Michezo

Video: Algeria Vs Tanzania 1-1

Taifa, Taifa Stars wamefanya kazi nzuri na kuonesha mchezo wenye nidhamu baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji wao Algeria katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2012 juzi usiku.

Stars ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa kiungo wake Abdi Kassim ‘Babi’ kwa mpira wa adhabu ndogo umbali kadhaa toka eneo la penalti katika dakika ya 31.

Algeria walionekana kuutawala mchezo hasa katika dakika za mwanzoni za mchezo na nusura wakaribie kufunga kupitia kwa Ghezzal aliyeutuliza mpira wa adhabu ndogo kwa kisigino chake lakini shuti dogo alilopiga likatoka nje kidogo ya lango la Stars.

Dakika moja baadaye Ziaya alikaribia kufunga lakini shuti lake la karibu lilitoka nje ya lango baada ya kubanwa na mabeki wa timu ya taifa,Taifa Stars kabla hajaupiga mpira huo.

Algeria waliendelea kutafuta bao la kuongoza na walitawala sehemu ya kiungo lakini washambuliaji wake hawakuwa makini kumalizia nafasi walizopata.

Iliwachukua Taifa Stars mpaka dakika ya 18 kufanya shambulizi lake la kwanza kupitia kwa Mrisho Ngassa. Pamoja na shuti lake kushindwa kulenga goli, lakini wageni hao walianza kuonesha dalili za kucheza vizuri kwa kugongeana pasi za hapa na pale.

Katika dakika ya 31 Taifa Stars ilifanya shambulizi la kushtukiza na kusababisha mlinzi Adlene Guedioura kufanya madhambi nje ya eneo la penalti, ndipo Babi alipiga faulo hiyo iliyowapita mabeki wa Algeria waliojipanga vibaya na kwenda moja kwa moja upande wa kulia wa kipa Rais M’Bolhi na kujaa wavuni.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars Jan Poulsen amekimwagia sifa kikosi chake, “nimekuwa kocha wa Taifa Stars kwa karibu mwezi mmoja sasa, niliwaahidi Watanzania kwamba nitajenga timu yenye umoja na inayocheza soka safi, hicho ndicho tulichokiona leo Algeria” alisema kocha huyo raia wa Denmark baada ya mechi hiyo.

Matokeo hayo ni kikwazo kwa kocha mkuu wa Algeria Rabah Sadane ambaye amejiuzulu wadhifa huo baada ya kutoka sare na Stars.

Shirikisho la Soka la Algeria jana lilithibitisha kutokea kwa tukio hilo baada ya timu kupata matokeo ambayo hayakutarajiwa. Saadane amekuwa kocha wa Algeria kwa miaka mitatu na kuifanya ishiriki fainali za kwanza za Kombe la Dunia Julai Afrika Kusini baada ya miaka 24 kupita, lakini timu ilirudi nyumbani mapema na kuishia hatua ya makundi..

{youtube}-kdDHZSzH8Y{/youtube}

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents