Uturuki: Fahamu sababu za Rais Erdogan kutishia kuwaachia wakimbizi zaidi ya milioni 3 kuingia Ulaya
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameishambulia jumuiya ya Kimataifa kwa kuikosoa operesheni ya nchi yake kaskazini-Mashariki mwa Syria na kutishia kuwaachia mamilioni ya wakimbizi wakisyria waingie Ulaya.
Akiwahutubia wanachama wa chama chake cha haki na maendeleo AKP mjini Ankara,rais Erdogan amesema Ikiwa Ulaya itaitaja operesheni yake hiyo kuwa ni uvamizi, watafungua milango na kuwaachia wakimbizi milioni 3.6 waelekee Ulaya.
Operesheni ya kijeshi ya Uturuki iliaoanzishwa dhidi ya wanamgambo wakikurdi juzi Jumatano imekosolewa na washirika wake wa Magharibi ambapo Umoja wa Ulaya imeitolea mwito Uturuki kusimamisha mashambulizi yake.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha DW, Erdogan amesema wanajeshi wa nchi yake wameshawauwa jumla ya kile alichokiita magaidi 109 na kuongeza kusema kwamba serikali yake inataka kuepusha kuundwa kwa dola la kiislamu kwenye maeneo ya mipaka yake.