Burudani

Utoaji wa elimu ya Ujasiriamali maeneo ya Buguruni umenitia moyo

Elimu ni popote kwani ni kuhakikisha ufahamu unaongezeka miongoni mwa jamii zetu kwa ajili ya matokeo bora zaidi katika maisha ya mtanzania.

DarEsSalaam-Buguruni

Nimeshazoea kupita mtaani na matangazo ninayoyasikia ni kuhusu starehe au matamasha, mikutano ya dini au siasa na mara chache sana nimeweza kusikia mtu akipita kwenye gari akitangaza kuhusu elimu ya ujasiriamali na kuhamasisha watu wahudhurie mafunzo hayo kwa kuwafuata mtaani na matangazo ya sauti.

Kwangu mimi bila kujali watafundishwa nini bali waliofanya jitihada hiyo wana uelewa fulani labda kwa kuwanufaisha wananchi au vinginevyo ila ni kitu ambacho kinatia moyo.

Wananchi wengi wanauelewa mdogo sana kuhusu ujasiriamali ingawa ni kitu wanachokifanya kila siku, hivyo kujikuta wakifanya mambo kama kawaida. Tunahitaji mtu au watu watakaoweza kusaidia kuwakomboa wananchi na si kwa kuwapa fedha bali kuwaongezea ufahamu na uelewa wa kile ambacho wanakifanya ili waweze kutoka hapo walipo.

Maendeleo kwenye jamii yanakuja kwa kubadilisha ufahamu wa mambo na kuboresha uelewa wa vitu, kwa muda mrefu tumekuwa tukifanya vitu kawaida na kutegemea matokeo bora zaidi.

Mtu asipoweza kubadili fikra zake hata ukimpa hela nyingi kiasi gani hatoweza kuzisimamia ataishia kufanya vitu ambavyo si sahihi na maranyingine kurudi kule kule alikotoka. Hiyo haiitaji muujiza kujua bali pale ambapo tukiweka msisitizo wa kielimu kwenye mfumo rasmi na usio rasmi tutaweza kutoka hapa kuelekea sehemu nyingine bora zaidi.

Kwa wale ambao wanakumbuka vijijini wakati wa elimu ya watu wazima ulipunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya watu waliokuwa hawawezi kusoma na kuandika, kwa sasa tunahitaji elimu nyingine ya kututoa hapa tulipo ili kuendana na mazingira na wakati tuliopo na hilo si jukumu la serikali peke yake bali mimi na wewe ambao tumeelimika kwa kiasi fulani tunasaidiaje jamii inayotuzunguka?

Awali Mwaisanila

A Personal Career Development specialist, passionate about empowering emerging generations of student, graduates and working class.

Related Articles

Leave a Reply

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents