Michezo

USAJILI: Simba SC sasa hizi kufuru yampa mkataba Golikipa Bora COSAFA

Klabu ya Simba imeendelea kujiimarisha kwa kumsajili kipa Said Mohammed Mduda kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Golikipa, Said Mohammed Mduda 

Mduda amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Wekundu hao wa Msimbazi, kabla ya kusafiri na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars leo kwenda Rwanda, kwa sasa ni kipa wa namba mbili kwa Taifa Stars baada ya Aishi Salum Manula ambaye pia amesajiliwa Simba SC kutoka Azam FC dirisha hili.

Kipa huyo wazamani wa Yanga SC aliteuliwa kuwa kipa bora wa michuano ya Kombe la COSAFA Castle nchini Afrika Kusini mwezi uliopita licha ya kudaka mechi moja tu ya kusaka mshindi wa tatu, akimpiku Manula aliyedaka mechi zote tano za awali.

Manula alidaka Stars ikishinda 2-0 dhidi ya Malawi, ikitoa sare ya 0-0 na Angola, 1-1 na Mauritius, ikishinda 1-0 dhidi ya Afrika Kusini na katika kipigo cha 4-2 dhidi ya Lesotho, lakini haikumsaidia kuonekana bora mbele ya jopo la wataalamu wa COSAFA.

Lakini Mduda baada ya kudaka vizuri ndani ya dakika 90 tu dhidi ya Lesotho na kuiongoza Stars kushinda kwa penalti 4-2 na kushika nafasi ya tatu, amekuwa kipa bora wa mashindano ya 2017.

Mduda alipangua penalti ya Nahodha wa Mamba, Thapelo Mokhehle kufuatia Sera Motebang kugongesha mwamba wa kulia mkwaju wake na kurudi uwanjani.

Waliofunga penalti za Lesotho ni Hlompho Kalake na Tsoanelo Koetle wakati Shiza Kichuya aligongesha mwamba wa juu penalti ya kwanza ya Tanzania, kabla ya Nahodha Himid Mao, Simon Msuva, Abdi Banda na Raphael Daudi kumtungua kipa wa Mamba Samuel Ketsekile kuipatia Taifa Stars ushindi mzuri wa 4-2.

Kutokana na ushindi huo, Tanzania ilipata dola za Kimarekani 10,000 zaidi ya Sh. Milioni 22 kwa fedha za nyumbani, wakati Lesotho wamepata dola 8,300.

Historia inaonyesha mwaka 2012 Simba SC ndiyo iliyomponza Mduda kufukuzwa katika klabu ya Yanga baada ya kumfunga mabao manne ndani ya dakika 45 za kipindi cha pili Mei 6, mwaka huo katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Wekundu hao wa Msimbazi wakishinda 5-0.

Siku hiyo, Mganda Emmanuel Okwi alifunga mawili dakika ya pili na ya 62, mengine matatu yakifungwa kwa penalti na Felix Sunzu dakika ya 56, Juma Kaseja dakika ya 67 na Patrick Mafisango dakika ya 72.

Mduda anakwenda kufanya idadi ya makipa watatu Simba baada ya Manula na Emmanuel Mseja aliyesajiliwa kutoka Mbao FC, kufuatia wote wa msimu uliopita Mghana Daniel Agyei na wazalendo Peter Manyika na Dennis Richard kutemwa.

By Hamza fumo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents