Habari

Urasimu bandarini wakera wabunge

UTATA wa umiliki wa kampuni ya Kukagua na Kuthamini Mizigo Bandarini (T-Scan) umechukua sura nyingine, baada ya baadhi ya wabunge kuitaka serikali kutaja mmiliki wa kampuni hiyo, ambayo wamedai imejijengea himaya ya urasimu na inanuka rushwa.

Na Midraji Ibrahim, Dodoma


UTATA wa umiliki wa kampuni ya Kukagua na Kuthamini Mizigo Bandarini (T-Scan) umechukua sura nyingine, baada ya baadhi ya wabunge kuitaka serikali kutaja mmiliki wa kampuni hiyo, ambayo wamedai imejijengea himaya ya urasimu na inanuka rushwa.


Wabunge hao walitoa dukuduku lao katika kikao cha kujadili utekelezaji wa bajeti ya serikali katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2007/2008, kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.


Mbunge wa Solwa (CCM), Ahmed Ally Salum, alisema yuko tayari kujitolea mwezi mmoja bila mshahara kumsaidia Waziri wa Fedha, Zakia Meghji na kuahidi kuwa mapato yataongezeka kwa asilimia 20.


Salum alisema kinachosababisha mapato ya serikali kutoongezeka ni urasimu uliowekwa na T-Scan ambao husababisha mzigo kukaa zaidi ya siku 30, huku wafanyabiashara wakikata tamaa na kuhamishia mizigo yao katika bandari ya Mombasa.


“Urasimu wao wanauita kuwa ni udhibiti…tungeweza kutengeneza T-Scan yetu ikawa chini ya TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) au Wizara ya Fedha ambayo itakuwa na uwezo wa kufanya marekebisho,” alisema mbunge huyo na kuongeza kuwa, kampuni hiyo hukaa na nyaraka kwa muda mrefu na baadaye hutoa makadirio ambayo yanawakatisha tamaa wafanyabiashara.


Mbunge wa Longido (CCM), Lekule Laizer, alisema kazi inayofanywa na T-Scan inaweza kufanywa na TRA kwa ufanisi mkubwa na kwamba wamekuwa watu wa ajabu wanaopinga hata bei ya gari iliyonunuliwa.


“Ni watu wa ajabu wanakubishia hata bei ya gari lako! pale pamejaa rushwa. Ningependa kujua ni ya nani?” alihoji Laizer.


Pia suala la kampuni hiyo lilizungumziwa na Mbunge wa Pangani (CCM), Mohamed Rished Abdallah, ambaye alisema ni kero na tatizo kubwa kwa uchumi wa taifa na kwamba serikali inapoteza fedha nyingi kwa ukaguzi wa magari nje ya nchi, ikiambulia dola 10 wakati mwenye gari analipa dola 200.


Susan Lyimo (Viti Maalum-Chadema), alisema kasi ya ukusanyaji mapato inayofanywa na TRA inakwamishwa na matumizi mabaya ya serikali na kuhoji zaidi ya Sh160 milioni zilizotumika wakati Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alipowaita viongozi wa mikoa kwa ajili ya kujadili suala la elimu, wakati tayari walishapewa semina elekezi.


Hata hivyo, Lowassa alimjibu kuwa Sh160 milioni zilisababisha kujengwa kwa shule 900 za sekondari.


Lyimo alisema katika kipindi kifupi, kupanda kwa mfumko wa bei kunampa wasiwasi na akaeleza wasiwasi wake kwamba mfumuko huo hautashuka.


Mbunge wa Mikumi (CCM), Clemence Lyamba, alisema, mfumo wa viongozi wanaofuja fedha za umma kulindana, bado ni mzimu unaowasumbua na kuongeza kuwa, iwapo hali hiyo itaendelea, wnanchi watazidi kukata tamaa.


Mbunge wa Kondoa Kusini (CCM), Pascal Degera, alisema taarifa nzuri zinazotolewa kwenye makaratasi sio hali halisi waliyonayo wananchi.


“fedha ya maji tunayopitisha hapa haifiki katika maeneo tunayopanga, utekelezaji wa bajeti hakuna nasema hatujafanya lolote, badala yake fedha za maji utasikia zimehamishiwa kwenye dharura,” alisema Degera.


Juma Kilimba (Iramba Mashariki-CCM), alisema iwapo serikali katika bajeti ijayo haitaweka kipaumbele kumaliza barabara ya kati, wananchi hawataelewa kwa sababu imekuwa kero kubwa na isiyomalizika.


Alipotakiwa kujibu hoja mbalimbali za wabunge, Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya, hakutaja mmiliki wa kampuni T-Scan zaidi ya kusema kuwa, waliitisha zabuni na kampuni nyingi zilishiriki na yenyewe ilishinda kwa vigezo vilivyowekwa.


Kuhusu urasimu uliolalamikiwa na wabunge, Kitilya alisema serikali inafanya marekebisho ambayo yanatarajiwa kuzaa matunda hivi karibuni na kuongeza mapato ya serikali kwa kiwango cha kushangaza.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents