Michezo

Uwanja wa Uhuru kufungwa

 

Mashabiki wa soka jijini Dar es Salaam wameshangazwa na uamuzi wa kuufunga kwa muda Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kwa ajili ya ukarabati ambao utawakosesha utamu wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa miezi mitatu.

Serikali imetangaza  kuufunga uwanja  huo ambao pia hutumika kwa shughuli za kimataifa kama gwarida na kuapishwa kwa viongozi wa kitaifa kama rais ili kuufanyia marekebisho.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini, Leonard Thadeo alisema serikali imeshatuma taarifa kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF) na watumiaji wengine wa uwanja huo kuhusu kufungwa kwake kwa ajili ya matengenezo hayo.

Thadeo alisema michezo yote ilitakiwa kusimamishwa tangu wiki iliyopita, lakini kutokana na kuchelewa kwa taarifa waliwaruhusu TFF kutumia uwanja huo kwa ajili ya mechi za ufunguzi wa ligi mwisho wa wiki.

Alisema marekebisho ya uwanja yatachukua muda mfupi au utachelewa kidogo kutegemea na upatikaji wa fedha za utegenezaji huo.

“Siwezi kusema ni muda gani uwanja wa Uhuru utakuwa umefungwa hiyo itategemea na upatikanaji wa fedha iliyowekwa kwa ajili ya kazi hii, lakini itakuwa si chini ya miezi mitatu au pungufu ya hapo,” alisema Thadeo.

Thadeo alifafanua kuwa gharama halisi za ukarabati  huo zitatangazwa baadaye. Alitaja maeneo ambayo yatafanyiwa ukarabati mkubwa ni pamoja na jukwaa kuu, jukwaa la kijani pamoja sehemu yote ya mzunguko.

“Baadhi ya maeneo ya uwanja huo si salama kwa watu wanaojitokeza uwanjani hapo kwa ajili ya kushudia shughuli mbalimbali za michezo uwanjani humo,” alisema.

Hata hivyo, taarifa hiyo inaonekana kama bado haijawafikia viongozi wa klabu nne kubwa za jiji hili zinazotumia uwanja huo kama uwanja wao wa nyumbani.

Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema amekuwa akisikia tetesi za kuwepo kwa jambo hilo, lakini bado hajapokea taarifa rasmi kutoka kwa TFF.

“Hatujapokea taarifa yoyote zaidi ya kusikia kutoka kwa mashabiki, tunalifuatilia jambo hilo kutaka kujua ukweli wake, punde tutakapopokea barua kutoka TFF, tutachukua uamuzi wapi tutapokwenda kuchezea,” alisema Mwalusako.

Kauli kama hiyo ilitolewa na afisa habari wa Simba, Cliffford Ndimbo, ambaye alisema kama watapokea taarifa kutoka kwa TFF, basi watakuwa hawana jinsi zaidi kukaa na kamati kuu na kuamua kutafuta uwanja.

Nao uongozi wa African Lyon ulisema hauwezi kuzungumzia lolote kuhusu hilo kwa sababu bado hajapokea taarifa rasmi.

Ofisa habari wa TFF, Florian Kaijage alisema hawezi kutuma taarifa yoyote kuhusu jambo kwa sasa shirikisho hilo ni kama mteja tu wa uwanja huo.

Taarifa iliyoifikia Mwananchi ilisema jana kuwa klabu zote tano zinazoutumia uwanja huo zitalazimika kutafuta uwanja mwingine katika mikoa ya jirani kama vile Jamhuri ulioo Morogoro, Mkwakwani Tanga au Sheikh Amri wa mjini Arusha kwa ajili ya michezo yao ya kipindi hicho.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa Uwanja wa Taifa utatumika kwa mechi za timu ya taifa kwa ajili ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika  pamoja na mchezo wa Yanga na Simba pekee.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents