Habari

Umuhimu wa teknolojia ya habari watambuliwa

SERIKALI inatambua umuhimu wa sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano kwa maendeleo ya Taifa na ndiyo maana suala hilo si tu limetungiwa sera bali pia ni moja ya vipaumbele katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025

Na Said Ameir, Bagamoyo


SERIKALI inatambua umuhimu wa sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano kwa maendeleo ya Taifa na ndiyo maana suala hilo si tu limetungiwa sera bali pia ni moja ya vipaumbele katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025


Kauli hiyo ilitolewa jana na Makamu wa Rais, Dkt. Ali Mohamed Shein, wakati akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Kimataifa juu ya Mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano unaofanyika mjini hapa.


Dkt Shein alisema mfumo wa teknolojia ya habari na mawasilino ni nyenzo muhimu katika kuharakisha maendeleo na utoaji huduma katika jamii na ndiyo maana Dira ya Taifa ya Maendeleo, inasisitiza matumizi ya teknolojia katika kuboresha maisha ya Watanzania na pia nyenzo ya kuwawezesha kukabiliana na ushindani katika medani za kimataifa.


“Kwa hiyo Serikali imekuwa ikifanya kila jitihada kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, uingizaji na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika mipango yetu ya maendeleo na uendeshaji wa Serikali,” alifafanua.


Aliongeza kuwa hivi sasa mbali ya mitaji na nguvukazi lakini habari na mawasiliano ni muhimu katika uzalishaji hivyo ametoa mwito kuwa matumizi yake yasiwe kwa watu wachache kama ilivyo sasa.


Alikosoa hali ya sasa ya maendeleo na uwekezaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano kunufaisha zaidi watu wa mijini na kuwaacha vijijini bila huduma hiyo muhimu.


Alitoa changamoto kwa washiriki wa mkutano huo kupendekeza namna ya kuhakikisha teknolojia ya habari na mawasiliano haiendelei kuwa bidhaa adimu katika jamii, ambapo alisema inapoendelea kuwa hivyo athari zake ni kuwatenga wengi katika shughuli za kiuchumi.


Naye Naibu Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia Bibi Gaudensia Kabaka, alibainisha kuongezeka kwa kasi kwa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kuwa kunaletea kuongezeka kwa pengo kati ya watu maskini na matajiri, watu mijini na vijijini na pia kati ya walio kwenye mtandao na wasio kwenye mtandao.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents