Habari

Video: Majaliwa afichua madudu ya watumishi Ngorongoro

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefichua uhalifu uliofanywa na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na wa hifadhi za taifa, ambao walihongwa shilingi milioni 100 na kushiriki kumwiba kifaru maarufu aliyepewa jina la John kutoka hifadhi hiyo.

unnamed-62
Waziri mkuu akizungumza na watumishi wa hifadhi ya Ngorongoro (picha ofisi ya waziri mkuu)

Mbali na kufichua hayo alienda sambamba na kuwataja wahusika kwa majina yao huku akiagiza ifikapo kesho, apewe maelezo ya nini kilichotokea kwa mnyama huyo adimu ambaye kwa taarifa alizonazo amekufa akiwa hifadhi ya Serengeti eneo la Grumeti mkoani Mara.

Alitoa agizo hilo Jumanne katika ofisi za makao makuu ya mamlaka hiyo wakati akizungumza na watumishi pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafugaji ambapo ilikuwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha.

Wakati akiendelea na hotuba yake, ghafla alimsimamisha mmoja wa mtumishi wa NCAA, Cuthbert Lemanya ambaye ni Mkuu wa Kanda katika eneo la Kreta na kumuuliza “Faru John yuko wapi?” Kabla ya kupewa jibu, Waziri Mkuu akawasimamisha watumishi wengine wawili ambao ni Israel Noman, Patrice Mattey na kuwauliza, “Faru John yuko wapi? Yupo Kreta? “Nina taarifa zenu kuwa mliiba faru John Kreta na kumpeleka Grumeti Serengeti, Disemba 17, mwaka jana ambapo mliahidiwa shilingi milioni mia mbili, na badala yake mkapewa shilingi milioni mia moja.Na mmepata mgawo wa shilingi milioni mia moja halafu mnataka kusingizia kuwa amekufa, yupo wapi Faru John,” aliuliza tena Majaliwa.

Sambamba na kumuulizia faru huyo Waziri Mkuu alisema watumishi wengine waliohusika ni Meneja Utalii aliyemtaja kwa jina moja la Kileo ambaye awali aliletwa kutoka Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na kuja NCAA kwa ajili ya kusaidiana na wenzake kuiba faru John na baada ya hapo alihamishiwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambapo watumishi wengine walisema kuwa mtumishi huyo amehamishiwa hifadhi hiyo.

Aidha alimtaja mhifadhi mwingine kwa jina moja la Macha ambaye awali alikuwa hifadhi ya Mkomazi “Ninaagiza Kileo na Macha kwa pamoja warudishwe hapa mara moja waje kujibu Faru John yuko wapi,” alihoji Waziri Mkuu na kuongeza kuwa Faru John aliyeondolewa NCAA taarifa alizonazo sasa amekufa, hivyo anataka nyaraka zote zilizotumika kumuondoa NCAA vikiwamo barua za kila vikao vilivyokaa.

https://youtu.be/wiUD7ZykNUA

Waziri mkuu alitoa agizo kwa daktari aliyethibitisha kufa kwa faru huyo pamoja na kuagiza pembe zake kufikishwa kwake “Ninataka taarifa zote za faru huyo, barua za vikao vilivyokaa kuamua Faru John aondoke, pia nataka pembe zake ziletwe na taarifa ya daktari aliyeithibitisha kufa kwa faru huyo,” alieleza Waziri Mkuu na kuongeza: “Halafu Waziri wa Maliasili na Utalii, Jumanne Maghembe hata wewe walikudanganya, hukuwa unajua faru huyu alivyoondoka. Nahitaji taarifa hizi kabla ya Disemba 8, mwaka huu.”

Pia alimuagiza Mhifadhi Mkuu wa NCAA kumsimamisha kazi Mhasibu Mkuu, Sezzary Simfukwe kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha; na sasa anahojiwa na Takukuru.

“Kuanzia leo Mkurugenzi Mkuu wa NCAA nakuagiza usimamishe kazi hadi hapo uchunguzi utakapokamilika. Haiwezekani mtumishi awe anachunguzwa na Takukuru halafu aendelee kuwa ofisini atavuruga uchunguzi asimamishwe hadi taratibu zote zimalizike na hili sijawahi liona tangu naanza uongozi,” alieleza.

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents