Habari

Vibarua wa jengo la BoT wachanganyikiwa

VIBARUA waliokuwa wakishiriki ujenzi wa jengo la minara miwili la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wamelalamikia kupunjwa mafao yao baada ya kumalizika kwa mkataba wao wa ujenzi.

Na Mkombe Zanda

 

VIBARUA waliokuwa wakishiriki ujenzi wa jengo la minara miwili la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wamelalamikia kupunjwa mafao yao baada ya kumalizika kwa mkataba wao wa ujenzi.

 

Vibarua hao zaidi ya 80 waliokuwa wakifanya kazi chini ya Kampuni ya Ujenzi ya Group Five, jana asubuhi walizuiwa kuingia ndani ya eneo la benki linaloendelea kujengwa, kwa maelezo kuwa mkataba wao na mwajiri wao umemalizika.

 

Vibarua hao walilalamikia fedha walizotangaziwa kupewa na mwajiri wao kuwa ni kidogo na hazilingani na muda waliofanya kazi hiyo, pamoja na kutopewa mafao mengine wanayostahili kama pesa za muda wa ziada kazini.

 

Malalamiko ya vibarua hao walioanza kufanya kazi hiyo mwaka 2003, yamekuja siku moja baada ya Mbunge wa Karatu, Dkt. Wilbroad Slaa, kuipa Serikali siku 24 kuanzia Agosti 22 mwaka huu, kuwashughulikia wahusika wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha ndani ya benki hiyo.

 

Malalamiko ya vibarua hao yalitolewa kwa niaba yao na Mwenyekiti wa Umoja wao, Bw. Edward Alex (kadi namba 807206), Makamu Mwenyekiti, Bw. Ramadhan Saidi (kadi namba 803964) na Katibu wake, Bw. Charles Mangala (kadi namba 807409).

 

Viongozi hao walimweleza mwandishi wa habari hizi, kwamba uongozi wa kampuni hiyo umepanga kuwalipa mafao ya sh. 150,000 kwa mtu aliyefanya kazi kwa miaka minne, sh. 100,000 kwa aliyefanya kazi miaka miwili, sh. 50,000 mwaka mmoja na sh. 25,000 chini ya miezi minane.

 

Mbali na hayo, lakini pia Bw. Alex alisema utaratibu uliotumiwa na uongozi wa kampuni hiyo katika kumaliza nao mkataba, haukuwa sahihi na haukuzingatia misingi ya kibinadamu, kutokana na kuwazuia kuingia ndani bila taarifa za mapema kuhusu hatua hiyo.

 

Mwandishi wa habari hizi jana kuanzia saa 2:20 asubuhi alifika kwenye eneo hilo na kuwashuhudia vibarua hao wakiwa nje ya lango la kuingia kazini, kutokana na kuzuiwa na uongozi.

 

Uchunguzi wa mwandishi wa habari hizi, ulibaini kuwa hawakuwa na uwezo wa kuingia ndani ya eneo hilo kutokana na mamlaka husika kufuta kumbukumbu za vitambulisho vyao kwenye mitambo maalumu inayovitambua na milango kufunguka.

 

Kwa kawaida vibarua hao na mtumishi mwingine wa kampuni hiyo anapotaka kuingia ndani ya eneo hilo, hulazimika kupitisha kitambulisho kwenye mitambo maalumu milangoni ambayo hukitambua mlango kufunguka hivyo kumruhusu kuingia.

 

Jana asubuhi hali ilikuwa ni tofauti kwa vibarua hao, ambapo hakuna hata mmoja ambaye kitambulisho chake kilitambuliwa na mitambo hiyo na hivyo kushindwa kuingia ndani kuendelea na kazi.

 

Kutokana na hali hiyo, vibarua hao walisema hawajui hatima yao, kutokana na uongozi wa kampuni hiyo kutokuwa tayari kuwasilikiza ili kufikia muafaka wa suala hilo.

 

Hata hivyo, juhudi za mwandishi wa habari hizi kuonana na uongozi wa kampuni hiyo ili kupata ufafanuzi wa suala hilo hazikufanikiwa, baada ya kuzuiwa na walinzi wa kampuni ya Knight Support waliokuwa wakilinda mlango wa kuingilia ndani ya eneo hilo.

 

Walinzi hao walidai wamepewa amri ya kuhakikisha hakuna mwandishi anayeruhusiwa kuingia ndani ya eneo hilo.

 

Hata hivyo Msimamizi Mkuu wa shughuli za ujenzi kwenye jengo hilo aliyejulikana kwa jina mmoja la Daniel, alikiri kwa njia ya simu kuondolewa kazini kwa vibarua hao kwa sababu mkataba wao wa kazi umemalizika.

 

Bw. Daniel ambaye hakuwa tayari kubainisha jina lake la pili, alisema muda wa vibarua hao umemalizika kutokana na kazi walizokuwa wakifanya kumalizika.

 

Hata hivyo, alipotakiwa kueleza kwa nini vibarua hao wametengewa kiasi kidogo cha mafao ikilinganishwa na muda waliofanya kazi kwenye kampuni hiyo, alidai hahusiki na suala hilo.

 

Lakini pia alipotakiwa kueleza ni nani mhusika wa malipo ya vibarua hao, Bw. Daniel hakuwa tayari kutoa ushirikiano zaidi ya kumtaka Mwandishi wa habari hizi kwenda kuonana naye kwenye eneo hilo.

 

Pamoja na mwandishi huyo kufika katika eneo hilo kama walivyokubaliana, Bw. Daniel alikataa kukutana naye kwa sababu ambazo hazikuwa bayana.

 

Hadi Mwandishi wa habari hizi anaondoka kwenye eneo hilo saa saba mchana jana, vibarua hao walikuwa nao wameshaondoka kurejea nyumbani huku wakiwa hawajui hatima ya maslahi yao.

 

Ujenzi wa jengo hilo ambao umegharimu mabilioni ya fedha, umekuwa katika utata mkubwa kiasi cha baadhi ya wabunge kuhoji na kutaka kuwasilisha hoja binafsi.

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents