Ulinzi unahitajika kwa Dada zake Balali

Baadhi ya wakazi jijini Dar es Salaam wameitaka serikali iwapatie ulinzi dada zake na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania BOT

Baadhi ya wakazi jijini Dar es Salaam wameitaka serikali iwapatie ulinzi dada zake na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania BOT, Hayati Dk Daud Balali kutokana na ukweli kwamba vigogo wamekuwa na hofu kubwa ya kwamba bomu wanaloweza kulilipua wanawake hao wanaweza kufanya lolote ilimradi wanusurike kwenye kashfa ya ulaji wa Shilingi bilioni 133 zilizochotwa na kuzua kashfa ya ufisadi.


Kinadada hao wanaojuikana kwa majina ya Magreth na Elizabeth, ambao wako nchini Marekani kuhudhuria mazishi, imeelezwa kwamba baada ya msiba kumalizika, wanatarajia kuja Dar es Salaam kuanika kilichoko kwenye waraka aliouacha marehemu Balali kuhusiana na kashfa hiyo ya EPA.


Magreth na Elizabeth watawapa nafasi waandishi wa habari kupata majibu ya maswali ambayo walikuwa wakiyatafuta kwa udi na uvumba kutoka serikalini bila mafanikio.


Wakati wanawake hao wakisubiriwa kwa hamu na waandishi wa habari pamoja na umma kwa ujumla, mdogo wake na marehemu aitwaye Pascal Balali amezungumza na waandishi akiwa kijijini kwao, Luganga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa akisisitiza kuwa mazingira ya kifo cha kaka yake yanaonyesha kuwa pana mkono wa mtu umehusika kwa namna moja au nyingine.


“Mazingira ya kifo cha Balali yamekuwa na utata mkubwa sana, Baada ya kuzushiwa kashfa tukasikia amepelekwa nje kutibiwa. Ugonjwa haukuisha hadi kifo chake. Ni suala la kusubiri tu,” amesema Pascal Balali alipozungumza leo asubuhi na mwandishi wetu aliyeko Iringa.


Baba zake wadogo waliokuwa wamekusanyika nyumbani kwao wameeleze kushutushwa kwao na msiba huo mzito wa ndugu yao ambao wamesema umewaachia pengo kubwa katika familia.


Kutokana na hali hiyo wakazi kadhaa wa Dar es Salaam wamependekeza wanawake hao dada ambao ni dada zake marehemu wapewa ulinzi mkali kutokana na yaliyokuwa yakifanyika baada ya marehemu kwenda kutibwa na mazingira yenyewe ya kifo.


“Hawa watu wanastahili ulinzi vinginevyo lolote laweza kuwatokea. Kwanza serikali yenyewe ilikuwa haipendi kueleza aliko Balali na mbaya zaidi hata habari za kifo chake zilikuwa kama zimefichwa. Hapo unategemea nini,” amesema mkazi wa Sinza Kijiweni, Omar Baraka.


Mkazi mwingine wa Mikocheni, Edwin Makoye, akizungumzia kuhusu suala hilo amesema Marehemu Balali alikuwa mtuhumiwa muhimu kuliko wote katika sakata la ufisadi wa Sh bilioni 133 walizochotewa wafanyabiashara 22 na kwamba nyaraka yoyote kuhusu fedha hizo ni mwiba mchungu kwa wanaochunguzwa.


“Uzoefu unaonyesha kwamba mtu anayejua siri zote hususan katika kashfa kubwa kama hii, maisha yake huwa yako hatarini siku zote. Sasa kama hawa wanawake wamejitoa mhanga kutoboa siri yanaweza kuwakuta. Serikali yenyewe inapaswa kutoa tamko rasmi la kuwalinda ili wawe salama popote watakapokuwa kabla ya kulipua bomu,” amesema Makoye ambaye kitaalama ni mwanasheria.


Kifo Balali kiltokea nchini Marekani Ijumaa iliyopita kimezua utata mkubwa kutokana na habari zake kuchelewa kutangazwa kwa umma. Balali alifariki dunia katika Jimbo la Boston nchini Marekani, lakini habari zake zikafichuliwa na gazeti moja la kila siku tena siku tano baada ya kifo hicho kutokea.


Dk Balali alikuwa akituhumiwa kuidhinisha Sh Bilioni 133 kutoka katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na kuzigawa kwenye makampuni 22 isivyo halali.


Baada ya kashfa hiyo kufika Bungeni, Dk. Balali alijitetea mbele ya waandishi wa habari kwamba anasingiziwa na kwamba yeye hana wasiwasi kuhusu tuhuma hizo. Siku chache baadaye baada ya tuhuma kuwa nzito zaidi, Dk Balali alikwenda nje ya nchi kinyemela kutibiwa.


 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents