Habari

Upelelezi kesi ya bosi wa Jamii Forums wakamilika

Upelelezi wa kesi ya kuzuia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi, inayomkabili Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kampuni ya Jamii Media Limited, Maxence Melo (40), umekamilika.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 13 mwaka huu, baada ya upande wa mashitaka kuomba muda wa kujipanga zaidi ili kusoma maelezo ya awali ya mshitakiwa.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Mohammed Salum amedai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

Pia aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kujipanga kumsomea mshitakiwa maelezo ya awali. Hakimu Mwambapa aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 13 mwaka huu, kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Melo anakabiliwa na mashitaka manne katika mahakama hiyo kwa mahakimu watatu tofauti ambao ni Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa na Hakimu Mwambapa.

Inadaiwa kuwa kati ya Aprili Mosi na Desemba 13, mwaka jana maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo inayoendesha tovuti ya Jamii Forum, alishindwa kutoa taarifa kuhusu miliki hiyo huku akijua kwamba jeshi hilo linafanya uchunguzi wa makosa ya jinai yaliyochapishwa kielektroniki kwenye tovuti hiyo.

Pia inadaiwa mshitakiwa alizuia jeshi hilo kufanya uchunguzi kinyume na Sheria Namba 22 (2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao Namba 14 ya mwaka 2015.

Salum amedai kuwa kati ya Mei 10 na Desemba 13 mwaka jana maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni, akiwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, alilizuia jeshi hilo kufanya uchunguzi kwa kushindwa kutoa taarifa zilizochapishwa na tovuti hiyo.

Aidha, katika kesi ya tatu, mshitakiwa alikabiliwa na mashitaka mawili ikiwemo la kuendesha mtandao kwa usajili usio wa Tanzania na kuzuia jeshi kufanya uchunguzi.

Wakili Salum amedai kuwa, kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13 mwaka jana, maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni, akiwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, alisajili tovuti ya Jamii Forum kwa kikoa cha .com badala ya .co.tz jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Alidai alifungua kampuni hiyo kwa Sheria ya Makampuni Namba 212 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kutumia cheti namba 66333.

Aidha, ilidaiwa kati ya Januari 26 na Desemba 13 mwaka jana, maeneo ya Mikocheni akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media inayoendesha mtandao wa jamiiforums huku akijua kwamba jeshi la polisi linafanya uchunguzi wa makosa ya jinai, yaliyochapishwa kwenye mtandao huo, alizuia jeshi hilo kwa kushindwa kutoa taarifa.

By: Emmy Mwaipopo

Chanzo: Habarileo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents