Tragedy

Updates: Aliyemuua mama yake Ufoo Saro alipanga kuua familia nzima, mdogo wake asimulia

Kwa mujibu wa mdogo wake na mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha ITV, Ufoo Saro aitwaye Goodluck aliyekuwepo wakati wa tukio la mauaji lililotokea asubuhi ya jana, ambapo mchumba wa Ufoo alimuua mama yake mtangazaji huyo, na pia yeye kujeruhiwa kabla ya mtu huyo aitwaye Anthery Mushi kujiua pia.

0L7C0700

“Tulisikia sauti ya risasi sebuleni…na hapo mama akawa anatuita anasema njooni hapa nakufa, tulipotoka nje tukakuta na dada nae ndo yuko chini, akatuambia rudini ndani anataka kutuua wote hawa, ndo tukarudi ndani. Baada ya kurudi ndani ndo akaanza kupiga risasi milangoni na madirishani akawa anasema tokeni nje nataka niwauwe,” Goodluck alikiambia kituo cha radio cha Times FM.

“Na sisi tukakimbia tukapanda juu dalini baada ya kusikia mlango wetu umeshapigwa sana risasi na dirishani, tukapanda juu ya dali, baada ya kupanda juu dalini tukasikia mlio wa risasi mbili zinalia tena sebuleni na hatukuwezi kutoka kule juu dalini. Baadae akatoka akaenda kufungua gas akawasha moto wa gas, sasa moshi ukawa unakuja kule juu dalini na hatuwezi kupumua, tukaja tukakuta jiko la gas lile limewaka liko karibu na pikipiki.

Baada ya polisi kuja na kuzunguka nyumba tukakuta mtu mwenyewe amekaa kwenye kochi na yeye kajiripua risasi. Tukaulizia dada yuko wapi tukaambiwa wamemuona dada mmoja hapa amechafuka damu amepelekwa Tumbi na pikipiki, ndo baada ya kufuatilia ndo tunasikia amepelekwa Muhimbili.”

Ufoo Saro amelazwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili na tayari amefanyiwa upasuaji. Jana kamishina msaidizi wa upelelezi kanda maalum ya Dar es Salaam Hemed Msangi,amesema kuwa Ufoo amejeruhiwa eneo la mkononi, begani na tumboni na hali yake inaendelea vizuri.

Sababu za tukio hilo bado hazijafahamika lakini kwa mujibu wa chanzo kimoja, linaweza kuwa limetokana na ugomvi wa kimapenzi kati yao.

“Alikuwa mume mtarajiwa wa Ufoo ila jamaa alikuwa akifanya kazi UN nchini Sudan Kusini ingawa kitengo chake bado hakijafahamika ila kwa habari za mtaani zisizokuwa na uhakika wanasema alikuwa mwanajeshi. Anaitwa Mushi. Bwana mushi alikuwa na mgogoro na Ufoo mpenzi wake ila mama mkwe akawa anamtetea Ufoo. Huyu dada alikuwa na mtu wa pembeni ikabuma. NIPO ENEO LA TUKIO,” kimesecha chanzo hicho japo binafsi Bongo5 haijazithibitisha.

Jana Jamii Forums waliandika:

Inasemekana kulikua kuna ugomvi kati ya wawili hao ambapo walishindwa kuelewana na ndipo walipoamua kwenda kwa mama mzazi wa Ufoo Saro(mama mkwe) ili awasuluhishe.

Baada ya usuluhishi kuanza na kuonekana kuwa tatizo liko kwa mwanaume, mwanaume huyo alimshutumu mama mkwe wake kwamba amekuwa na mazoea ya kumtetea mwanae na ndipo alipotoa bastola na kumpiga mama yake na Ufoo Saro risasi ya kichwa na kumuua papo hapo…. Alipomuua mama huyo, mwanaume huyo alimpiga Ufoo Saro risasi mbili, moja ya tumboni na nyingine ya mguuni na kudhani kwamba amemuua kumbe amemjeruhi tu kisha kujipiga mwenyewe risasi ya kidevuni na kufariki dunia hapo hapo.

Inadaiwa kuwa kufuatia tukio hilo polisi waligawanyika katika timu tatu ambapo moja ipo Muhimbili, ya pili Kibamba yalipotokea mauaji na ya tatu inashughulika mtaani kutafuta taarifa muhimu za mauaji.

Source: Jamii Forums, ITV, Michuzi, Mchomeblog, Times FM Blog

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents