Siasa

Vibarua Bandarini wacharuka

Zaidi ya vibarua 1,500 wa Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) jana walifunga milango ya ofisi za mamlaka hiyo na kuzuia mtu yeyote kuingia wala kutoka nje wakipinga kufukuzwa kazi.

Na Godfrey Monyo

 
Zaidi ya vibarua 1,500 wa Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) jana walifunga milango ya ofisi za mamlaka hiyo na kuzuia mtu yeyote kuingia wala kutoka nje wakipinga kufukuzwa kazi.

 

Vibarua hao walifikia hatua hiyo baada ya kuambiwa kwamba hawahitajiki tena kwani kazi zao zitakuwa zinafanywa na makampuni binafsi baada ya kitengo chao kubinafsishwa.

 

Toka asubuhi hadi mchana walishinda nje ya lango kuu la kuingilia ndani ya ofisi za mamlaka hiyo zilizopo Barabara ya Bandari.

 

Katika sakata hilo Mkuu wa wilaya ya Temeke, Bw. Abdallah Kihato, jana aliokolewa na polisi baada ya vibarua hao kumsonga kwa madai kuwa anawapa majibu ya kisiasa.

 

Wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali vibarua hao kutwa nzima ya jana walikuwa wakiimba nyimbo za kuhamasishana ili kuendelea kudai haki zao.

 

Baadhi ya mabango yalisema, Mkurugenzi wa PTA unamtia aibu Rais Kikwete, Tumechoka kuburuzwa, Rais Kikwete tuambie kama hizi ndizo ajira milioni moja ulizoahidi wananchi, na viongozi wa TPA ni wezi na waonevu.

 

Mmoja wa vibarua hao, Bw. Mbaraka Said alisema, wamefanyakazi kama vibarua wa bandari muda mrefu.

 

Alisema baadhi yao wamefanya kazi kuanzia miaka mitano hadi 14.

 

Alisema sakata hilo lilianza juzi ambapo walipofika asubuhi waliambiwa kwamba kuanzia siku hiyo hakuna kazi bila ya kupewa maelezo zaidi.

 

Bw. Saidi alisema, wanachotaka ni kulipwa angalau kifuta jasho kwa sababu PTA imewatumikisha muda mrefu na kwamba kuwaondoa hivi hivi ni uonevu mkubwa.

 

Aliongeza kuwa walikuwa wakifanya kazi mbalimbali zikiwemo za kupakua shehena za mizigo zinazoletwa na meli pamoja na shughuli nyingine wanazopangiwa kwa siku.

 

Naye kibarua mwingine, Bw. Mbaga Malisa alisema, siku za kawaida walikuwa wakilipwa Sh. 5,000 mwisho wa wiki Sh. 10,000.

 

Bw. Malisa alidai kwamba kufukuzwa kwao kwa maelezo kuwa makampuni binafsi ndio yatakayoleta vibarua ni mbinu za viongozi wa PTA kwani kampuni hizo ni mali zao wenyewe.

 

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kikao cha menejimenti na wawakilishi wa vibarau hao, Mkuu wa wilaya, Bw. Kihato alisema, atahakikisha suluhu inapatikana ndani ya siku tatu.

 

Hata hivyo, alisema uongozi wa PTA umemwambia kuwa wao hawana kitu chochote cha kuwalipa kwani watu hao walikuwa ni vibarua.

 

Makampuni yaliyopewa kazi hiyo ni Tondoma, Nagla Shipping Services, Evans Manyasco, Mackbin na Organized Labour Pull.

 

Mkurugenzi wa PTA, Bw. Mgawe alikataa kuzungumzia suala hilo na kuendelea kujifungia ndani mpaka waandishi walipoondoka.

 

Hadi waandishi wa habari wanaondoka eneo la tukio sa 10:00 jioni bado vibarua hao walikuwa wamejikusanya nje ya lango la kuingilia ndani ya ofisi za PTA.

 

Wafanyakazi wa PTA waliokuwa ndani walizuiwa kutoka nje, jambo lililowalazimu kuruka ukuta na waandishi wa habari walitolewa nje kwa msaada wa polisi.

 

Naye Simon Mhina anaripoti kwamba Wafanyakazi wa viwanda vikubwa vya Steel Masters na Murzah Soap and Detergents Ltd, vyote vya jijini Dar es Salaam, jana walifanya mgomo mkubwa uliofuatiwa na maandamano, wakipinga hatua ya viongozi wao kupuuza ongezeko la mishahara.

 

Katika Kiwanda cha Steel Master kinachotengeneza bidhaa zote zinazotokana na vyuma, wafanyakazi wapatao 300, walikusanyika kwenye lango kuu na kutangaza mgomo.

 

Wafanyakazi hao, walisema katika hali ya kusikitisha uongozi umeamua kuwalipa Sh. 80,000 kwa mwezi badala ya Sh. 150,000 kama sheria inavyotaka.

 

Muda wote wakiwa nje ya kiwanda hicho, wafanyakazi hao walikuwa wanatoa sauti za kulaani uongozi huo, kwa kutowajali huku ukipuuza maagizo kadhaa ya serikali.

 

“Wametuambia kwamba tujaze fomu ya kukubaliana na mshahara huu mpya ambao hautoshi, kibaya zaidi wametutisha kwamba mfanyakazi ambaye hatotaka kusaini mkataba mpya aondoke… Hili ni kosa na uonevu mkubwa,“ alisema.

 

Baada ya malalamiko hayo, wafanyakazi hao, walianza maandamano makubwa kuelekea kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Abbas Kandoro.

 

Hata hivyo, baada ya kufika kwa Mkuu wa Mkoa walisema hawakuridhishwa na majibu waliyopewa, hivyo wakaamua kuendelea na maandamano yao kuelekea kwa Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana Bw. John Chiligati huku magari mawili ya polisi yaliwafuatilia kwa nyuma.

 

Kundi la wafanyakazi hao lilipofika makutano ya Barabara ya Shaurimoyo na ile ya Nyerere, kundi la askari polisi liliwazuia na kuwaeleza kwamba walichokuwa wanafanya ni sawa na maandamano yasiyo na kibali.

 

Alipoulizwa juu ya sakata hilo, mmoja wa maafisa wa Kiwanda hicho aliyejitambulisha kwa jina moja la Kanjan alikiri kuwaelekeza wafanyakazi kujaza fomu hizo.

 

Hata hivyo, alisema fomu hizo hazina matatizo yoyote kwa vile zililenga kuwapa taarifa za kuongezewa mshahara.

 

Naye Waziri Chiligati alilimbia gazeti hili kwa njia ya simu kwamba matatizo ya wafanyakazi hao yatashughulikiwa na Idara ya Usuluhishi na Maamuzi ambayo iko chini ya Wizara yake.

 

Katika Kiwanda cha Murzah Soap, wafanyakazi walianza mgomo kwa kufunga milango na kuweka mabango nje ya kiwanda hicho, wakilaani tangazo la uongozi la kutowalipa mshahara uliotangazwa na serikali .

 
Kufuatia hali hiyo Polisi walifika katika kiwanda hicho kilichopo maeneo ya Buguruni na kufanya mazungumzo na uongozi.

 

Hata hivyo baada ya kuona hakuna uharibifu wowote, polisi hao waliondoka katika eneo hilo.

 

Moja ya mabango yaliyowekwa kwenye lango kuu, lilikuwa likilaani hatua ya uongozi kuwalipa Sh. 850 kwa siku.
Nipashe lilielezwa kwamba uongozi umetimka kiwandani hapo baada ya sakata hilo kuanza.

 

Naye Joseph Mwendapole anaripoti kwamba Serikali imesema waajiri katika sekta binafsi ambao hawawezi kulipa viwango vipya vya mishahara wafunge makampuni yao.

 

Aidha, imewataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi kutoa taarifa kwa serikali endapo waajiri watakataa kulipa viwango vipya.

 

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Bw. John Chiligati, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

 

Alisema safari hii serikali haitakubali visingizio vya waajiri ambao wamekuwa wakiwanyonya wafanyakazi wao kwa kuwalipa kidogo.

 

“Nasema tutakuwa wakali na hatutakubali visingizio vya aina yoyote zaidi ya waajiri kulipa viwango vilivyotangazwa,“ alisema.

 

Alisema makampuni ya ulinzi yamekuwa yakiongoza kwa kuwalipa mishahara midogo wafanyakazi wake.

 

Bw. Chiligati, alisema wenye makampuni hayo wamekuwa wakitoa visingizio vingi kuwa hawana uwezo wa kuwalipa wafanyakazi wao.

 

“Wanasema hawawezi kulipa viwango vipya eti ni kiasi kikubwa mbona wakati ule wanawalipa mshahara wa Sh. 40,000 walikuwa wanaweza kukaa miezi mitatu hawawalipi?“

 

Alihoji.
Aliongeza kuwa kama wanaona hawana uwezo wa kutekeleza maagizo ya serikali wafunge makampuni yao na kwenda kufanya biashara zingine.

 

“Nilienda katika ubalozi mmoja, yule balozi akaniambia kwamba anailipa kampuni ya ulinzi Sh. 290,000 kwa kila mlinzi lakini wale walinzi waliniambia kuwa kila mmoja wao analipwa Sh. 40,000 tu. Nilishangaa sana,“ alisema.
Alisema huo ni unyonyaji mkubwa ambao serikali haitaendelea kuufumbia macho.

 

Kuhusu wafanyakazi kupunguzwa, Waziri Chiligati, alisema mwajiri anapoamua kupunguza wafanyakazi anapaswa kufuata sheria za kazi zilizopo na si kufanya anavyotaka.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents