Michezo

USAJILI: Azam FC yanasa saini ya straika Ghana

Uongozi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imemsajili mshambuliaji, Bernard Arthur akitokea Liberty Professional ya Ghana.

Arthur amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, na zoezi zima limefanikishwa na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohammed, aliyekuwepo nchini Ghana kukamilisha usajili wake.

Usajili wa Arthur mwenye umri wa miaka 20, ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi la timu hiyo kwenye usajili huu wa dirisha dogo, anayekuja kuziba pengo la straika mwingine, Yahaya Mohammed, aliyeondoka kwa makubaliano maalumu ya pande mbili wiki chache zilizopita.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa timu ya WAFA (Ghana) na Asec Mimosa ya Ivory Coast, anaungana na washambuliaji wengine wa timu hiyo katika kukiongezea makali kikosi hicho, ambao ni Mbaraka Yusuph, Wazir Junior, Yahya Zayd, Shaaban Idd pamoja na wale waliopandishwa kutoka Azam B, Paul Peter na Andrea Simchimba.

Liberty Professional ni moja ya kitovu kikubwa cha kutoa mastaa wa baadaye nchini Ghana, wachezaji waliotesa barani Ulaya waliowahi kupitia hapo ni nyota wa zamani wa Chelsea, Michael Essien, Sulley Muntari (Pescara, Italia) na Asamoah Gyan (Kayserispor, Uturuki).

Azam FC inamatumaini makubwa kuwa usajili wa nyota huyo, utaweza kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji na kutatua tatizo la ukosefu wa mabao linaloonekana, hii ikitarajia kuendeleza mbio za kuwania taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania walizozianza vema hadi sasa.

Arthur aliyekuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya vijana ya Ghana chini ya umri wa miaka 20 (Ghana U-20), ni mmoja wa washambuliaji bora kwa sasa katika Ligi Kuu nchini Ghana (GPL), msimu huu akifunga jumla ya mabao 11, tisa akifunga ndani ya ligi hiyo na mawili (Kombe la FA).

Moja ya sifa zake kubwa ni uwezo wa kumiliki mpira na kuwatoka mabeki wa timu pinzani kwa spidi, kukaa na mipira na kusambaza kwa wachezaji wenzake, kutumia vizuri miguu yote miwili, uwezo wa kupiga mashuti kwenye eneo lolote la ushambuliaji pamoja na kusaidia ukabaji pale timu pinzani inapokuwa ikishambulia.

Arthur alianzia soka lake katika timu ya Mighty Cosmos kwenye eneo alilozaliwa na kukulia la Dansoman nchini Ghana, akiwa kijana mdogo mwaka 2005-2010.

Cosmos aliyoanzia soka lake Arthur, pia wamewahi kucheza nyota wengi wa soka la Ghana wakiwamo nahodha wa zamani na timu ya Taifa ‘Black Star’, Stephen Appiah na Michael Essien.

Mbali na kucheza Liberty, mshambuliaji huyo pia amewahi kucheza kwa mabingwa wa msimu uliopita nchini Ghana, WAFA huku pia akiwahi kutolewa kwa mkopo kujiunga na vigogo wa Ivory Coast, Asec Mimosa.

Nyota huyo anavutiwa na staa wa Ghana, Asamoah Gyan, ambaye ndiye mfano wake wa kuigwa (role model), ambapo anapenda siku moja wacheze naye pamoja katika timu Taifa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents