Habari

Umeme utaendelea kukatika-Tanesco

Tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara, huenda likaendelea kutokana na uchakavu wa mfumo wa miundombinu ya usambazaji wa nishati hiyo, imefahamika.

Na Dunstan Bahai



Tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara, huenda likaendelea kutokana na uchakavu wa mfumo wa miundombinu ya usambazaji wa nishati hiyo, imefahamika.


Hayo yalibainika jana baada ya Meneja Uhusiano wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Bw. Daniel Mshana, kutoa ufafanuzi kuhusiana na tatizo la kukatika kwa umeme lililotokea usiku wa kuamkia jana.


Akifafanua juu ya kukatika kwa umeme usiku huo, Bw. Mshana alisema tatizo hilo lilisababishwa na hitilafu ya mitambo ya kuzalisha nishati hiyo iliyopo Kidatu, mkoani Morogoro.


Kwa mujibu wa Bw. Mshana, tatizo hilo liliwaathiri wateja wote waliounganishwa kwenye gridi ya Taifa, ikiwemo Zanzibar.


Alisema, hitilafu ya mitambo hiyo ya Kidatu ilianza matatizo saa 10:45 usiku wa kuamkia jana na kurejea saa 12:27 asubuhi.


Alitaja matatizo yanayolikumba shirika hilo na kusababisha kukatika katika kwa umeme kuwa ni uchakavu wa mfumo huo mzima wa mitambo ya usambazaji wa nishati hiyo ambayo tangu kuwekwa kwake miaka mingi iliyopita, haijabadilishwa na badala yake inafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara.


Katika kulipatia utatuzi suala hilo, Bw. Mshana alisema, uongozi wa shirika umeanza jitihada za kutafuta wafadhili, ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Misaada la Sweden na wafadhili wengine mbalimbali.


Matatizo mengine ni pamoja na wizi wa mafuta ya transfoma ambapo usiku wa kuamkia jana peke yake wezi waliiba mafuta hayo kwenye transfoma mbili za Mbweni kwa Masister yenye nguvu ya kVA 200 na ile ya Victoria Makumbusho yenye nguvu ya kVA 315.


�Kwa kweli inakera sana, pamoja na shirika kujitahidi katika kuboresha huduma zake kwa wateja pamoja na uchakavu wa mitambo uliopo, lakini jitihada hizo zinakwamishwa na watu wachache, kwakweli inakera sana,� alisema mshana kwa uchungu.


Kuhusu matatizo ya kukatikakatika umeme kwa muda mfupi na kisha kurejea hasa katika Jiji la Dar es Salaam, Meneja Uhusiano huyo wa Tanesco alisema, kutokana na tahadhari ya kuwepo kwa mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, shirika nalo linajiandaa ili mvua hiyo isilete madhara kwenye mfumo wa umeme.


Miongoni mwa tahadhari ambazo shirika linachukuwa alizitaja kuwa ni pamoja na kuondoa nguzo zilizochakaa na kuweka mpya, kubadilisha baadhi ya vifaa pamoja na kukata matawi ya miti yaliyo jirani na nyaya za kusafisha umeme.


Hata hivyo, aliwataka wananchi waliopo karibu na transfoma, kuwa walinzi kwani kuibwa kwa mafuta hakulisababishii shirika tu hasara bali pia wananchi wenyewe.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents