ya kikemia. Uvunaji wa mirungi huhitaji umakini wa hali ya juu kwani kemikali mojawapo ambayo ni cathinone hupotea hewani kirahisi kama kama mmea huu utaachwa ukauke ndani ya masaa 48, hivyo bhasi wavunaji huhifadhi mirungi kwenye mifuko ya plastiki na kuizungushia majani ya migomba kipindi wanasafirisha ili kuifanya isipoteze kemikali muhimu ya cathinone. Wakati mwingine huzihifadhi ndani ya maji ili zisipoteze ubora wake.

Mnamo mwaka 1980 WHO (Shirika la Afya Duniani) liliiweka Mirungi katika fungu la madawa ya kulevya ambayo inasababisha nafsi kutawaliwa nayo au kuwa na uraibu (addiction) kwa daraja ya kati hadi ile yenye nguvu. Watumiaji wake hujitetea kwa kuamini kuwa majani hayo huwapatia nguvu, na uchangamfu na mliwazo wa furaha.

Madhara ya muda mfupi yatokanayo na matumizi ya mirungi (khat)
• Kujiamini kupita kiasi
• Magonjwa ya vidonda vya tumbo (ulcers)
• Shikizo la damu
• Ukosefu wa hamu ya kula chakula (loss of appetite)
• Upungufu wa hayaa na Kukosa usingizi (insomnia)
• Kuongezeka kwa mapigo ya moyo
• Kukosa haja kubwa (constipation)
• Uropokaji, uchache wa adabu, ujuaji wa kila kitu
• Kukosa usikivu na utulivu
• Magonjwa ya akili
• Tahadhari


Madhara ya muda mrefu

• Huzuni/mfadhaiko wa mawazo
• Upungufu wa msukumo wa kufanya jimaa (sex drive). Na pia kuwahi kumaliza haraka na kutoweza kudumu kwenye tendo la ndoa kwa muda mrefu (pre-ejakulation)
• Humpelekea mlaji kutawaliwa nayo (Addiction)
• Msongo wa mawazo
• Kupata njozi zinazojirudia rudia
• Mahangaiko ya akili
• Kushindwa kujizuia kufanya vitendo visivyofaa kwenye jamii.
• Kuwa kwenye hatari kubwa ya kupata Shambulio la moyo
• Utumiaji wa muda mrefu husababisha kuharibu utendaji kazi wa ini, na pia kusababisha ubadilikaji rangi meno, kudhoofika, na fizi kuuma na harufu ya mdomo
• Kansa ya mdomo

Athari zisizozuilika
• Kifo
• Kiharusi kutokana na shambulio la moyo

Your Health, My Concern

IMEANDIKWA NA:
FORD A. CHISANZA
Scientist/Researcher
Intern pharmacist
Location: Off Mandela Road, Mabibo – External,
P.o.Box: 77150, Dar Es Salaam, Tanzania.
Mobile:+255 652466430/+255 684363584
Email: [email protected]
[email protected]

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents