Habari

Utata Chuo Kikuu Dar

WAKATI vinara wa mgomo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wakifanya kila njia kuhakikisha kuwa wanafunzi wanarudishwa chuoni haraka iwezekanavyo

na Lucy Ngowi

 

 

 

WAKATI vinara wa mgomo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wakifanya kila njia kuhakikisha kuwa wanafunzi wanarudishwa chuoni haraka iwezekanavyo, uongozi wa UDSM, jana ulilazimika kuchukua hatua za haraka kudhibiti wimbi la wanafunzi ambao walianza kukusanyika chuoni hapo.

 
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika zilizopatikana chuoni hapo, uongozi wa chuo ulilazimika kuchukua hatua hiyo, baada ya wanafunzi wengi kukusanyika kufuatia taarifa zilizoandikwa na gazeti moja la kila siku (si Tanzania daima), kuwa masharti ya kuwawezesha kurejeshwa masomoni yamelegezwa.

 
“Habari ile iliwapotosha, wakaanza kukusanyika na hali ikaanza kuwa kama vile wakati wa mgomo, tukalazimika kutafuta njia ambazo zitatuwezesha kukabiliana na hali hiyo,” alisema mmoja wa viongozi waandamizi wa chuo hicho ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini.

 
Tanzania Daima ilishuhudia wanafunzi hao wakiwa wanajikusanya katika ofisi za usajili chuoni hapo, huku wengine wakisongamana katika ofisi za serikali ya wanafunzi (DARUSO), kwa lengo la kupata uhakika wa masharti yaliyolegezwa.

 
Hali hiyo iliulazimisha uongozi wa UDSM kutoa tangazo lililowatahadharisha wanafunzi hao kutoonekana katika eneo hilo hadi hapo taratibu za kuwarejesha chuoni zitakapokamilika.

 
Habari zilizothibitishwa na viongozi waandamizi wa chuo zilibainisha kuwa, licha ya kutoa tangazo hilo ambalo lilibandikwa katika mbao za matangazo na kuta za majengo, pia ujumbe huo ulisambazwa kwa njia nyingine zikiwemo kutumia magari yenye vipaza sauti.

 
Aidha, askari wa chuo walikuwa na kazi ya ziada kusambaza ujumbe huo kwa maneno na kuwaeleza wanafunzi waliokuwa wameanza kukusanyika, waondoke bila kuleta rabsha.

 
“Tunashukuru kuwa walituelewa na wakaondoka na sasa hali ni shwari,” alibainisha kiongozi huyo mwandamizi wa UDSM.

 
Ilani hiyo iliyotolewa kama tahadhari, iliyotolewa na uongozi wa chuo jana, ilisema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mwanafunzi yeyote aliyesimamishwa ambaye ataonekana katika maeneo ya chuo.

 
Tangazo hilo lililotolewa na Ofisa Uhusiano wa UDSM, lilisema kuwa, wanafunzi wote waliosimamishwa hawaruhusiwi kuonekana chuoni hapo hadi hapo taratibu za kuwarudisha zitakapokamilika.

 
Tanzania Daima ilifika katika eneo hilo la chuo jana asubuhi na kuwakuta baadhi ya wanafunzi wakisoma tangazo hilo. Wanafunzi hao walitii amri hiyo na kuonekana wakiondoka mmoja mmoja na wengine kwa makundi kama walivyokuja.

 
Tanzania Daima ilishuhudia askari wa chuo hicho wakifanya kazi ya ziada ya kueleza wanafunzi hao kwa mdomo kuwa hawaruhusiwi kuwepo katika eneo hilo.

 
Hali iliyojitokeza jana, iliwaacha wanafunzi wengi njia panda, wasielewe nini cha kufanya kwani walikwenda wakiwa na matumaini kuwa watarejeshwa chuoni ili waweze kuendelea na masomo.

 
Imebainika kuwa, wengi wa wanafunzi waliokuwa wakionekana katika eneo la chuo hicho, ni wale wasio na uwezo wa kulipa asilimia 40 ya gharama ambazo hazilipiwi na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

 
“Kuandika barua si tatizo, tatizo kubwa ni jinsi ya kupata hizo asilimia 40,” alisema mmoja wa wanafunzi wakati akijadiliana na wenzake.

 
Wengi wa wanafunzi hao wameonyesha kukata tama, wakisema familia zao hazina uwezo wa kulipa asilimia 40 pamoja na fedha za matibabu kiasi cha sh 100,000 kama moja ya sharti la kukubaliwa kurejea chuoni.

 
Taarifa nyingine ambazo hazikuthibitishwa zinaeleza kuwa, kuna wanafunzi wengine baada ya kufukuzwa, wameshindwa kurejea majumbani kwao kwa kuwa wazazi wao walishawapatia fedha hizo asilimia 40, lakini wao wakazitumia kwa mambo mengine.

 

“Inasemekana kuna wazazi wengine walishatoa hiyo pesa ila watoto wao wakazila. Shida imekuja pale waliporudishwa… wameshindwa kurudi majumbani kwao, hivyo wamekuwa wakionekana katika baa maarufu zilizoko eneo la Sinza,” alisema mmoja wa maofisa wa chuo kikuu ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji.

 

Alipofuatwa atoe ufafanuzi juu ya mchakato wa kuwashughulikia wanafunzi waliosimamishwa, Ofisa Uhusiano wa UDSM, Julius Saule alisema kuwa kwa sasa hana cha kuzungumza.

 
“Waandishi tunasema hatufungui mdomo. Hatuna cha kueleza zaidi,” alisema Saule.

 

Wakati hayo yanatokea, uongozi wa DARUSO, umekuwa ukihaha kutafuta mbinu za kuishinikiza serikali ikubaliane na madai yao, na pia kuushinikiza uongozi wa UDSM kuwarejesha chuoni wanafunzi bila masharti magumu yaliyotangazwa.

 
Hata hivyo, mambo yanaonekana kuwa magumu kwao kwani kwa muda mrefu, wameshindwa kutoa kauli yoyote, licha ya kuahidi mara kadhaa kufanya hivyo.

 
Wanafunzi hao wamefikia hatua ya kuzima simu zao, na imekuwa shida kupatikana ili kutoa ufafanuzi kwa nini wamekuwa wakiahirisha mikutano na waandishi wa habari ambayo wamekuwa wakiipanga.

 
Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents