Habari

Usajili wa daladala sasa kwa kampuni tu

KATIKA hatua mpya ya kudhibiti usafiri wa abiria nchini, Mamlaka ya
Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), umeandaa
mapendekezo ya kisheria ambayo sasa daladala zitakuwa zikisajiliwa kwa
kutumia kampuni na si mtu binafsi.

Na Mwandishi Wa Mwananchi

KATIKA hatua mpya ya kudhibiti usafiri wa abiria nchini, Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), umeandaa mapendekezo ya kisheria ambayo sasa daladala zitakuwa zikisajiliwa kwa kutumia kampuni na si mtu binafsi.

Chini ya utaratibu huo, usajili wa daladala utafanywa kama ilivyo kwa mabasi makubwa yaendayo mikoani.

Hata hivyo, mpango huo hautanyima haki watakaotaka kusajili gari moja moja lakini kampuni itakayosajili magari kila moja litakuwa na leseni yake maalumu.

Meneja mawasiliano wa Sumatra, David Mziray, alilithibitishia Mwananchi wiki hii kuhusu mapendekezo hayo.

Kuanzishwa kwa mpango huo, kutafanya wamiliki wa makampuni yatakayosajili daladala kuweza kuajiri madereva na makondakta kama yanavyofanya mabasi ya mikoani.

Mpango wa kuajiri madereva na mkondakta wa daladala umekuwa ukijadiliwa kwa muda mrefu kama hatua ya kufanya shughuli za usafirishaji abiria katika miji kuwa ya kisasa na yenye kuzingatia sheria na kuondoa wapigadebe ambao wamekuwa kero kwa wasafiri.

Kwa upande wa wamiliki, madereva na makondakta wa daladala maarufu kama vipanya, mapendekezo hayo kama yakipita na kuingia katika sheria ya utoaji leseni ya usafiri, yatakuwa na faida hiyo ya kutoa ajira lakini pia yatakuwa ni machungu kwani nyingi zitakuwa nje ya miji.

Kwa muda mrefu kumekuwa na mpango wa kuondoa vipanya kutoka katikati ya miji na kuvipeleka nje ili kuruhusu mabasi makubwa yenye uwezo wa kubeba abiria wengi zaidi kwa wakati mmoja.

Daladala maarufu kama vipanya zimekuwa zikichukuliwa kama chanzo cha msongamano wa magari katika barabara za miji mikubwa likiwamo jiji la Dar es Salaam.

Vyenyewe pia vimekuwa vikiendeshwa na madereva wasiokuwa na ajira huku baadhi wakiwa hawana leseni za udereva kutoka vyuo vya serikali kama kile cha taifa.

Akizungumzia zaidi mapendekezo hayo, Mziray alisema kwa sasa upo ugumu wa kufuatilia daladala zinazokiuka sheria kutokana na kwamba usajili wake umefanywa kwa watu wengi.

Mziray alifafanua kwamba, ni rahisi kwa mamlaka kuweza kudhibiti kampuni itakayokiuka sheria na taratibu za uendeshaji.

“Ni kweli mapendekezo yapo, unajua kama kampuni moja ikipewa leseni kwa kuwa na mabasi 20, inakuwa rahisi kuweza kusimamia utekelezaji sheria kuliko sasa ambapo usajili hufanyika kwa mtu mmoja mmoja,” alifafanua Mziray.

Kwa sasa mapendekezo hayo tayari yamekwishaandaliwa na yanasubiriwa kuandaliwa muswada ili upelekwe bungeni kupitishwa kuwa sheria.

Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliagiza mwanzoni mwa mwaka huu viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kutafuta mbinu za kuondoa msogamano wa magari katikati ya jiji.

Hata hivyo, jitihada za kuwaondoa wapigadebe katika maeneo ya jiji zimeshindikana kutokana na askari wa jiji kuzidiwa nguvu na wapigabege.

Hivi sasa jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kuwa na jumla ya daladala 6,000 ambazo zinafanya kazi katika maeneo mbalimbali.

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents