Michezo

Usajili wa Emmanuel Okwi wazuiwa Yanga

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesimamisha usajili wa mshambuliaji Emmanuel Okwi kutoka Uganda katika timu ya Yanga wakati likisubiri ufafanuzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
okwi

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana leo imesimamisha usajili huo baada ya kubaini kuwa Okwi aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali maalumu kutoka FIFA.

Okwi ambaye aliingia mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia aliruhusiwa na FIFA kuchezea SC Villa kwa kibali maalumu (provisional permit) cha miezi sita ili kulinda kiwango chake wakati suala lake dhidi ya Etoile du Sahel likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa.

Katika FIFA kuna kesi tatu kuhusiana na suala la mchezaji huyo. Wakati Okwi ameishitaki klabu hiyo FIFA kwa kutomlipa mshahara, Etoile du Sahel imemshitaki mchezaji huyo kwa utoro. Nayo Simba imeishitaki Etoile du Sahel kwa kushindwa kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola za Marekani 300,000.

Hivyo, TFF imeiandikia FIFA kutaka kujua iwapo mchezaji huyo anaweza kucheza Ligi nchini Tanzania wakati Etoile du Sahel ikiwa imefungua kesi katika shirikisho hilo la kimataifa ikidai Okwi bado ni mchezaji wake.

Source:BBC

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents