Habari

Usafiri wa bajaj balaa

Usafiri wa bajaj balaa
Ni dhahiri sasa usafiri wa pikipiki ya miguu mitatu aina ya bajaj ni
hatari kwa usalama wa abiria baada ya kugundulika kwamba katika kipindi
cha miezi mitatu tu zimehusika katika ajali zilizoua watu 591 nchini

Sambamba na vifo hivyo, bajaj zimethibitika kusababisha ajali 4,202 katika kipindi hicho.

Kutokana na hali hii inayotishia usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini Nchini (Sumatra) imesema usafiri wa bajaji kuwa si salama kwa matumizi ya mijini.

Kadhalika Sumatra imeonya kwamba kama wamiliki wa bajaj wataendelea kupuuza sheria za barabarani, serikali inaweza kuangalia upya kuruhusu ama kuzuia usafiri huo kutumika kwa kuwa umeonekana kuwa ni hatari kwa usalama wa abiria wake.

Msimamo huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Israel Sekirasa, kwenye mkutano wa wadau waliokutana kwa ajili ya kujadili athari za matumizi ya bajaj nchini.

Alisema usafiri huo haufai katika maeneo ya mijini ambayo yana msongamano wa magari kwa kuwa zinachangia kusababisha ajali nyingi za barabarani.

Mapema mwaka huu serikali ilipeleka mswada bungeni kuruhusu usafiri wa bajaj kutumika kubebea abiria. Pia usafiri wa pikipiki kubeba abiria nao uliruhusiwa.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili watu walikuwa wanatumia bajaji kiholela kwa ajili ya kusafirisha abiria na kwamba katika kipindi chote hicho serikali imekuwa ikitafakari athari zinazotokana na usafiri huo kabla ya kuuruhusu rasmi.

Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani (Trafiki), James Kombe, aliwaagiza wamiliki wa bajaj kuziba mlango wa kulia wa abiri kwa kutumia vyuma (nondo) ili usitumike kabisa.

Alisema matumizi ya mlango wa kulia ni hatari kwa kuwa mara nyingi abiria wanaoshukia huko hupata ajali kirahisi. Aliwaambia wadau hao kuwa madereva wengi wa bajaji hawajui sheria na baadhi wanazijua, lakini wanazivunja kwa makusudi hali inayosababisha kuwepo kwa ajali nyingi za barabarani.

Kamanda Kombe alikerwa na tabia ya madereva ya bajaji ‘kuchomekea’ kwa kuwa ni hatari na itaendelea kuongeza ajali za barabarani kwa kuhusisha vyombo vingine vya usafairi yakiwemo magari, mikokoteni na baiskeli.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa chama cha wenye bajaji, Adam Yelu, alisema ajali nyingi za bajaji zinatokana na madereva wengi kutokuwa na ujuzi wa kuziendesha.

Alisema nchi mbalimbali duniani zinatumia usafiri huo, lakini ajali ni chache ukilinganisha na hapa nchini kwa madereva wao wana ujuzi wa kutosha.

Mkutano huo ulihusisha wadau mbalimbali ikiwemo serikali, wamiliki wa bajaji, Jeshi la Polisi na madereva wa bajaji.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents